Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania, Marehemu Daudi
Ballali hakuwa mgonjwa wakati akiondoka na aliugua kwa takriban miezi
kumi kabla ya kukutwa na mauti, Mei 16, 2008 nyumbani kwake, Washington
DC nchini Marekani.
Ballali aliondoka nchini wakati kashfa za wizi
kwenye akaunti ya EPA zikiwa zimeshamiri na wakati kesi za watuhumiwa
zikianza kusikilizwa huku jina la gavana huyo wa zamani likitajwa,
ilitaarifiwa kuwa alifariki baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Miezi mitatu baada ya Ballali kuanza kuugua, Rais
Jakaya Kikwete alikiri kuwa na taarifa za ugonjwa wake, lakini kakanusha
kuwa amekimbia tuhuma za ufisadi zilizokuwa zinaelekezwa Benki Kuu
(BoT).
Hata hivyo suala la gavana huyo likaendelea kuwa
kitendawili hadi mauti yake, ambayo pia iliamsha mjadala mpya; baadhi
wakidai hakuwa amefariki na wengine wakihoji mazingira ya kifo chake.
Lakini uchunguzi uliofanywa na gazeti hili na
kuthibitishwa na baadhi ya ndugu wa marehemu, umebaini kuwa gavana huyo
alifariki na kuzikwa nchini Marekani, lakini wakati anaondoka nchini
Agosti 2008, Ballali hakuwa mgonjwa kama inavyodaiwa na wengi.
Taarifa kutoka ndani ya BoT alikokuwa akifanya
kazi akiwa gavana pia zinasema kiongozi huyo alikwenda Marekani kwa
mambo makubwa mawili; Kwanza kufanya baadhi ya kazi zinazohusiana na
taasisi hiyo kuu ya fedha nchini na pili kusalimia familia yake ambayo
wakati wote imekuwa ikiishi Marekani.
Hata hivyo, Gavana wa BoT, Profesa Beno Ndulu jana
alikataa katakata kuzungumza iwapo taasisi yake ina taarifa iwapo
Ballali aliondoka nchini akiwa mgonjwa au la, na badala yake akataka
suala hilo waulizwe wanafamilia.
“Hayo mambo yalishaandikwa sana na nyie mmeandika
sana. Kila mtu anafahamu kwamba aliondoka akiwa mgonjwa, sasa hizo
taarifa nyingine unazoniambia mimi siwezi kuzizungumzia. Kaulize familia
yake,” alisema Profesa Ndulu.
Wakati Ballali akiwa gavana, Profesa Ndulu alikuwa
mmoja wa manaibu wake na baadaye aliteuliwa kushika wadhifa huo baada
ya ‘bosi’ wake kuondolewa kwenye nafasi hiyo baada ya kampuni ya Earnst
and Young kubaini ufisadi mkubwa kwenye benki hiyo.
Hata hivyo, dada yake na Ballali, Margaret Mpango
alisema kaka yake hakuwa mgonjwa na alitarajia kukaa siku chache nchini
Marekani.
“Safari yake ilikuwa ya siku chache tu. Alikwenda
Marekani lakini alikuwa amepanga kurejea nchini baada ya muda mfupi
maana nyumbani kwake simu zake mbili zilikuwa mezani pamoja na funguo za
gari ambalo lilikuwa limeegeshwa nje kwa style (mtindo) ambayo
ilionyesha kwamba angerudi mapema,” alisema.
Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake mjini
Kigoma, Margaret ambaye ni mke wa askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana,
Dk Gerard Mpango, alisema baadhi ya nguo za marehemu zilitumwa Marekani
baada ya kuanza kuumwa.
“Kama mtu alikuwa anakwenda kukaa sana kwa maana ya ugonjwa,
basi angechukua nguo za kutosha, lakini wakati wifi (mke wa Ballali,
Anna Muganda), aliponiomba kwenda kuchukua baadhi ya nguo, vitu vya kaka
vilikuwa vimeachwa katika hali ambayo ilionyesha kwamba hakai sana,”
alisema Margaret na kuongeza:
“Nakumbuka kwamba hata mikoba yake miwili
iliyokuwa na vitu vyake vya kazini ilikuwa imewekwa mahali ambako
hapakuwa siri. Na hii ni dalili kwamba alipanga kwamba angekwenda na
kurudi baada ya muda mfupi.”
