Kwa mwanamke kumpata mwanaume mwenye muafaka, yaani mwanaume ambaye ni husband material si kazi rahisi. Inaweza kuchukua miezi kama siyo miaka ya kucheza pata potea kabla ya kumpata mwanaume halisi wa ndoto yako. hata hivyo wakati mwingine inaweza kutokea mwanamke akafanya majaribio kadhaa ya kuwa na mitoko (dating) na wanaume tofauti tofauti na bado akajikuta anatoka kapa, yaani hakuna hata mmoja anayefikia viwango vyake alivyojiwekea na kujikuta umri unasonga na bado wako single. Jambo hilo huwachanganya sana wanawake wengi na kuwaletea msongo wa mawazo au vurugu kichwani na kuonekana kama vile wamedata wakati siyo kweli ni kutokana na mapito katika harakati za kumpata mwenza mwenye muafaka.

Hapa chini nitaeleza sababu zinazosababisha wanawake wengi kukwama pale wanapokuwa kwenye harakati za kutafuta mwanaume wa ndoto zao:



1. Hujui unatafuta mwanaume wa aina gani?


Huu ni ujinga unaofanywa na wanawake wengi. Kuna idadi ya kutosha ya wanawake ambao wanakuwa na mitoko na wanaume wa aina tofauti tofauti lakini ndani ya nafsi zao hawajui wanataka kuolewa na mwanaume wa aina gani. Mbaya zaidi wanawake hawa wanajikuta wakipoteza muda wao mwingi wa kuwa na mitoko lakini hawajui wabnachokitafuta, mwisho wa siku hujikuta akiwa ametoka na wanaume wengi sana lakini hakuna hata mmoja waliyemuona anafaa, na jambo hilo huwa linawachanganya na kujikuta wakiwa na msongo wa mawazo, kumbe masikini ya Mungu hawajui kwamba mwanaume wanayemtafuta anafananaje.

2. Kujihisi kutokuwa salama


Kama mwanamke anajihisi kutokuwa salama anapokuwa na mtoko kunamuweka katika mazingira ya kutompata mwanaume anayemtarajia kwa sababu hana uhakika anatafuta mwanaume wa aina gani. Kutojiamini kwa mwanamke kunamfanya kushindwa kufanya juhudi binafsi za kumnasa mwanaume wa ndoto zake kutokana na kujiuliza maswali mengi kwamba mwanaume aliye mbele yake ndiye au siye? Mwanamke kutokuwa na uhakika kama atataka mwanaume wa aina gani kunamuweka katika mazingira ya kushindwa kumvutia mwanaume mwenye muafaka hata kama aakuwa na mtoko naye mara kadhaa. Kumbuka tu kwamba maamuzi ya kuwa na uhusiano kati ya mwanaume na mwanamke yapo zaidi kwa mwanamume, hivyo ili mwanaume aweze kujenga uhusiano na mwanamke ni lazima mwanamke huyo amvutia. Kwa kitendo cha kutojiamini mbele ya mwanaume kinamuweka mwanamke katika mazingira ya kuwekwa pembeni. Ni pale tu utakapokuwa umejua unachokitaka au aina ya mwanaume unayemtaka ndipo utakapojiweka kwenye nafasi nzuri ya kutengeneza nafasi ya kukutana na wanaume wa aina hiyo na ukichanganya na kujiamini ndipo utakapofanikiwa kumvutia mwanaume huyo na kumnasa.



3. Ukosefu wa mbinu za kuwanasa wanaume wenye muafaka


Kwa kawaida kila mtu ana udhaifu wake, hivyo linapokuja suala la mtoko, kila mmoja anajaribu kuwa makini kuficha udhaifu wake. Ukweli ni kwamba jambo hilo linaweza kuwa ni kikwazo kwa mwanamke kumpata mwenza sahihi. Unakuna mwanamke anakuwa na mtoko na mwanaume na katika mazungumzo tu ya kawaida anajitahidi sana kutotofautiana na mwanaume aliyetoka naye au anajifanya ni malaika asiyekosea na kujitahidi kuonyesha rangi yake halisi kwamba yeye ni mwanamke wa aina gani. Ni nyema mwanamke akajipambanua na kuonyesha kwamba yeye ni mwanamke wa aina gani kwani yaweza kuwa kwa jinsi yeye alivyo na anavyoyachukulia mambo ikawa ni sifa ambayo inaweza kumvutia mwanaume aliyetoka naye....

4. Mwanamke anaweka nguvu nyingi kwa aina moja ya mwanaume anayemtarajia


Katika mchakato wa kuwa na mitoko, mwanamke anakuwa amejiwekea aina moja ya mwanaume anayemtaka na anaelekeza nguvu nyingi katika kumtafuta mwanaume wa aina hiyo hiyo. Si vibaya kujiwekea malengo na matarajio kwa aina ya mwanaume unayemtaka lakini vigezo vyako vinakufungwa kwa aina moja tu ya mwanaume hilo ni tatizo. Jaribu kutoka kidogo nje ya vigez ulivyojiwekea inaweza kukusaidi kujua aina tofauti tofauti za wanaume...



5. Bado unatembea na kumbukumbu ya mwanaume/wanaume ulioachana nao

Kwa kawaida wakati mwingine ni ngumu sana kuendelea na maisha yako ya kawaida baada ya kuachana na mpenzi wako uliyempenda sana, hasa kama mlikuwa pamoja kwa kipindi kirefu kidogo na mlipendana sana. Hata hivyo kama bado moyo wako umekuwa ni mgumu kumsahau mpenzi wako mliyeachana itakuwa ni vigumu kuwa na mitoko na kumpata mwanaume wa ndoto zako. kwa kifupi ni kwamba hutofanikiwa kwa sababu hujakuwa tayari.



6. Unajitahidi sana kuchukua tahadhari kupita kiasi....

Baada ya kuwa mwanamke ameumizwa sana katika mahusiano yake ya nyuma mara nyingi humuwia vigumu kusahau na kusonga mbele. Lakini pia huyachukulia mahusiano kwa tahadhari kubwa. Kwa kawaida si ajabu kukuta mwanamke aliyetendwa akiwa amejiwekea ulinzi madhubuti dhidi ya wanaume akijitahidi kwa kadiri awezavyo kuwakwepa na hata kuwakataa au kuwakatisha tamaa kwa kuogopa kuumizwa tena. Lakini ukweli ni kwamba kamwe haiwezekani mwanamke kupata mwenza wa ndoto zake iwapo hatakuwa na moyo wa kuthubutu hata kama atakuwa ameumizwa katika mahusiano yake ya nyuma, mara nyingi tunashauriwa kuyatumia makosa yetu kama elimu ya kutuwezesha kufikia matarajio yetu, kwa kuumizwa mara kadhaa kunampa mwanamke uwanja mpana wa kuwajua wanaume wakware na hila zao. hata hivyo inashauriwa mwanamke kujipa muda kidogo ili kuponya kidonda cha kuumizwa katika uhusiano kabla ya kuanza kuwa na mitoko na wanaume wengine watakaoonekana kuvutiwa naye, kwani kama akiharakisha anaweza kushindwa kumshawishi mwanaume aliyetoka naye kutokana na kutojiamini.



7. Kazi inachukua sehemu kubwa ya maisha yako...


Mtu kuipenda kazi yake siyo kitu kibaya, lakini si vyema kazi yako ikachukua sehemu kubwa ya maisha yako na muda wako kiasi cha kukufanya ushindwe kujichanganya katika mambo ya kijamii au kuwa na mitoko itakayokukutanisha na watu mbalimbali wa kubadilishana nao uzoefu. Wakati mwingine mwanamke anaweza akajikuta hapati mwanaume wa kumuomba mtoko kwa sababu ya kuonekana kwake kuwa na udhati (serious)na mambo yake au kazi yake. Unaweza kumkuta mwanamke muda wote yuko bize na kazi kiasi cha kukosa muda wa kuchangamana na watu wengine. Mwanamke wa aina hii ni vigumu sana kupata mwanaume wa ndoto zake. Inashauriwa ili kumpata mwanaume wa ndoto zake ni vyema mwanamke akajiunga na vikundi vya kijamii hususan kwa huku kwetu viko vikundi kama Vikoba vinavyowakutanisha watu mbalimbali kwa shughuli za kiuchumi au kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii ambazo ni rahisi kuwakutanisha watu.



