Maelezo hayo ya Mwalimu Nyerere yapo kwenye kitabu
chake cha Uongozi Wetu Na Hatima ya Tanzania kilichoandikwa mwaka 1994
na kutolewa 1995.
“Wakati Mwalimu anaandika kitabu hiki mwaka 1994
taifa letu lilikuwa linakabiliwa na changamoto kadhaa za kihistoria
ambazo ndizo zilimfanya kuingilia kati na kuandika kijitabu hiki ambacho
kilikuwa kama nasaha, onyo, na usia kwa Watanzania,” inasema sehemu ya
utangulizi wa kitabu hicho.
Katika sura ya nne ya kitabu hicho, pamoja na
mambo mengine Mwalimu Nyerere alizungumzia suala la Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar ambapo alieleza sababu zilizofanya muungano wa
serikali mbili ukaanzishwa.
“Labda ni vizuri kukumbuka kwamba shabaha ya
baadhi yetu ilikuwa ni kuziunganisha nchi za Afrika Mashariki ziwe nchi
moja,” alisema katika kitabu chake hicho.
Alieleza kuwa, wakati Zanzibar na Tanganyika
zinaungana, Kenya, Uganda na Tanganyika zilikuwa katika mazungumzo ya
kutafuta uwezekano wa kuungana.
“Kama jambo hilo lingetokea, nina hakika kabisa
kwamba mfumo wa nchi mpya ambayo ingezaliwa ungekuwa ni wa shirikisho;
ama shirikisho la nchi tatu zenye serikali nne, au shirikisho la nchi
nne zenye serikali tano.
“Kwa kweli hata kesho nchi za Afrika Mashariki
zikiamua kuungana na Tanzania ikawa ni mshiriki, naamini kuwa ni rahisi
zaidi kushirikisha Tanzania yenye serikali mbili ya Zanzibar na ya
Tanganyika kuliko Tanzania yenye serikali mbili, ya Tanzania na
Zanzibar,” alisema.
No comments:
Post a Comment