SAA 24 baada ya Yanga kumsajili mshambuliaji wa zamani wa Simba,
Emmanuel Okwi kutoka SC Villa ya Uganda, wachezaji wa timu hiyo wameupa
dole gumba uongozi wakisema: “Asanteni kwa kutuletea fundi.”
Wakizungumza na Mwanaspoti mara baada ya mazoezi
ya Yanga jana Jumatatu asubuhi kwenye Uwanja wa Bora, Kijitonyama jijini
Dar es Salaam, wachezaji hao waliupongeza uongozi kwa kusema Okwi ni
mchezaji hodari atakayeongeza ufanisi kikosini mwao.
Mchezaji wa kwanza kuzungumza na Mwanaspoti
alikuwa Haruna Niyonzima ambaye alisema amefurahi kuona Okwi amejiunga
na Yanga kwani ilikuwa ni ndoto yake ya siku nyingi kucheza na mchezaji
huyo.
“Ujue najiona kama naota, kweli Okwi amejiunga na
Yanga? Hebu niambie ukweli. Okwi ni mchezaji niliyekuwa nikitamani
kucheza naye siku moja, sasa kama kweli amesajiliwa itakuwa poa sana,”
alisema Niyonzima.
Straika Jerry Tegete alisema: “Ni mchezaji mzuri
anayeweza kuiletea mafanikio Yanga ndani ya muda mfupi, namkaribisha
katika timu na nitashirikiana naye kuiletea timu mafanikio.”
Kwa upande wao, beki Juma Abdul na kiungo Frank
Domayo, wamesisitiza kwamba kamati ya usajili imefanya uamuzi sahihi na
wakasema timu hiyo itatisha kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania
Bara.
Kipa Juma Kaseja aliyewahi kucheza na Okwi katika
kikosi cha Simba kilichoifunga Yanga mabao 5-0 mwaka jana, alisema:
“Okwi namjua vizuri, nilicheza naye Simba, Yanga itakuwa vizuri sasa
katika safu ya ushambuliaji kwani jamaa (Okwi) ana vitu vingi ambavyo
washambuliaji wengine hawana.”
Okwi anatarajiwa kutua nchini wiki hii kujiunga na
wenzake wanaojiandaa na mechi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba
itakayochezwa Jumamosi Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment