SHIRIKISHO la Soka la Uganda (Fufa) limetamka kwamba halina
pingamizi dhidi ya Emmanuel Okwi kutua Yanga, lakini katika hali ya
kushangaza limeandika barua kwenda Fifa likitaka ufafanuzi kuhusu
uhamisho wa mchezaji huyo.
Okwi amesajiliwa Yanga akitokea SC Villa ya Uganda
ambayo awali ilimchukua mchezaji huyo kwa mkopo wa miezi sita kutoka
Etoile du Sahel ya Tunisia.
Mchezaji huyo aliidhinishwa Villa na
Fifa-Shirikisho la Kimataifa la Soka- baada ya kugoma kurudi Etoile
ambayo ilikuwa haijamlipa fedha zake za mshahara na marupurupu mengine.
“Tumewaandikia Fifa kwa sababu tunataka watuambie
kama uhamisho wake ni sahihi,” alisema Edgar Watson ambaye ni Ofisa
Mtendaji Mkuu wa Fufa.
Lakini Mwanasheria wa Okwi, ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Villa, Edgar Agaba, amesisitiza kwamba kila kitu kiko sawa
na Okwi ni mali ya Yanga.
Septemba 28 mwaka huu, Fifa iliiruhusu Fufa
kumuidhinisha Okwi kuichezea SC Villa kwa muda wa miezi sita ruhusa
ambayo ilitokana na maombi ya Fufa ya Septemba 4 iliyoomba hati ya
uhamisho wa kimataifa (ITC) kutoka Shirikisho la Soka la Tunisia ambako
Okwi alikuwa akichezea Etoile.
Kwa mujibu wa taarifa ya Fufa iliyosainiwa na
Ofisa Habari wake, Rogers Mulindwa, hatua ya Fufa kuomba ITC ya Okwi
ilitokana na mchezaji huyo kuilalamikia Etoile baada ya kushindwa
kumlipa haki zake ikiwamo mshahara hivyo akaomba kuachana nao ili
ajiunge na Villa.
Sakata hilo liliamuliwa na Fifa kupitia Kamati ya
Hadhi za Wachezaji chini ya Jaji Geoff Thompson raia wa Uingereza kwa
kutoa ruhusa ya mchezaji huyo kupata leseni ya kuichezea Villa kwa muda
wa miezi sita.
Hata hivyo, Ofisa Habari wa Fufa, Rogers Mulindwa
alisema kwamba Okwi ana uhuru wa kujiunga na timu yoyote kwa kuwa suala
lake lilimalizwa na Sahel waliomtoa kwa mkopo Villa ili kulinda kipaji
chake.
“Unajua alikuwa na matatizo Sahel na Fifa
wakamuidhinisha achezee Villa, sasa baada ya hapo ana haki kucheza Yanga
au Simba, mambo mengine yanayoendelea najua ni ushabiki wa ndani kati
ya klabu za Tanzania,’’ alisema Mulindwa.
No comments:
Post a Comment