8. Kuwa na mtazamo hasi (Negative) kuhusu wanaume

Huwezi kamwe kumpata mwanaume wa ndoto zako kama una mtazamo hasi kuhusu wanaume. Kama unatawaliwa na fikra za kukata tamaa au kuna sauti ndani yako (little Voices) zinakwambia kamwe huwezi kumpata mwanaume sahihi kwa sababu wanaume wa kuoa wamekwisha au hawapo, na ukaamini na kujenga hofu, ni dhahiri kwamba haitatokea kumpata mwanaume sahihi kama ulivyoamini. Kumbuka kwamba sisi ni kile tunachowaza na kuamini kwa hiyo ni kiasi tu cha kubadilisha mawimbi yako ya namna ya kufikiri kwa kuwaza mambo mazuri unayoyahitaji huku ukiamini kabisa kwamba inawezekana. Lakini pia labda nitoe ushauri wa bure kwa wanawake. Kama unataka mwanaume wa ndoto zako awe wa namna gani basi tengeneza picha yake kichwani mwako na kisha kila siku asubuhi fanya tahajudi kwa dakika kumi tu, na nuia kwamba ungependa ukutane na mwanaume huyo na akupende mfunge ndoa na kuzaa watoto.


9. Kila mwanaume anayekuomba mtoko unagundua siyo sahihi kwako

Kuwavuta wanaume wasiyo sahihi na wasiokidhi viwango vyako kunachangiwa na mambo mengi. Hebu chunguza mawazo yako, chunguza marafiki zako unaoambatana nao, chunguza maeneo unayoishi, chunguza maeneno unayotembelea, Je wewe ni mwanamke wa aina gani, una tabia gani nk......... Ni vyema kama unajiwekea malengo ya kumpata mwanaume mwenye tabia uzitakazo, basi mchakato wa kumpata ni pamoja na kujiweka katika mazingira ya kumvutia mwnaume huyo. Isije ikawa unatamani kumpata mwanaume msomi mcha Mungu na mchapa kazi na anayejali familia (sifa ambazo wanawake wengi huzitamani) lakini wewe mwenyewe hauko hivyo, sasa utatengenezaje connection ya kukutana na mwanaume huyo! Kumbuka pia mwanaume wenye haiba hiyo naye ana ndoto zake ni pale tu ndoto zenu zitakapo match ndipo makapovutana na kukutana na kufikia kufunga ndoa na kujenga familia bora.



10. Unawalinganisha wanaume kupita kiasi

Ni vyema kujifunza kutokana na makosa uliyowahi kuyafanya katika mahusiano yako ya nyuma, lakini makosa hayo yasigeuke na kuathiri mtazamo wako kuhusu wanaume. Ninachotaka kusema hapa ni kwamba si vyema kumlinganisha kila mwanaume unayekutana naye na mwanaume uliyewahi kuwa na uhusiano naye huko nyuma. Kila unapokuwa na mtoko na mwanaume nenda huku kichwa chako kikiwa kitupu kabisa ili kupata mtazamo mpya kuhusu mwanaume huyo kutokana na mazungumzo yenu. ukiwa tayari una hofu za kujiuliza kama atakuwa ni mwanaume sahihi au atakuwa kama fulani, ni kama vile umeshamhukumu na kila jambo atakalofanya au kusema utakuwa na mjadala mzito kichwani ukijaribu kulinganisha na kutafuta majibu jambo ambalo litakufanya usiwe na uzingativu kwenye mazungumzo yenu.......