Thursday 24 July 2014

Hawa wako kwenye rada ya Simba.

ZOEZI la usajili linaonekana kuupasua kichwa uongozi mpya wa klabu ya Simba kutokana na kuwepo kwa mkanganyiko mkubwa juu na nani asajiliwe katika kikosi hicho.
Simba tayari imewasajili mabeki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Joram Mgeveke na makipa Hussein Shariff ‘Casillas’ na Peter Manyika Junior ikiwa ni jitahada zake za mwanzo za kuboresha kikosi hicho.
Kwa sasa viongozi wa Kamati ya Usajili ya Simba wanahaha ndani na nje ya nchi kuangalia uwezekano wa kuongeza nyota kadhaa katika kikosi cha timu hiyo. Ifuatayo ni orodha ya wachezaji 10 wanaoweza kuvaa jezi za Simba msimu ujao na ambao wamekuwa wakiupasua kichwa uongozi mpya.

1. Jean-Claude Iranzi
Ni straika wa APR ya Rwanda yuko kwenye rada za viongozi wa Kamati ya Usajili ya Simba ikiwa ni jitihada za kumwongezea nguvu Mrundi Amissi Tambwe katika upachikaji wa mabao klabuni hapo. Iranzi alizungumza na Mwanaspoti na kukiri kufanya mazungumzo ya awali na uongozi wa Simba hivyo huenda tukamwona kwenye jezi ya wekundu hao msimu ujao,ingawa bado viongozi wa juu wanabishana.

2. Paul Kiongera
Rais wa Simba, Evans Aveva katikati ya wiki iliyopita alikwea pipa hadi nchini Kenya kwenda kufanya mazungumzo na mshambuliaji huyo wa KCB ya nchini humo baada ya jitihada za Kamati ya Usajili kufeli. Awali Kamati ya Usajili ya Simba ilifanya makubaliano na Kiongera na kukubaliana kumlipa dola 15000 (Sh 24.3 milioni) kama ada ya usajili lakini mmoja wa vigogo hao wa Simba alikurupuka na kujikuta akipandisha dau hilo hadi dola 25000 (Sh 32.3).
Habari kutoka ndani Simba zinadai kuwa Aveva ameshafanikiwa kumalizana na Kiongera na atatua nchini muda wowote kuanzia leo ili kusaini mkataba na wekundu hao.

3. Pierre Kwizera
Kiungo Pierre Kwizera anayekipiga timu ya Afad Abidjan ya Ivory Coast aliwasili nchini alfajiri ya Jumamosi iliyopita na kufanya mazungumzo na viongozi wa Kamati ya Usajili ya Simba na kufikia makubaliano ya awali. Baada ya kufikia makubaliano hayo Pierre tayari amerejea nchini Ivory Coast kwenda kumalizana na klabu yake hiyo ya awali kwaajili ya kukamilisha dili hilo la kuhamia Simba. Ujio wa Pierre unaweza kuua dili la Iranzi kutokana na nafasi za wachezaji wa kigeni klabuni hapo kusalia mbili pekee. Nafasi ya pili itajazwa na Kiongera.

4. Elius Maguri
Baada ya Simba kushindwa kukamilisha dili la usajili wa mchezaji yoyote kutoka klabu ya Mbeya City, sasa wamehamishia rada zao kwa mpachika mabao wa Ruvu Shooting, Elius Maguri. Mshambuliaji huyo ambaye alimaliza msimu uliopita akiwa na mabao 14 huenda akaongezwa msimbazi ili aongeze nguvu katika kikosi hicho kilichomaliza katika nafasi ya nne msimu uliopita. Taarifa zaidi zinadai kuwa Simba imeshamalizana na mchezaji huyo na kazi imeabaki kumalizana n

5. Saady Kipanga
Licha ya Klabu ya Mbeya City kugoma kuwauzia Simba mchezaji yoyote, Kipanga bado ana mapenzi ya kutua Simba na tayari ameshafanya makubaliano na baadhi ya viongozi wa kamati ya Usajili. Dili la Kipanga linaonekana kuwa gumu kutokana na Mbeya City kuwa na msimamo mkali hivyo endapo uhamisho wa Elius Maguli utafanikiwa dili la Kipanga linaweza kuwekwa kapuni.

6. Edward Charles
BEKI ngongoti wa JKT Ruvu, Edward Charles amekuwa kwenye rada za Simba kwa muda mrefu sana na huenda wiki hii viongozi wa Kamati ya Usajili wa klabu hiyo ukamalizana na mchezaji huyo. Taarifa za ndani kutoka Simba zinaeleza kuwa dili hilo limekwamishwa na wakala wa Charles ambaye ni Mjomba wake kutaka Simba itoe Sh 25 milioni wakati Simba wako tayari kutoka Sh 18 milioni pamoja na kulipa fidia ya mkataba wake wa mwaka mmoja uliosalia Ruvu.

7. Jabir Aziz ‘Stima’
Taarifa za ndani kutoka Kamati ya Usajili ya Simba zinadai kuwa kuna uwezekano kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Jabir Aziz ‘Stima’ aliyetemwa na Azam akarejeshwa klabuni hapo. Dili la Stima linaonekana kukwamishwa na dili jingine la Michael Mgimwa ambaye tayari ameanza mazoezi na klabu hiyo. Awali baadhi ya viongozi wa Kamati ya Usajili walimtaka Stima akafanye mazoezi na klabu hiyo ili kocha mkuu wa timu hiyo Zdravko Logarusic aweze kuuona uwezo wake lakini mchezaji huyo aligoma na kutaka kupewa mkataba kwanza.

8. Deus Kaseke
Simba bado haijakata tamaa ya kumnasa kiungo mshambuliaji wa Mbeya City, Deus Kaseke ambaye amewekewa ugumu na klabu yake. Kocha Logarusic aliingia matatani na uongozi wa klabu hiyo wikiendi iliyopita baada ya kuutaka uongozi wa klabu hiyo kumsajili Kaseke pamoja na wenzake wanne kutoka Mbeya City. Taarifa za ndani zaidi kutoka Simba zinadai kuwa Logarusic anaukubali sana uwezo wa Kaseke.

9. Haruna Moshi ‘Bobani’
Kamati ya usajili ya Simba imekumbwa na mpasuko mkubwa baada ya baadhi ya vigogo wa kamati hiyo kuibua upya uwezekano wa kumrejesha kiungo wa zamani wa timu hiyo, Haruna Moshi ‘Bobani’. Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe alisema hawawezi kumrejesha Bobani kutokana na nidhamu yake mbaya lakini inasemekana kuwa baadhi ya wajumbe wanampigia chepuo mchezaji huyo kwa madai kuwa kiwango chake bado kinaridhisha.

10. Shaaban Kisiga
Uchovu! Kamati ya Usajili ya Simba imeonekana kuchoka baada ya baadhi ya wajumbe wake kupendekeza kusajiliwa kwa Kiungo Shaban Kisiga. Kiungo huyo kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kutemwa na Mtibwa Sugar aliyoichezea msimu uliopita. Hivyo katika majira haya ya usajili usishangae kusikia Kisiga amesajili kuichezea Simba kwa mara ya pili.

No comments:

Post a Comment