Wednesday, 16 April 2014

MSEKWA ATOBO SIRI YA MUUNGANO

Wiki mbili kabla ya Tanzania kuadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa ametoboa siri ya Muungano huo akisema “mchakato wa kuundwa kwake ulifanywa kwa siri na haraka sana,” kutokana na upepo wa kisiasa na usalama wa kipindi hicho.

Akizungumza katika moja ya mfululizo wa vipindi vya miaka 50 ya Muungano vinavyorushwa na Redio ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC Taifa), Msekwa alisema woga wa hayati Abeid Amani Karume kupinduliwa na maadui, ulikuwa ni miongoni mwa sababu za kuharakisha Muungano huo.

Msekwa aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati Muungano unaasisiwa, alisema pia yeye na wenzake walichelewa kujua kwamba Mwalimu Julius Nyerere (Rais wa Kwanza wa Tanganyika) na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Karume walikuwa na majadiliano ya kuunganisha nchi hizo.

“Kikubwa cha kusema ni kwamba mazungumzo ya Muungano huo yalifanywa kwa siri.... kwa siri sana baina ya waasisi wa nchi hizo. Kwa nini yalifanywa kwa siri? Siyo kwa sababu walikuwa wababe, la hasha, bali kwa mazingira ya wakati ule, kulikuwa na maadui ambao wasingependa nchi hizi kuungana,” alisema Msekwa na kuongeza:

“Kwa woga huohuo, ndipo Mwalimu alipokubaliana na mwenzake wafanye mazungumzo ya siri mpaka waliposaini yale makubaliano na kunijulisha.”

Msekwa ambaye pia amewahi kuwa Spika wa Bunge la Muungano, alisema baada ya makubaliano ya Muungano, Nyerere alimwita na kumjulisha kuwa walishakubaliana (na Karume) kuungana, hivyo walihitaji baraka za Bunge kuridhia Muungano huo.

“Mwalimu akaniambia, ‘wewe Katibu wa Bunge unaweza ukawaita wabunge wakaja kwa harakaharaka kuridhia makubaliano?’

“Nakumbuka siku hiyo ilikuwa Jumanne na Mwalimu alipendekeza wabunge wafike Ijumaa ya juma hilohilo, nao wabunge wakaja wakaridhia.”

Simulizi hii ya Msekwa kuhusu Muungano imekuja wakati kukiwa na vuguvugu la muundo wa Muungano katika Bunge Maalumu la Katiba, kutokana na mapendekezo yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba kupendekeza serikali tatu badala ya Serikali mbili za sasa.

Bunge kuridhia

Aliongeza kuwa, baada ya Bunge la Tanganyika kuridhia Mwalimu Nyerere aliutaka muswada huo “kwa haraka sana”  ili aufanye kuwa sheria na alitaka kupelekewa kwa mkono.

“Baada ya wabunge kuridhia pale Karimjee, nikauchukua muswada na kuupeleka Ikulu, sio mbali pale.

“Mwalimu alifurahi sana, alishajua kuwa ulikuwa umesharidhiwa kwa sababu alikuwa anafuatilia mkutano wa Bunge kupitia redio, ukumbuke zamani hakukuwa na televisheni,” Msekwa anasimulia.

Sababu za kuharakisha

Msekwa alisema kulikuwa na sababu kuu mbili za kuharakisha Muungano; moja ni Mwalimu Nyerere kutaka nguvu ya Afrika itokane na miungano ya nchi, wakati Karume alitaka kuimarisha usalama wa Zanzibar miezi miwili baada ya kuuondoa utawala wa Sultani Januari 12, 1964.

Aliongeza kuwa Nyerere alikuwa amejifunza kutokana na makosa ya awali ambapo maadui waliharibu mpango wa kuziunganisha nchi za Afrika ya Mashariki na kuwa shirikisho.

Hata hivyo, Msekwa aliongeza kuwa, Mwalimu alimwambia Karume wangoje kwa muda, lakini kiongozi huyo wa Zanzibar hakuafikiana na wazo hilo kutokana na masuala yake ya kiusalama.

Alisema hata wakati Bunge la Tanganyika likiridhia muswada wa kuanzisha Muungano, tayari wenzao wa Zanzibar walikuwa wamekwishauridhia.

Muundo wa Muungano

Msekwa alisema suala la kubuni muundo wa Muungano ambalo linasumbua vichwa wajumbe wa Bunge la Katiba sasa, halikuwa tatizo kubwa wakati huo, japo Karume alimwomba Nyerere watengeneze Serikali moja.

