Maalim Seif Sharif Hamad ashutumiwa kuwa ni Mwanasiasa anayebadilika kama kinyonga
MAKAMU
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, ametajwa katika Bunge
Maalumu la Katiba, kuwa miongoni mwa viongozi wa mstari wa mbele
kupinga muundo wa serikali tatu mwaka 1984, huku akiwaita wanaoutaka
kuwa ni wahaini wanaostahili kuchukuliwa hatua.
Akichangia mjadala katika Bunge hilo jana, Mjumbe Muhammed Seif Khatib
alieleza namna Seif alivyokuwa akijitoa mhanga kutetea serikali mbili
kiasi cha kuiba nyaraka za Ikulu kuzima mtandao wa waliotaka serikali
tatu.
Khatib ametoa ushuhuda huo huku akinukuu maneno ya Seif kama yalivyokuwa
wakati akiwasilisha hoja za kutetea serikali mbili ndani ya kikao cha
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, mwaka 1984.
Alisema katika taarifa rasmi za NEC ya CCM, zinaonesha Seif akisema
amesikitishwa na kuumizwa sana na mbinu chafu za kutaka serikali tatu,
zinazofanywa na baadhi ya viongozi wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar
walipoelezea msimamo wa makubaliano ya serikali tatu, na kuhoji ukweli
wa jambo hilo.
Kwa mujibu wa Khatib, kauli hiyo ya Seif aliitoa alipokuwa akimtuhumu
aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, kwa kupanga njama za
kuanzisha muundo wa Muungano wa serikali tatu, kwa kushirikiana na
baadhi ya viongozi wenzake.
“Nataka niwarejeshe wabunge kwamba, Aboud Jumbe angefanikiwa na hoja
yake ya kutaka serikali tatu, leo hii tusingekuwa na mkutano huu,
hakufanikiwa kwa kuwa kiongozi mmoja wa CUF, Seif Sharrif Hamad,
alimsimamisha na hayo yamo kwenye taarifa sahihi za mkutano wa CCM,
Dodoma mwaka 1984,” alisema Khatib.
Khatib alinukuu kauli ya Maalim Seif: “Msimamo wa Jumbe umetufadhaisha
sisi sote, tunataka maelezo yake ni dhahiri hoja ya serikali tatu
haikuanzishwa na watu wadogo, imechangiwa pia na baadhi ya viongozi wa
Baraza la Mapinduzi na Aboud Jumbe ni chanzo cha hayo.
Kwa mujibu wa Khatib, taarifa hizo rasmi za CCM zinaonesha wazi kuwa
Seif alikuwa mstari wa mbele kuzuia serikali tatu, na kuwa mtetezi wa
serikali mbili, ambapo alijaribu kufanya kazi tatu.
Alitaja kazi ya kwanza aliyofanya Seif ni ile ya Uchunguzi, ya pili ya
Mwendesha Mashtaka, ya tatu Wakili CCM na aliwatuhumu watu wanne,
akiwemo Jumbe, Jamal Faki, Abuu Salim na Wolfgang Dourado, ambaye
alikuwa Mwanasheria Mkuu wa kwanza Zanzibar.
Seif kwa mujibu wa Khatib, aliwaita akina Jumbe kuwa ni wasaliti wa nchi
na aliamua kwenda kuwashitaki katika kikao cha NEC ya CCM, na kusema
wao wanataka serikali tatu hivyo wanastahili kuhukumiwa.
“Seif huyo alisema anasikitishwa sana na Dourado kusafiri kwake na
amekuwa akiukashifu Muungano na kudai sio halali, na kudai jeuri ya
Dourado ameipata wapi ya kusemea Wazanzibari na kudai ruhusa kapewa na
nani ya kwenda Ulaya,” alisema Khatibu akimnukuu Seif akitoa mashitaka
kwa Mwenyekiti wa CCM, wakati huo Mwalimu Julius Nyerere.
Khatib alisema Seif hakuishia hapo bali aliwashitaki watuhumiwa wote
kwenye Mahakama ya NEC na kuiomba iwahukumu watakaohusika na kuhitimisha
kuwa wanaotaka serikali tatu ni kinyume na matakwa yao na shabaha ya
malengo yao na hiyo inahatarisha usalama wa nchi, na kwamba ni vitendo
vya uhaini.
Khatib aliendelea kusema, kama hilo halikutosha, kwenye hotuba ya Rais
wa Zanzibar, Seif alituhumiwa kuwa ndiye aliyeiba waraka wa siri Ikulu
ya Zanzibar, ili kuzima mtandao uliokuwa umejipanga kuanzisha serikali
tatu.
