Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake
Rais Jakaya Kikwete, imeanza kuwahoji mawaziri waliotajwa ni ‘mzigo’ kwa
Serikali.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye,
jana alilithibitishia gazeti dada la Mwananchi, The Citizen juu ya
kuanza kwa kikao cha Kamati Kuu (CC), lakini hakuwa tayari kuingia kwa
undani kuhusu ajenda.
Hata hivyo, habari za ndani zilieleza kwamba
miongoni mwa ajenda kuu za CC ni kuwahoji mawaziri wanaolalamikiwa na
wananchi, kwamba wameshindwa kutekeleza majukumu yao.
Wakiwa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Nape
aliwatupia lawama mawaziri wakati akielezea changamoto zinazowakabili
wakulima ambao ni asilimia 80 ya Watanzania, huku mawaziri husika
wakikaa kimya.
Mawaziri waliotajwa mzigo ni Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa; Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Christopher Chiza na Naibu wake, Adam Malima, kwamba
wameshindwa kazi na alipendekeza wang’olewe.
Hata hivyo, gazeti hili jana lilishuhudia mawaziri
kadhaa wakifika na kuingia kwenye mkutano wa CC, taarifa zingine
zilisema mawaziri waliofika kwenye kikao hicho walihojiwa na wajumbe wa
CC.
Kuhojiwa na CC
Mawaziri waliohojiwa na CC hadi kufikia saa 8:00
mchana jana walitajwa kuwa ni Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza. Mkuya ndiye
ambaye kwa sasa anaisimamia Wizara Fedha kutokana na Waziri wa Fedha, Dk
William Mgimwa kulazwa nchini Afrika Kusini akisumbuliwa na maradhi
ambayo hayajatajwa.
Waandishi wa gazeti hili jana waliwashuhudia
takriban mawaziri 10 wakiingia katika ofisi za makao makuu ya CCM,
Dodoma, maarufu White House, huku baadhi wakiwa si wajumbe wa CC.
Habari zilizotufikia jioni ziliwataja wengine kuwa
ni Dk David Mathayo David (Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi),
Hawa Ghasia (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa-Tamisemi), Dk Kawambwa, Celina Kombani (Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma).
Dk Kawambwa wakati akitoka kwenye kikao cha CC
aliulizwa na waandishi wa habari kilichotokea na yeye alijibu kwa
kifupi; “Mawaziri mizigo ndiyo tunatoka.”
Mawaziri ambao si wajumbe wa CC ni Mkuya, Chiza,
Dk Kawambwa, Hawa Ghasia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
anayeshughulikia Utawala Bora, George Mkuchika ambaye naye taarifa
zilidai alihojiwa.
Azimio la Bunge
Tayari Bunge limepitisha azimio la kumtaka Ghasia
pamoja na naibu mawaziri wake wawili, Aggrey Mwanry na Majaliwa Kassim
Majaliwa, kupima na kutafakari kama bado wanatosha kusimamia wizara
hiyo.
Kiini cha Bunge kupitisha azimio hilo ni taarifa
ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kubainisha kuwapo wizi,
ubadhirifu na mtandao wa ufisadi ndani ya Tamisemi, Halmashauri na
Hazina.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye baadhi ya
wabunge wamemtaja kama waziri mzigo namba moja, amesema yuko tayari
kuachia ngazi kama Rais ataamua kumwondoa katika wadhifa huo.
Pinda alitoa kauli hiyo juzi bungeni mjini Dodoma
wakati akijibu swali la papo kwa hapo kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalumu,
Rukia Ahmed (Cuf) aliyetaka aeleze anajisikiaje kuitwa mzigo namba
moja.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema yeye anasimamia
wizara 20, hivyo kama wapo watakaomhukumu kwa sababu ya wizara moja ama
mbili kutofanya vizuri basi watu hao watakuwa hawamtendei haki.
Alisema kama Rais atamwona ameshindwa kuwajibika
yuko tayari kuachia ngazi na endapo Rais hatafanya hivyo na wabunge bado
wakaona ipo haja hiyo, wampigie kura ya kutokuwa na imani naye.
Kauli ya CCM
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye,
mbele ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, alisema kuwa
mawaziri hao wameshindwa kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia Watanzania.
Alisema kuwa Waziri Chiza na Malima wamebaki
wakifunga tai na kuvaa suti mjini wakati wakulima wa Ruvuma na mikoa
mingine ya Tanzania wakiteseka.
Nape alisema Waziri Kawambwa naye anatakiwa
kuchukuliwa hatua kwa kuingia mkataba na kampuni ya ujenzi ya
Progressive iliyopewa zabuni ya kutengeneza barabara ya Namtumbo hadi
Tunduru wakati mkandarasi huyo hana uwezo wa kuijenga na matokeo yake
amefukuzwa kazi.
Dk Kawambwa ametupiwa lawama hizo kutokana na
kuipa kazi kampuni hiyo wakati akiwa Waziri wa Miundombinu pamoja na
kushindwa kusimamia elimu.
Mwananchi
Mwananchi
No comments:
Post a Comment