“Karume alimtaka Mwalimu waunde serikali moja; yeye awe Makamu wa Rais na Nyerere awe Rais. Lakini Mwalimu hakutaka wazo hilo akihofia maadui wangesema ameimeza Zanzibar na pia alizingatia udogo wa nchi hiyo pamoja na hofu ya kuwa mkoloni mamboleo,” alisimulia Msekwa.

Msekwa alisema mara tu baada ya Nyerere kusaini muswada wa Muungano kuwa sheria, alianza kuunda Serikali ya Jamhuri ya Muungano na aliwachukua wajumbe 20 kutoka Zanzibar kuingia katika Bunge la Muungano.

Alisema baada ya Muungano huo hakukuwa na chokochoko zozote na hata maadui waliotaka kuipindua Serikali ya Zanzibar walikata tamaa.

“Hakukuwa na kitu kinachoitwa kero za Muungano mpaka pale Aboud Jumbe alipoingia madarakani baada ya kifo cha Karume 1972. Jumbe na wenzake walikuwa wanahoji Tanganyika tuliyoungana nayo ipo wapi?” alisema.

Mhifadhi mkuu apigwa risasi.

Mmoja wa viongozi wakuu wa uhifadhi wa wanyama pori barani Afrika Emmanuel de Merode, amejeruhiwa vibaya baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana katika moja ya mbuga kongwe barani afrika.

Bwana Merode,ambaye ni raia wa Ubelgiji ni mkurugenzi wa mbunga ya wanyama pori ya Virunga,ambayo ni makao ya Sokwe wanaokaa milimani katika Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo.Sokwe hao ni baadhi ya wanyama walio katika hatari ya kutoweka kutokana na kuwindwa sana.

Alipigwa risasi akiwa anaendesha gari kati ya eneo lililo kati ya makao makuu ya mbuga hiyo na mji wa Goma ambako amelazwa hospitalini.

Sababu ya kupigwa risasi kwa mhifadhi huyo haijajulikana, lakini makundi ya watu ambao hukata miti kiharamu, wawindaji haramu na waasi huendesha shughuli zao katika eneo hilo.

AAJABU YA DUNIA NA MABADILIKO YAKE. India kutambua waliobadilisha jinsia

Mahakama ya juu zaidi nchini India imetoa uamuzi wa kihistoria unaotambua watu waliobadilisha jinsia yao kama watu wa kawaida katika jamii.Kawaida kuna jinsia mbili, mke au mume lakini mahakama hiyo imesema kuwa watu wanaoamua kubadilisha jinsia yao kuambatana na hisia zao pia ni lazima watambuliwe na jamii na walio katika aina ya jinsia
kivyao.

Mfano wa watu kama hao ni mtu anayezaliwa kama mwanamke lakini anahisi kisaokolojia kuwa yeye ni mwanaume na hivyo hubadilisha jinsia yake na kuwa mwanamume kwa hata kufanyiwa upasuaji.

Uamuzi huu wa mahakama bila shaka ni wa kihistoria na unasema watu hao wasio jitambua kama wanaume au wanawake wanaruhisiwe na kutambulika kama wanavyotaka

Katika kitambulisho chao hawatajulikana kama wanaume au wanawake bali 'Transgender' kama jinsia ya tatu, sio wanaume wala wanawake.
"ni haki ya kila binadamu, kuchagua jinsia wanayoitaka,'' alisema jaji katika uamuzi huo ambao unawapa watu hao haki ya kujitambulisha kama wanaume au wanawake

Iliamuru serikali kuwapa watu hao nafasi za kazi na elimu kama jamii ya watu waliotengwa. Mahakama pia imeitaka serikali kuwapa huduma muhimu watu hao wanaochagua kujitambulisha watakavyo.Takwimu zinasema kuwa watu milioni mbili nchini India wamebadilisha jinsia yao.
Wanaharakati wanasema kwamba, watu hao wanatengwa na kuishi katika umaskini mkubwa na pia wanachukiwa kwa sababu ya kubadilisha jinsia yao.

Wengi hujikimu kimaisha kwa kuwa waimbaji , kuombaomba barabarani na kujihusisha na biashara ya ngono.Kadhalika wanaharakati wanasema kuwa watu hao hunyimwa huduma za matibabu hospitalini.''Watu hawa ni raia wa India na lazima waheshimiwe na kupewa nafasi ya kunawiri maishani,'' alisema jaji katika uamuzi wake."lengo la katiba ni kuhakikisha kila mtu wa India anapewa nafasi ya kuishi vyema na kujiendeleza.