Kwa mujibu wa Khatibu, Seif amelikiri kwenye kitabu cha Profesa Issa
Shivji na kusema alifanya hivyo kwa lengo la kutetea serikali mbili.
“Maalim Seif wa mwaka 1984 alikuwa mtetezi wa serikali mbili lakini
baada ya kufukuzwa kwenye chama mnamo Mei 13, mwaka 1988 saa nne usiku,
kuanzia hapo akawa mtetezi wa serikali tatu, Januari mwaka jana akaanza
kudai serikali ya Mkataba, huyo ndio Seif.
“Kwake yeye kudai serikali tatu kipindi hicho ilikuwa ni uhaini, leo je?
Hapa tunajifunza kwamba baadhi ya viongozi wa upinzani akiwepo Maalim
Seif ni kinyonga wakipita kwenye mvua wanafanana na rangi ya mvua,
baharini ni kama bahari akipita kwenye jua ni kama jua.
“Seif ni kinyonga, wananchi wawe macho kwani anabadilika kila mara awali
aliwashutumu wote waliotaka serikali tatu, akisisitiza ziwe mbili
lakini leo amebadilika tena anataka Mkataba,” alisema Khatibu.
Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Hamad Rashid Mohamed, alisema Seif ni
kiongozi hatari na kigeugeu ambaye awali alikuwa na msimamo wa serikali
tatu lakini sasa anasimamia Muungano wa Mkataba.
Hamad ambaye mbali na ujumbe wa Bunge Maalumu ni Mbunge wa Wawi kupitia
CUF, nafasi aliyorejeshewa na Mahakama baada ya kutaka kunyang’anywa na
chama chake, amesema mwaka 1992, uongozi wa CUF ulisimamia serikali tatu
lakini juzi Seif katika mikutano ya hadhara alisema msimamo wa chama
hicho ni Muungano wa mkataba.
“Tuangalie viongozi wanaobadilika badilika, mwaka 1992 msimamo wa CUF
ulikuwa serikali tatu, juzi serikali ya mkataba, anabadilika kila baada
ya dakika tatu, kiongozi wa aina gani huyu? “Mwaka 1984 Seif alitaka
serikali mbili, mwaka 1992 akiwa CUF msimamo ukawa Serikali tatu, juzi
mkataba, huyu ni kiongozi wa aina gani, ni wa kuwaongopea watu,”
aliendelea kusema Hamad.
Alisema wakati wakidai Katiba mpya, CUF na vyama vingine vya upinzani
viliandamana na kuwaingiza watu kwenye ulemavu, wajane na watoto,
wanafunzi walikosa masomo na leo badala ya kuhakikisha Katiba
inapatikana, wanahatarisha amani na kutaka mapinduzi tena.
Alihoji kati yake na Maalim Seif, msaliti ni nani kwani wakati wakiwa
wanatafuta serikali ya umoja wa kitaifa, walikutana sehemu mbalimbali
ikiwemo Dodoma na kuafikiana namna ya kuunda serikali hiyo, lakini
alishangaa wenzake watano akiwemo Seif walijifungia ndani, wakaja na
mkataba na kuhoji kama ni usaliti, nani msaliti wa wenzake.
“Tulienda kwenye kikao cha Halmashauri Kuu (wakati wakiwa CCM kabla ya
kufukuzwa) na ikapendekezwa Mwinyi (Rais Ali Hassan) agombee urais na
kwa vyovyote Maalim Seif awe Waziri Mkuu…kama haitoshi, wakati Idrisa
(Abdul Wakil) akiwa Rais, Seif aliendelea kuwa Waziri Kiongozi Zanzibar,
sasa Wazanzibari msaliti mnamfahamu?” alihoji Hamad.
Alisema yeye tangu mwaka 1982 yupo Tanzania Bara na kwamba uhusiano wake
na Bara si wa kawaida, ni wa kindugu wa damu na kusema kama kuna watu
wanasema yeye amekimbia, hakimbii mapambano wala hakimbii tendo la
kihistoria. “Mheshimiwa Mwenyekiti nilifiwa mimi, mtu wa kwanza kuja
alikuwa Kingunge Ngombale Mwiru (Mjumbe wa Bunge hilo) ndio wengine
wakafuata, undugu wetu si wa kawaida,” alisisitiza Hamad.
No comments:
Post a Comment