YANGA imefanya umafia, imemsajili mshambuliaji wa zamani wa
Simba, Emmanuel Okwi kwa mkataba wa miaka miwili na nusu na huenda
akaichezea timu hiyo Jumamosi ijayo katika mechi ya Mtani Jembe dhidi ya
Simba, Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abdallah
Bin Kleb aliliambia Mwanaspoti jana Jumapili jioni kuwa mshambuliaji
huyo amesaini mkataba wa miaka miwili na nusu.
“Kaka ni kweli tumemsajili Okwi, tumepata mpaka ITC yake. Sisi tumemsajili kutoka SC Villa ya Uganda,” alisema Bin Kleb.
Bin Kleb alifafanua kuwa katika suala hilo
wamemshirikisha meneja wa Okwi, wakala wake na mwanasheria na kwamba
mikataba yote imesainiwa.
Usajili huo ni wazi kwamba utawashangaza mahasimu
wao, Simba ambao walikuwa na mgogoro na mchezaji huyo na klabu
waliyomuuza ya Etoile du Sahel ya Tunisia kwa ada ya Dola 300,000 (Sh
480 milioni) fedha ambazo bado hawajalipwa mpaka sasa.
Hata hivyo wakati Simba wakiwa katika mgogoro huo,
Yanga wameibuka na kumsajili mchezaji huyo jana Jumapili saa chache
kabla ya muda uliowekwa na TFF kwa klabu kukamilisha usajili wa
wachezaji wa Ligi Kuu Bara. Klabu zote za Ligi Kuu zilitakiwa kufanya
kusajili wa wachezaji wapya kuanzia Novemba 15 hadi Desemba 15 saa sita
usiku (jana Jumapili).
Okwi kwa mara ya kwanza alisajiliwa na Simba mwaka
2010 akitokea Sports Club Villa ya Uganda kabla ya kumuuza Sahel
Januari mwaka huu lakini tangu Simba wamuuze suala la malipo limekuwa
gumu huku Okwi mwenyewe akilalamika kuidai klabu hiyo mishahara na
marupurupu.
Kutokana na hali hiyo alikubali kusaini SC Villa
mkataba wa miezi sita baada ya klabu hiyo kuomba kibali maalumu Fifa ili
kumtumia kwa lengo kuokoa kipaji chake jambo ambalo viongozi wa Simba
walilipinga na kuahidi kulikatia rufaa Fifa.
Kwa kipindi kirefu Kocha wa Yanga, Ernest Brandts
amekuwa akilalamika kutoridhishwa na safu yake ya ushambuliaji na ni
wazi kwamba usajili wa mshambuliaji huyo utakuwa umemfariji Brandts na
atamtumia vyema kwenye Ligi Kuu Bara mzunguko wa pili na mashindano ya
kimataifa.
Mwanaspoti
Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment