Elizabeth John
SAFARI ya kupigania mafanikio ya kitu chochote yahitaji kujituma, kutokata tamaa kwa kile unachokitafuta na ndio maana kuna usemi kuwa mtafutaji hachoki na ikitokea akasema amechoka, ujue ameshafanikiwa.
Ndivyo ilivyo katika maisha ya mwanadamu katika kupigania hiki na kile iwe katika michezo, siasa, bishara, elimu na mengineyo; yahitaji uvumilivu mkubwa kutokana na changamoto kadha wa kadha zinazoweza kuibuka wakati wa kuyatafuta hayo mafanikio.Wengine hufananisha harakati za kusaka mafanikio ya maisha kwa ujumla na safari ndefu ambayo yaweza kuambatana na milima na mabonde kwa maana ya mitihani mingi ambayo mhusika hana budi kuitambua na kuivuka katika kufanikisha malengo yake.
Mchezaji wa soka Ally Abdallah, ni miongoni mwa chipukizi wenye malengo ya kufika mbali licha ya kukabiliana na matatizo mengi ambayo kwake anaona ni hali inayopaswa kuwepo katika harakati za kupigania mafanikio yake kwani lengo ni siku moja kuwa mchezaji wa mkubwa nchini ikiwemo kucheza soka nje ya Tanzania.
Anasema ili aweze kufanikiwa kuwa mchezaji wa kulipwa, amekuwa akijituma kwenye mazoezi ili kufikia kiwango cha kuchezea moja ya timu za Ligi Kuu Tanzania Bara ili aweze kuimarisha kipaji chake ikiwemo kupata uzoefu zaidi na siku moja aitwe kwenye kikosi cha timu ya Tanzania, Taifa Stars.
“Natamani siku moja nijiunge na timu ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara ili niweze kuboresha zaidi kipaji changu na kupata uzoefu zaidi kutoka kwa wachezaji mahiri ili niweze kufikia kiwango cha kuitwa Taifa Stars,” anasema kijana huyo anayechezea timu ya Night Stars ya Temeke.
Hata hivyo, anadokeza kuwa pamoja na juhudi zake kubwa dimbani, bado hajaonwa na timu kubwa akiamini ni kutokana na kukosa sapoti yoyote na kusema kwake hilo ndilo tatizo kubwa akiamini pamoja na juhudi za mchezaji, bado msaada huhitajika.
Changamoto
Ally anasema changamoto kubwa kwake ambayo inasumbua kichwa ni timu yake kushindwa kushiriki Ligi Daraja la Kwanza kwani hadi sasa bado ipo Daraja la Pili na kuongeza kuwa hiyo inamuuma sana hasa kuona wachezaji aliokuwa akicheza nao wakicheza Ligi Kuu.
“Roho inauma sana kuona watu ambao nilikuwa nacheza nao wamefika mbali, mimi bado nipo hapa,” anasema mchezaji huyo akimtaja Edward Chistopher ambaye kwa sasa anachezea Simba.
Anasema kama angekuwa na sapoti, naye leo hii angekuwa mbali kama ilivyo kwa wenzake ambao wanang’ara, lakini anasema hiyo kwake ni chachu ya kuzidi kujituma dimbani akiamini kila kitu kina wakati wake, japo kibinadamu angetamani awe mbali.
Ushauri
Anaisihi serikali ianzishe kituo kwa ajili ya kutafuta chipukizi wenye vipaji ambao watakuwa wanailetea ushindi timu hiyo katika mashindano mbalimbali ya kimataifa tofauti na ilivyo sasa ambapo timu hiyo imekuwa ikishindwa licha ya kupewa matunzo na maandalizi mazuri kutokana na uwepo wa wadhamini.
“Sio tunakuwa na wachezaji wachache wa timu ya taifa, wakati vipaji vipo vingi mtaani vikiachwa. Kiukweli mtaani kuna vipaji vingi sana na wengine wanakata tamaa ya kufanya mazoezi kutokana na kukosa hata kucheza mechi za kirafiki,” anasema.
Ally anawaomba wachezaji wenzake wafanye mazoezi kwa bidii bila kukata tamaa ikiwa ni pamoja na kushika mafunzo ambayo wanapewa na makocha wao.
“Inatakiwa usikate tamaa unapokata tamaa ya kuacha mazoezi kipaji chako kinaweza kikapotea na baadaye kushindwa kabisa kucheza vizuri,” anasema.
Historia yake
Nyota huyo aliyezaliwa Machi 27, 1988, wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam, ni mtoto wa tatu kati ya watano katika familia ya Mzee Abdallah Mhina yenye maskani yake Temeke.
Alisoma elimu ya Msingi katika shule ya Ruvuma, Chang’ombe jijini Dar es Salaam na kuhitimu mwaka 2002 na kusema akiwa shuleni, ndipo alijifunza kucheza soka akishiriki mashindano mbalimbali.
Mwaka 2001, alishiriki mashindano ya mkoa yaliyoshirikisha wanafunzi wenye umri wa miaka chini ya 14 ambapo ilikuwa ndio ligi ya kwanza kwake.
Mwaka 2006, alihitimu elimu yake ya sekondari katika shule ya Makongo, lakini matokeo hayakuwa mazuri, ndipo akaamua kujikita zaidi kwenye soka ambapo kabla ya kuichezea Night Star, aliwahi kucheza TP Vita ya Temeke.
“Mechi ambayo sitakuja kuisahau ni ile tuliyocheza na Super Politan; nilikuwa nahodha wa timu yetu ya TP Vita pamoja na ugumu wa mechi hiyo tulifanikiwa kushinda mabao 2-0,” anasema.
Anasema anatamani kuwa mchezaji mzuri kama Athumani Idd ‘Chuji’ kutokana na juhudi zake akiwa uwanjani na kumsababishia aipende timu ya Yanga kutokana na uwepo wa mchezaji huyo mashuhuri.
Nje ya soka, Ally anapenda muziki wa taratibu ‘RnB’ ambapo Tanzania anamkubali mkali wa muziki huo, Benard Paul ‘Ben Pol’.
Kwa sasa anafanya biashara kwa ajili ya kumpatia kipato cha kuendeshea maisha yake.
Kwa maoni na ushauri 0714321298 au lizzbeth87@yahoo.com
No comments:
Post a Comment