KILIMANJARO Stars imeingiza mguu mmoja kwenye robo fainali ya
Chalenji baada ya kuichapa Somalia 1-0 lakini Kim Poulsen amecharuka na
kuwaita kikosini Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Poulsen ametangaza hali ya hatari kwenye mechi
zijazo ikiwemo dhidi ya Burundi keshokutwa Jumatano mjini Nakuru na
kusisitiza hakuna masihara tena kuanzia sasa kwavile mafowadi waliopo
wameshindwa kuonyesha makali.
Bao pekee la Kili Stars lilifungwa na Haruna Chanongo dakika 57 akipokea krosi ya Ramadhani Singano ‘Messi’.
Matokeo hayo ni tofauti na msimu uliopita ambao Stars ikicheza na Somalia tarehe kama ya jana Jumapili iliifunga mabao 7-0.
Kim alisema: “Katika mechi mbili tulizocheza dhidi
ya Zambia na Somalia hakuna straika aliyefunga, ni kiungo na beki. Hii
inamaanisha bado sisi si hatari kwenye ushambuliaji.”
“Nimewaita mastraika Samatta na Ulimwengu watatua
leo (jana Jumapili) jioni na kuanzia mechi na Burundi tutakuwa hatari.
Kwenye hizi mechi zilizopita fowadi yangu haikuwa na madhara jambo
ambalo linafanya tufunge magoli machache na mepesi.
“Hatukuwa na madhara kwa mabeki, lakini ninaamini
kwa ujio wa Samatta na Ulimwengu tutafanya mabadiliko makubwa kwavile
wana uzoefu mkubwa na ni wachezaji ambao wamezoea mashindano, tutakuwa
na madhara sana kuanzia mchezo ujao, hilo ndilo ninaloweza
kuwathibitishia,” alisisitiza kocha huyo ambaye anaitumia michuano hiyo
kuisuka timu kwa fainali za Afrika mwakani.
Katika mechi dhidi ya Somalia, Stars ilitengeneza
nafasi nyingi lakini ikashindwa kumalizia huku wapinzani wao wakicheza
kwa kukamia na kukaba kitimu tofauti na misimu iliyopita.
Stars ilichezesha kikosi chenye badiliko moja tu
ya kile kilichotoka sare ya bao 1-1 na Zambia mjini Machakos. Katika
kikosi cha jana Poulsen alimuweka benchi Hassan Dilunga na kumuanzisha
Athuman Idd katikati akicheza na Frank Domayo.
Stars ilikuwa hivi; Ivo Mapunda, Himid Mao, Erasto
Nyoni, Said Morad, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Aboubakary Salum,
Athuman Idd, Mrisho Ngassa/Mussa Shah, Elius Maguri/Chanongo na Amri
Kiemba/Ramadhani Singano.
Kukamia kwa Somalia kuliwachanganya wachezaji wa
Stars ambao walionekana kupaniki, ingawa kipindi cha pili Mussa Shah,
Chanongo na Messi walibadili mchezo na kwenda sawa na vijana wa Somalia
ambao fowadi yao ilikuwa butu.
Uwanja uliokuwa chepechepe ulikuwa kikwazo cha
Stars kuonyesha mchezo mzuri ingawa pointi nne zimeipa faida ya kunusa
robo fainali.
Mwanaspoti
Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment