Akichangia mjadala katika Bunge hilo jana, Mjumbe Muhammed Seif Khatib alieleza namna Seif alivyokuwa akijitoa mhanga kutetea serikali mbili kiasi cha kuiba nyaraka za Ikulu kuzima mtandao wa waliotaka serikali tatu.

Khatib ametoa ushuhuda huo huku akinukuu maneno ya Seif kama yalivyokuwa wakati akiwasilisha hoja za kutetea serikali mbili ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, mwaka 1984.

Alisema katika taarifa rasmi za NEC ya CCM, zinaonesha Seif akisema amesikitishwa na kuumizwa sana na mbinu chafu za kutaka serikali tatu, zinazofanywa na baadhi ya viongozi wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar walipoelezea msimamo wa makubaliano ya serikali tatu, na kuhoji ukweli wa jambo hilo.

Kwa mujibu wa Khatib, kauli hiyo ya Seif aliitoa alipokuwa akimtuhumu aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, kwa kupanga njama za kuanzisha muundo wa Muungano wa serikali tatu, kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wenzake.

“Nataka niwarejeshe wabunge kwamba, Aboud Jumbe angefanikiwa na hoja yake ya kutaka serikali tatu, leo hii tusingekuwa na mkutano huu, hakufanikiwa kwa kuwa kiongozi mmoja wa CUF, Seif Sharrif Hamad, alimsimamisha na hayo yamo kwenye taarifa sahihi za mkutano wa CCM, Dodoma mwaka 1984,” alisema Khatib.

Khatib alinukuu kauli ya Maalim Seif: “Msimamo wa Jumbe umetufadhaisha sisi sote, tunataka maelezo yake ni dhahiri hoja ya serikali tatu haikuanzishwa na watu wadogo, imechangiwa pia na baadhi ya viongozi wa Baraza la Mapinduzi na Aboud Jumbe ni chanzo cha hayo.

Kwa mujibu wa Khatib, taarifa hizo rasmi za CCM zinaonesha wazi kuwa Seif alikuwa mstari wa mbele kuzuia serikali tatu, na kuwa mtetezi wa serikali mbili, ambapo alijaribu kufanya kazi tatu.

Alitaja kazi ya kwanza aliyofanya Seif ni ile ya Uchunguzi, ya pili ya Mwendesha Mashtaka, ya tatu Wakili CCM na aliwatuhumu watu wanne, akiwemo Jumbe, Jamal Faki, Abuu Salim na Wolfgang Dourado, ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa kwanza Zanzibar.

Seif kwa mujibu wa Khatib, aliwaita akina Jumbe kuwa ni wasaliti wa nchi na aliamua kwenda kuwashitaki katika kikao cha NEC ya CCM, na kusema wao wanataka serikali tatu hivyo wanastahili kuhukumiwa.

“Seif huyo alisema anasikitishwa sana na Dourado kusafiri kwake na amekuwa akiukashifu Muungano na kudai sio halali, na kudai jeuri ya Dourado ameipata wapi ya kusemea Wazanzibari na kudai ruhusa kapewa na nani ya kwenda Ulaya,” alisema Khatibu akimnukuu Seif akitoa mashitaka kwa Mwenyekiti wa CCM, wakati huo Mwalimu Julius Nyerere.

Khatib alisema Seif hakuishia hapo bali aliwashitaki watuhumiwa wote kwenye Mahakama ya NEC na kuiomba iwahukumu watakaohusika na kuhitimisha kuwa wanaotaka serikali tatu ni kinyume na matakwa yao na shabaha ya malengo yao na hiyo inahatarisha usalama wa nchi, na kwamba ni vitendo vya uhaini.

Khatib aliendelea kusema, kama hilo halikutosha, kwenye hotuba ya Rais wa Zanzibar, Seif alituhumiwa kuwa ndiye aliyeiba waraka wa siri Ikulu ya Zanzibar, ili kuzima mtandao uliokuwa umejipanga kuanzisha serikali tatu.

Kwa mujibu wa Khatibu, Seif amelikiri kwenye kitabu cha Profesa Issa Shivji na kusema alifanya hivyo kwa lengo la kutetea serikali mbili.