Wanafunzi wa kike watekwa nyara Nigeria.


Polisi nchini Nigeria wanasema kuwa shule ya mabweni ya wasichana imeshambuliwa katika jimbo la Borno Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo huku wasichana wakitekwa nyara.

Wazazi wanasema kuwa zaidi ya wasichana miambili wametekwa nyara na washambuliaji hao.Washambuliaji wanaaminika kuwa wanachama wa kundi la wapiganaji wa kiisilamu la Boko Haram. Utekaji nyara huo ulifanyika usiku wa manane katika shule ya Chibok Kusini mwa mji wa Borno , karibu na mpaka na Cameroon.Inaarifiwa wasichana 300 walikuwa wanajiandaa kwa mitihani yao. Mmoja wa wasichana alifanikiwa kutoroka na aliambia BBC kuwa walikuwa wanalala wakati walipovamiwa na wanaume waliokuwa wamejihami.

Waliowashambulia wanaaminika kuwa wapiganaji wa kundi la Boko Haram.
Wanaume hao waliingiza magunia ya chakula katika malori yaona kuwaamuru wasichana kupanda lori hizo.Wasichana 15 walifanikiwa kutoroka baada ya lori walimokuwa kukumbwa na hitilafu.

Wakazi wa kijiji cha Chibok wanasema kuwa walisikia milipuko kadhaa huku nyumba 170 zikiteketezwa.Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa wanajeshi wawili waliuawa huku mali ikiharibiwa wakati wa shamblizi hilo mjini Chibok.

Mnamo siku ya Jumatatu, zaidi ya watu 70, waliuawa katika milipuko miwili ya mabomu katika kituo cha mabasi mjini Abuja.Kundi la Boko Haram pia limelaumiwa kwa kufanya shambulizi hilo.

Wanaume Vifua wazi marufuku Uingereza.


Wanaume wanaovua mashati wamepigwa marufuku kuitembelea bustani ya mapumziko na kujivinjari ya Adventure Island.
Ni eneo ambalo watu wanakwenda kujivinjari na familia zao, kwa kutazama wanyama, watoto hupata kubembea na pia watu huota jua.Bustani hiyo iliyopo mjini Southend nchini Uingereza, imeweka ilani zinazowaomba wanaume wasivue mashati yao, na kwamba watakao patikana watafukuzwa.
Mkurugenzi mkuu, Marc Miller, amesema anataka wanaume waonyeshe "ustaarabu".

Meli yenye watu 460 yazama Korea Kusini.



Oparesheni ya uokozi inaendelea kufuatia ishara za dharura zilizoripotiwa kutoka meli moja iliyobeba takriban abiria 460 katika pwani ya Korea Kusini.

Maafisa wanasema kuwa walinzi wa pwani hiyo wanatumia, meli za wanamaji wa Korea pamoja na ndege za uokoaji kuwaokoa watu waliokuwa katika meli hiyo.Shughuli zinaendelea hivi sasa kuokoa zaidi ya abiria 460 wa ferry hiyo .

Jeshi la wanamaji likishirikiana na maafisa wanaolinda usalama katika bahari ya rasi ya Korea wanasema watu wengi wamefanikiwa kuolewa.Maafisa wanasema walipokea habari kuwa meli hiyo imepata matatizo ikiwa imebeba idadi kubwa ya wanafunzi ikitoka Incheon iliyoko kwenye visiwa vya kifahari vya Jeju .

Waokoaji wamewanusuru tayari abiria 160 huku wengine waliosalia wakishauriwa waruke baharini iliwaokolewe.

Walioshuhudia wanasema kulisikika kishindo kikubwa kabla ya ferry hiyo kuanza kuzama zaidi ya kilomita 20 kutoka ufukweni.

Shughuli ya uokoaji bado inaendelea.

Tuesday, 15 April 2014

TheChoice: JUA SABABU 10 ZA WANAWAKE KUTOKUOLEWA NA KUISHIIA ...

TheChoice: JUA SABABU 10 ZA WANAWAKE KUTOKUOLEWA NA KUISHIIA ...: Pamoja na kuwa kuna wanawake husita kuolewa, lakini jambo hili si kubwa sana kwa wanawake kama ilivyo kwa wanaume. Kwa kiasi kikubwa ka...