Kipa mpya wa Simba, Ivo Mapunda amesema hahofii ushindani
atakaokutana nao kutoka kwa makipa wengine wa timu hiyo na kudai kuwa
yuko tayari kuikabili changamoto hiyo na hatimaye kusimama langoni kama
kipa namba moja.
Mapunda alisaini mkataba wa miaka miwili wa
kujiunga na klabu ya Simba juzi usiku akitokea Gor Mahia ya Kenya,ikiwa
ni saa chache baada ya kuidakia timu ya Taifa ya Tanzania Bara
(Kilimanjaro Stars) katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu dhidi ya
Zambia kwenye Chalenji.
Ni dhahiri, Mapunda aliyewahi pia kuidakia Yanga
atakuwa na kazi ya ziada ya kuthibitisha ubora wake ili aweze kupewa
hadhi ya kuwa kipa wa kwanza Simba na kuwabwaga makipa wengine wa timu
hiyo ambao ni Yaw Berko kutoka Ghana na Abuu Hashim.
Hata hivyo, Berko ambaye alimwaga wino hivi
karibuni kujiunga na Wekundu wa Msimbazi ndiye anaonekana kuwa tishio
kwa Mapunda kutokana na rekodi yake nzuri aliyoiandaa wakati akiichezea
Yanga. Lakini, kipa huyo kasaini mkataba wa miezi sita tu.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu saa chache kabla
ya kuondoka Kenya kurejea Tanzania, Mapunda alisema “sina wasiwasi,
mimi ni kipa mzoefu na hata Watanzania wanajua uwezo wangu.
“Baada ya kusaini, sasa ni kazi tu, kikubwa naomba
ushirikiano na Benchi la Ufundi, uongozi, wachezaji wenzangu na
mashabiki na wadau kwa ujumla,” alisema Mapunda.
Klabu zingine alizowahi kuzichezea Mapunda ni
Tukuyu Stars na Tanzania Prisons za Mbeya, Moro United (Morogoro)
Bandari Mombasa (Kenya) na Saint George ya Ethiopia.
Mapunda pia aliiwezesha Gor Mahia kutwaa ubingwa
wa Ligi Kuu ya Kenya msimu huu ikiwa imepita miaka 18 tangu ilipofanya
hivyo kwa mara ya mwisho.
Wakati huohuo; Simba imesisitiza kwamba sasa
imemaliza kazi baada ya kupata majembe mawili ya maana na sasa inarudi
uwanjani huku beki mpya, Donaldi Mosoti akiahidi kufanya kazi ya
uhakika.
Beki huyo amesaini mkataba wa miaka miwili mbele ya mwanasheria na Katibu wa Simba, Evodius Mtawala mjini Nairobi.
Mtawala alisema: “Tumemaliza usajili sasa tunarudi
uwanjani kufanya kazi.”Mbali na huyo hata kipa namba moja wa Stars, Ivo
Mapunda naye amesaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu kuichezea
Simba.Mapunda alikuwa kipa tegemeo wa Gor Mahia ya Kenya hasa kwenye
penalti sawa na Mosoti ambaye mashabiki wa Gor Mahia hawaamini kwamba
ameondoka.Mosoti alisema jana mjini hapa kwamba: “Nimefurahi sana
kusaini na Simba, nakwenda kufanya kazi na Loga (Zdavko Logarusic)
ambaye nimekaa nae kwa mafanikio Gor Mahia.”
“Nina uzoefu wa kutosha na soka la Afrika
Mashariki na ninadhani nitafanya kazi nzuri na Simba kama Wakenya
wenzangu waliopita, kikubwa ni ushirikiano tu.”Makamu Mwenyekiti wa
Kwanza wa Gor mahia, Faz Ochieng alisisitiza jana kwamba watakaa
kujadiliana nini cha kufanya na hajapata taarifa rasmi za kuondoka kwa
wachezaji hao lakini akakiri mikataba yao inamalizika mwezi huu.
No comments:
Post a Comment