Kuugua kwake
Taarifa zinaonyesha kwamba Agosti 17, 2007 zikiwa
ni siku chache tangu alipofika Washington, Ballali alijumuika na familia
yake, ndugu wa karibu na marafiki zake akiwamo mtangazaji wa zamani wa
Sauti ya Amerika (VOA), Athanas Maijo.
Maijo alialikwa katika hafla hiyo ya kumbukumbu ya
kuzaliwa kwa Ballali alipotimiza umri wa miaka 65, kutokana na ukweli
kwamba, wawili hao waliwahi kuwa marafiki wa karibu na waliwahi kufanya
kazi pamoja VOA katika miaka ya 60, wakati Ballali alipokuwa akisoma
Chuo Kikuu cha Howard, Washington.
Habari zaidi zilizopatikana mjini Washington
zinasema baada ya kumaliza shughuli zilizompeleka Washington, mwishoni
mwa Agosti Ballali aliamua kwenda kufanyiwa uchunguzi wa afya na daktari
wake aliyeko katika Hospitali ya Massachusetts iliyoko Boston, na
baadaye angerejea nyumbani.
Hata hivyo, baada ya kufika hospitalini hapo,
daktari wake alishtuka kutokana na matokeo ya vipimo vya tumbo
alivyomfanyia, hivyo kuamua alazwe ili apate matibabu zaidi.
“Alikwenda kule na mke wake (Mama Muganda) na
hawakuwa hata wamebeba nguo za kutosha kwani hawakujua kama angekutwa na
matatizo yaliyosababisha alazwe, kwa hiyo ilibidi nguo pamoja na vitu
vingine vipelekwe baada ya kulazwa kwake,” kilieleza chanzo chetu jijini
Washington.
Habari kutoka kwa ndugu wa karibu wa gavana huyo
zinasema daktari huyo katika vipimo vyake, alibaini kuwapo kwa tatizo
kubwa katika utumbo mpana, hivyo aliamua kumfanyia upasuaji mkubwa baada
ya kushaurina na madaktari wenzake katika hospitali hiyo,
wakishirikiana na daktari wa Ballali aliyekuwa Washington akifanya kazi
katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Georgetown.
Upasuaji huo ulikumbwa na changamoto kubwa kwani
tatizo aliloliona daktari kupitia vipimo vya kitaalamu, lilikuwa ni
tofauti kabisa na tatizo halisi ambalo daktari huyo alikutana nalo
wakati akitaka kutekeleza wajibu wake.
“Ilibidi sasa awasiliane na daktari mwenzake yule
wa Washington kumwambia tofauti hizo, kwa hiyo alimshauri kwamba atibu
matatizo yote mawili, lile alilokuwa akiliona kwenye vipimo na lile
alilokutana nalo wakati akitaka kuanza upasuaji,” alidokeza ndugu
mwingine wa Ballali ambaye hata hivyo alikataa katakata kutaja aina ya
matatizo hayo.
Alisema tiba hiyo ambayo alimsababisha Ballali
kulazwa kwa siku kadhaa na kuyeyusha mipango yake ya kurejea Tanzania
mapema, ndiyo iliyomwezesha kuishi kwa muda mrefu zaidi, vinginevyo
asingevuka 2007.
Wakati wote alipokuwa amelazwa, hakuna kiongozi yeyote wa
Serikali kutoka Tanzania wala ubalozini Washington DC aliyefika kumjulia
hali.
Juzi Katibu Mkuu Kiongozi Ombeni Sefue, ambaye
wakati wa kifo cha Ballali alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani,
alikiri kwamba alihudhuria ibada na baadaye mazishi wakati huo.
