Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela
amefariki dunia jana nyumbani kwake, Mtaa wa Houghton, Johannesburg
akiwa na umri wa miaka 95.
Mandela aliyeliongoza taifa hilo kuanzia mwaka
1994 hadi 1999, kwa muda mrefu alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya mapafu
na takriban nusu mwaka. Madaktari walimruhusu kutoka hospitali
alikokuwa amelazwa kwa muda wa miezi mitatu na kushauri aendelee kupata
matibabu nyumbani kwake.
Tangu juzi, ilielezwa kwamba kulikuwa na pilikapilika nyingi zilizoashiria kwamba pengine kungekuwa na tukio lisilo la kawaida.
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma jana kwa majonzi
makubwa alitangaza kifo cha Mandela na kusema kuwa kiongozi huyo mwenye
historia ya pekee katika Bara la Afrika amepumzika kwa amani… “Baba
Mandela amefariki na amepumzika kwa amani, taifa letu limempoteza mtu
muhimu na wa pekee.”
Rais Zuma alitangaza msiba huo akiwa Ikulu,
Pretoria Alhamisi saa 02:50 za Afrika Kusini (saa 03:50 usiku kwa saa za
Tanzania) na kwamba kiongozi huyo alifariki akiwa amezungukwa na mke
wake, Graça Machel pamoja na wanafamilia wengine.
Zuma alisema Mandela atafanyiwa mazishi ya kitaifa
na kwamba kuanzia leo taifa hilo litakuwa kwenye maombolezo huku
bendera zikipepea nusu mlingoti hadi hapo atakapozikwa.
Juzi, mtoto mkubwa wa Mandela, Makaziwe alisema afya ya baba yake ni mbaya na kwamba alikuwa amelala kwenye “kitanda cha mauti”.
Shirika la Habari la Afrika Kusini (SABC),
lilimnukuu mtoto huyo wa Mandela akisema: “Baba bado yuko pamoja nasi,
yuko mahututi, nadhani bado anatufundisha somo, somo la upendo na somo
la uvumilivu.”
Mjukuu wa Mandela, Ndaba alinukuliwa na shirika
hilo akisema: “Afya yake siyo nzuri sana, bado yuko na sisi, ingawa
haendelei vizuri sana, bado yupo kitandani nyumbani.”
Dunia yamlilia
Chama tawala cha Afrika Kusini (ANC) leo alfajiri, kilieleza kusikitishwa kwake na kifo cha muasisi huyo.
“Taifa letu limempoteza shujaa wa haki, usawa,
amani na haki ambaye alikuwa tumaini la mamilioni wa watu,” alisema
Katibu Mkuu wa ANC, Gwede Mantashe.
No comments:
Post a Comment