Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo,
HALI ya kiafya ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es
Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo, 70, aliyeadhimisha miaka 30
ya uaskofu hivi karibuni ni tete.Ilielezwa na baadhi ya watu walio karibu na kiongozi huyo kuwa kutokana na hali yake kuwa tete ilisababisha siku ya maadhimisho hayo Jumatano iliyopita ashindwe kushiriki katika maandamano ambayo yalishirikisha maaskofu na mapadri wa kanisa hilo katika Kanisa la Msimbazi jijini Dar.
Haijawekwa wazi kinachomsumbua kiongozi huyo anayeheshimika katika dhehebu hilo ndani na nje ya nchi lakini habari zinasema Kadinali Pengo hatakiwi kusafiri kwa umbali mrefu kwa kutumia barabara.
Katika sherehe hiyo ambayo pia alikuwa akiadhimisha miaka 43 ya upadri na miaka 16 ya ukadinali, kiongozi huyo aliingia na kutoka kwa kutumia mlango wa mbele na alipokea pongezi akiwa ameketi. Hakuna kiongozi yeyote aliyekuwa tayari kuzungumzia afya ya Kadinali Pengo siku hiyo.
Hata hivyo, Januari mwaka huu askofu msaidizi wa kanisa hilo jimboni humo, Mhashamu Titus Mdoe, alitangaza kuwa Kadinali Pengo ni mgonjwa na alitoa taarifa hiyo wakati wa misa takatifu iliyofanyika kwenye Kigango cha Nzasa, Parokia ya Temboni jimboni humo.
Mhashamu Mdoe hakutaja ugonjwa unaomsumbua Kadinali Pengo, lakini aliwataka Wakatoliki na watu wenye mapenzi mema, kuendelea kumuombea ili apate nafuu.
Alisema ugonjwa wa Kadinali Pengo unaweza kuchangiwa pia na hali ya kuelekea katika uzee, ingawa sababu hiyo haijafikia kuwa chanzo kikuu cha kumfanya augue. Katika misa iliyofanyika wiki iliyopita, Msimbazi, Dar, Pengo alisema:
“Ushirikiano ninaoupata na amani iliyopo ni matunda ya Mwenyezi Mungu. Kipindi nakuja Dar es Salaam, kulikuwa na parokia 20, lakini leo kuna parokia 79, ndoto yangu kabla Mungu hajanichukua nataka niache parokia 100 na hiyo itawezekana kwa ushirikiano wenu.”
Naye Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Tarcisius Ngalalekumtwa alimshukuru Kardinali Pengo kwa jitihada zake za kudumisha amani na usawa nje na ndani ya jimbo hilo. Pengo ni kadinali wa pili kutoka Tanzania, aliyeteuliwa baada ya kifo cha Kadinali Laurean Rugambwa mwaka 1997.
No comments:
Post a Comment