Hata hivyo, alipoulizwa iwapo aliwahi kumjulia
hali Ballali alipokuwa amelazwa, Sefue alisema hakuwahi kufanya hivyo na
alipoulizwa sababu za kutokwenda alisema kwa kifupi: “Ndiyo hivyo,
haikutokea, lakini ukweli ni kwamba Ballali aliumwa na bahati mbaya
alifariki dunia.”
Kutoka hospitali
Desemba 2007, Ballali aliruhusiwa kutoka hospitali
na alikaa kwa muda katika hoteli moja mjini Boston na baada ya kupata
nafuu alirudi nyumbani kwake Washington ambako aliendelea kuuguzwa, huku
afya yake ikielezwa kwamba ilikuwa ikiendelea kuimarika.
Hata hivyo, mwanzoni mwa Aprili 2008, Ballali
alilazwa tena, safari hii katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Georgetown
ambako alikaa hadi mwanzoni mwa Mei mwaka huo, alipoambiwa na madaktari
kwamba asingeweza kupona na kwamba mauti yangemkuta katika wiki mbili.
Habari kutoka ndani ya familia yake zinasema
madaktari waliokuwa wakimtibu walimwambia kwamba asingeweza kuishi kwa
zaidi ya wiki mbili, hivyo walimshauri ahamie kwenye nyumba maalum ya
kusubiri kifo kwa watu ambao magonjwa yao yameshindikana.
Hata hivyo, Ballali alikataa na badala yake kutaka
arejeshwe nyumbani kwake, Washington ambako aliendelea kuugua na
hatimaye kukutwa na mauti Mei 16, 2008 kisha kuzikwa katika makaburi ya
Gate of Heaven yaliyopo Silver Spring, Maryland.
Gazeti hili liliwasiliana na hospitali zote mbili
ambako Ballali aliwahi kulazwa, lakini lilijibiwa kwamba taarifa za
mgonjwa huyo zinaweza kutolewa tu ikiwa familia yake ndiyo
inayozihitaji.
Mkanganyiko wa taarifa
Kilichobainika kinapingana na taarifa kadhaa
zilizowahi kupatikana kutoka katika vyanzo mbalimbali serikalini,
zikidai kwamba Ballali alikuwa mgonjwa wa kansa ya damu (leukemia) na
kwamba kwa muda mrefu alikuwa akitibiwa Afrika Kusini kabla ya kutibiwa
Marekani.
Hata hivyo, baada ya kifo chake suala la kansa ya
damu lilipotea kabisa na hakuna anayelizungumzia hivi sasa, kwani kila
ndugu anayeulizwa anasema hafahamu sababu za kifo chake.
Akizungumza na mwandishi wa Mwananchi katika mahojiano
yaliyofanyika Machi 1, mwaka jana, katika Kijiji cha Luganga, Wilaya ya
Mufindi, Iringa, Paschal Ballali ambaye ni mdogo wake na marehemu
alisema hana kumbukumbu kwamba kaka yake aliwahi kuugua ugonjwa wa
kansa.
“Nakumbuka siku chache kabla ya kwenda Marekani
nilikutana na kaka akitoka kazini pale BoT na aliniambia kwamba
atasafiri kwa siku cheche na atarudi. Lakini hakuniambia kwamba anaumwa,
na hata katika kuishi kwake sikumbuki kama aliwahi kusema kwamba
anaumwa kansa,” alisema Paschal.
Kuhusu kutibiwa Afrika Kusini, Paschal alisema
siku chache baada ya kuanza kazi BoT, Ballali aliwahi kuanguka ghafla
akiwa ofisini kutokana na kufanya kazi muda mrefu, na kwamba wakati huo
ndipo alipokwenda kutibiwa nchini humo.
“Tena nakumbuka kipindi hicho ni kama 2002
aliporudi baada ya kupona, alituita nyumbani kwake, Dar es Salaam
tukashiriki kutoa shukrani kanisani kisha alifanya sherehe ndogo ya
tukio hilo, tangu hapo sijawahi kusikia kwamba anakwenda Afrika Kusini
kutibiwa,” alisema Paschal.
Mwananchi
Mwananchi
No comments:
Post a Comment