Sanamu hiyo yenye urefu wa mita tisa humuonyesha Mandela akitabasamu, huku akiwa ameonyesha ishara ya kukumbatia.
Wakati akizindua sanamu hiyo jana, Rais Zuma
alisema kwamba sanamu nyingi za Mandela zinamuonyesha akinyoosha mkono
wake mmoja juu kama ishara ya mapambano iliyokuwa ikitumiwa na Chama cha
ANC.
Lakini, ishara ya kukumbatia iliyokuwa ikitumika
katika sanamu hii ni tofauti, kwasababu inamuonyesha Madiba akikumbatia
nchi nzima na watu wake wote bila kujali rangi, itikadi wala tabaka.
Zuma aliizindua sanamu hiyo muda mfupi baada ya kumalizika kwa mazishi
ya kiongozi huyo yaliyoshuhudiwa na umati mkubwa watu mbalimbali,
wakiwamo viongozi wa nchi tofauti yaliyofanyika katika Kijiji cha Qunu.
Katika uzinduzi huo alikuwapo Waziri wa Utamaduni,
Paul Mashatile na familia ya Madiba ambapo Zuma alikuwa na mkewe,
Thobeka Madiba Zuma.
Pia, alikuwapo Makamu wa Rais, Kgalema Motlanthe
na viongozi wengine nchini humo wakishuhudia kuzinduliwa kwa sanamu hiyo
ya historia.
Uzinduzi huo uliofanyika katika jengo hilo, pia ulishuhudiwa na waandishi wa habari kutoka sehemu mbalimbali.
Mandela alizikwa juzi katika kijiji ambacho
alizaliwa cha Qunu, mazishi yake yalihudhuriwa na umati mkubwa wa watu
wakiwamo viongozi mbalimbali duniani.
No comments:
Post a Comment