“Maalim Seif wa mwaka 1984 alikuwa mtetezi wa serikali mbili lakini baada ya kufukuzwa kwenye chama mnamo Mei 13, mwaka 1988 saa nne usiku, kuanzia hapo akawa mtetezi wa serikali tatu, Januari mwaka jana akaanza kudai serikali ya Mkataba, huyo ndio Seif.

“Kwake yeye kudai serikali tatu kipindi hicho ilikuwa ni uhaini, leo je? Hapa tunajifunza kwamba baadhi ya viongozi wa upinzani akiwepo Maalim Seif ni kinyonga wakipita kwenye mvua wanafanana na rangi ya mvua, baharini ni kama bahari akipita kwenye jua ni kama jua.

“Seif ni kinyonga, wananchi wawe macho kwani anabadilika kila mara awali aliwashutumu wote waliotaka serikali tatu, akisisitiza ziwe mbili lakini leo amebadilika tena anataka Mkataba,” alisema Khatibu.

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Hamad Rashid Mohamed, alisema Seif ni kiongozi hatari na kigeugeu ambaye awali alikuwa na msimamo wa serikali tatu lakini sasa anasimamia Muungano wa Mkataba.

Hamad ambaye mbali na ujumbe wa Bunge Maalumu ni Mbunge wa Wawi kupitia CUF, nafasi aliyorejeshewa na Mahakama baada ya kutaka kunyang’anywa na chama chake, amesema mwaka 1992, uongozi wa CUF ulisimamia serikali tatu lakini juzi Seif katika mikutano ya hadhara alisema msimamo wa chama hicho ni Muungano wa mkataba.

“Tuangalie viongozi wanaobadilika badilika, mwaka 1992 msimamo wa CUF ulikuwa serikali tatu, juzi serikali ya mkataba, anabadilika kila baada ya dakika tatu, kiongozi wa aina gani huyu? “Mwaka 1984 Seif alitaka serikali mbili, mwaka 1992 akiwa CUF msimamo ukawa Serikali tatu, juzi mkataba, huyu ni kiongozi wa aina gani, ni wa kuwaongopea watu,” aliendelea kusema Hamad.

Alisema wakati wakidai Katiba mpya, CUF na vyama vingine vya upinzani viliandamana na kuwaingiza watu kwenye ulemavu, wajane na watoto, wanafunzi walikosa masomo na leo badala ya kuhakikisha Katiba inapatikana, wanahatarisha amani na kutaka mapinduzi tena.

Alihoji kati yake na Maalim Seif, msaliti ni nani kwani wakati wakiwa wanatafuta serikali ya umoja wa kitaifa, walikutana sehemu mbalimbali ikiwemo Dodoma na kuafikiana namna ya kuunda serikali hiyo, lakini alishangaa wenzake watano akiwemo Seif walijifungia ndani, wakaja na mkataba na kuhoji kama ni usaliti, nani msaliti wa wenzake.

“Tulienda kwenye kikao cha Halmashauri Kuu (wakati wakiwa CCM kabla ya kufukuzwa) na ikapendekezwa Mwinyi (Rais Ali Hassan) agombee urais na kwa vyovyote Maalim Seif awe Waziri Mkuu…kama haitoshi, wakati Idrisa (Abdul Wakil) akiwa Rais, Seif aliendelea kuwa Waziri Kiongozi Zanzibar, sasa Wazanzibari msaliti mnamfahamu?” alihoji Hamad.

Alisema yeye tangu mwaka 1982 yupo Tanzania Bara na kwamba uhusiano wake na Bara si wa kawaida, ni wa kindugu wa damu na kusema kama kuna watu wanasema yeye amekimbia, hakimbii mapambano wala hakimbii tendo la kihistoria. “Mheshimiwa Mwenyekiti nilifiwa mimi, mtu wa kwanza kuja alikuwa Kingunge Ngombale Mwiru (Mjumbe wa Bunge hilo) ndio wengine wakafuata, undugu wetu si wa kawaida,” alisisitiza Hamad.