AFANDE Sele, mwanamuziki maarufu wa kizazi kipya nchini, aliwahi
kuimba katika wimbo wake fulani hivi akisema; ‘Aliwazalo mjinga ndilo
litakalomtokea.’
Leo, miaka kadhaa baada ya mstari ule, Yanga kimewatokea walichokuwa wanawaza kwa muda mrefu, lakini wakaonekana wajinga.
Tangu Emmanuel Okwi apate makali katika miguu yake
miaka minne iliyopita Mtaa wa Msimbazi, jijini Dar es Salaam, Yanga
walikuwa wanawaza kumpata, na kweli wamempata.
Maswali mengi kuliko majibu
Kabla Okwi hajavaa jezi za njano na kijani, kuna
maswali mengi yanayopaswa kujibiwa ingawa majibu yake hayaonekani
hewani. Tatizo si Yanga imempataje Okwi. Tunajua kuwa fitina maridadi za
usajili kwa sasa zimehamia Yanga baada ya kufifia kwa kundi la Friends
of Simba la klabu ya Simba ambao ndio walikuwa hodari zaidi kwa fitina
hizi kabla ya kuibuka kwa watu wanaoitwa akina Bin Kleb, Seif Magari,
Mussa Katabaro na wengineo pale Jangwani.
Lakini maswali yanakuja. Ni kweli Simba haijalipwa
pesa za Okwi? Kama wamelipwa, nani alipokea? Kwa nini SC Villa
wameruhusiwa kumuuza mchezaji ambaye alitajwa kuwa yupo kwa mkopo tu
klabuni kwao kwa ruhusa maalumu kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa
(Fifa)?
Nani hasa alikuwa anammiliki Okwi kati ya SC Villa
ya Uganda na Etoile du Sahel ya Tunisia? Lakini pia kwa sasa kuna mfumo
wa Transfer Matching System (TMS) ambapo jina la mchezaji mwenye
matatizo lisingeweza kukubali kuingia katika orodha ya wachezaji wa
Yanga. Mbona Yanga wamefanikiwa kuliingiza jina la Okwi? Kwa nini
wamepata ITC kama kweli Okwi alikuwa ana matatizo?
Kitanzi katika shingo ya Simba
Alfajiri ambayo kiungo Patrick Mafisango
alifariki, ilidaiwa kwamba dakika chache kabla hajakutana na ajali
alikuwa anakwepa kusaini mkataba mpya na klabu ya Simba huku viongozi
wao wakidaiwa kutembea na dola kadhaa za kumpa Mcongo huyo.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa Mafisango alikuwa na
mpango wa kwenda kucheza nje ya nchi, au kusaini Yanga. Kama kweli
angesaini Yanga, leo Yanga ingekuwa na wachezaji wanne muhimu zaidi
katika kikosi cha Simba kilichotamba miaka mitatu iliyopita wakiunda
‘uti wa mgongo’ wa timu.
Ili timu iwe imara inahitaji kuwa na wachezaji
wanne ambao ukiwapanga uwanjani unapata ‘uti wa mgongo’, yaani kipa,
beki wa kati, kiungo na mshambuliaji.
Kikosi hicho kiliundwa kwa msingi wa kipa, Juma
Kaseja, katika ulinzi, nguzo alikuwa Kelvin Yondani, katika kiungo
msingi alikuwa Mafisango, katika ushambuliaji nguzo alikuwa Okwi.
Mwanaspoti
Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment