KOCHA Mkuu wa Yanga, Ernest Brandts, ametamka kuwa hana wasiwasi
na Ligi ya Mabingwa Afrika na kwamba atawachapa Wacomoro kwenye mechi
ya kwanza huku akiipigia hesabu kali Al Ahly ya Misri.
Yanga itacheza michuano hiyo mikubwa ya klabu
barani Afrika na imepangwa kuanza na Komorozine ya Comoro katika raundi
ya kwanza. Mechi zitaanza Februari mwakani. Kama itavuka raundi hiyo,
itakutana na Al Ahly katika raundi ya pili, wapinzani hao ndio mabingwa
watetezi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Brandts alisema:
“Hatuna wasiwasi na ratiba, tutacheza na Wacomoro na baadaye Al Ahly.
Siwafahamu hao Wacomoro lakini tumejiandaa kupambana nao, bila shaka
itakuwa si timu ya kutisha sana na tunachokifanya sasa ni kuhakikisha
tunapata taarifa zao.
“Ninahitaji kuwafahamu kwa kupata mikanda yao ya
video, niwaone namna gani wanavyocheza na ni wachezaji gani ni tegemeo
lao, kuhusu Al Ahly naifahamu ni timu kubwa, lakini Yanga nao ni kubwa
kama unavyojua, siku zote timu nzuri inapangwa na wazuri wenzao kwa
maana hiyo hakuna shida, tunajiandaa.
“Lakini kwa sasa Al Ahly nimeiweka pembeni kwanza,
ninachoangalia ni huu mchezo wa kwanza na Komorozine, kuona ni namna
gani tutapambana nao na kufuzu hatua ya pili na ndipo Al Ahly watafuata.
“Timu ipo vizuri, najivunia hilo kwani hakuna
kocha yeyote duniani asiyependa kuwa na timu nzuri. Watu wengi
wanajaribu kukiangalia kikosi chetu kwa ajili ya Ligi Kuu pekee, lakini
mimi naangalia mbele zaidi hasa mashindano ya kimataifa, lazima tuanze
kuweka mikakati sasa.
“Tuna timu nzuri hivyo viongozi wanapaswa kuanza
maandalizi kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa ambayo tutashiriki mapema
Februari kuhakikisha tunafanya vizuri pia.
“Ubora wa kikosi chetu unatakiwa tuuonyeshe hata
kimataifa ili tujitofautishe na wengine kwenye ligi ya ndani, kama
tulishindwa huko nyuma kuvuka hatua nyingine tujitahidi sasa kwenda
mbele zaidi, naamimi hilo linawezekana kama tutapata maandalizi mazuri.”
No comments:
Post a Comment