YANGA wamepagawa na tukio la saa 24 zilizopita, Emmanuel Okwi ni
mchezaji wao. Usishangae Ndio kawaida ya timu zetu. Haijalishi kama
kocha anataka au hataki, kitu muhimu ni kumkomoa mtani.
Kuna neno jipya siku hizi linaitwa fursa.
Watanzania mmoja mmoja wanalitumia kwa umakini kuliko klabu zetu
zinavyoweza kulitumia. Fursa ni kujipatia chochote kwa haraka haraka
katika kile ambacho wengine hawajaona.
Kwa mfano, wakati huu huu ambao mashabiki wa Yanga
wamepagawa, walipaswa kukimbilia katika maduka ya klabu yao kununua
jezi ya Okwi 25. Jezi maridadi kabisa ambayo ingeuzwa kuanzia Sh15,000
kwenda juu.
Lakini iko wapi jezi hii? Duka liko wapi? Hakuna
shabiki anayejua. Kinachotokea ni kwamba baada ya muda mfupi wajanja
wataingia katika viwanda vya kijanjajanja Kariakoo na kutoa jezi zao
feki ambazo hazina uhusiano na klabu.
Nasikia mchezaji mwenyewe amechota dola 60,000.
Klabu yake SC Villa imechota dola 20,000. Kwa nini mchezaji asirudishe
kiasi walau nusu ya kiasi kilichotumika kwa mauzo ya jezi na vifaa
vinavyoambatana na jina lake wakati huu mashabiki wakiwa wameingia
wazimu kwa ujio wake?
Hapa ndipo soka la Tanzania lilipopotea tangu
miaka mingi iliyopita. Kila kitu kinaendelea kufanywa kama burudani tu.
Kinafurahisha nafsi za mashabiki kwa macho tu, lakini klabu maarufu
zenye mashabiki zaidi ya milioni tano nchi nzima zinaendelea kuishi kwa
hisani ya watu wachache.
Wakati Arsenal wakimpima afya Mesut Ozil kabla
hajamalizia kusaini mkataba wa timu yao, tayari klabu ilikuwa inaanza
kuchapisha jezi yake namba 11 kwa ajili ya kuanza kupunguza maumivu ya
kumnunua mchezaji huyo kwa bei mbaya.
Nisingeshauri hili kama ningekuwa raia wa Kenya
ambako siasa inapendwa zaidi kuliko soka. Lakini katika nchi yenye
wazimu kama hii, mchezaji kama Okwi anaweza kutumika katika kutengeneza
noti nyingi klabuni.
Hapa naizungumzia nchi maskini yenye wazimu wa
soka inayopatikana katika dunia ya tatu. Hata hivyo bado tunatupa pesa
jalalani na kulalamika kwamba maisha yamekuwa magumu.
Matokeo yake, mpaka leo, mchezaji anasajiliwa kwa
gharama ya dola 80,000 kwa jumla lakini ataenda kufanya mazoezi katika
uwanja mbovu wa Loyola. Klabu haiwezi kujitegemea kwa kutengeneza uwanja
wa kisasa wa mazoezi.
Na kama uwanja ule ule wa Kaunda ungekuwa
umetengamaa, wiki ya kwanza ya mazoezi ya Okwi na Yanga ingeingiza kiasi
cha Sh 10 Milioni. Hizi ni hesabu za wenzetu wenye akili ya kibiashara
zaidi kuliko ya kutegemea mifuko ya watu.
Lakini kwa sasa watu wanaopiga pesa nyingi zaidi
kwa ujio wa Okwi Yanga ni kampuni za magazeti kuliko timu yenyewe. Jina
lake litatumika kutengeneza pesa nzuri kwa siku nyingi zijazo hasa
ukizingatia kuwa hata klabu zenyewe hazina magazeti yaliyotengamaa
kuitengeneza habari na kuiuza.
Natabiri kuwa tutaendelea kutegemea wahisani kwa miaka mingi
ijayo kama hatuwezi kuwa na akili ya haraka ya kutumia rasilimali watu.
Kila siku mchezo wa soka utakuwa unaburudisha mioyo yetu tu, lakini
hatutaweza kuutumia katika kutengeneza pesa.
Kwa wenzetu usajili kama huu ungeinufaisha klabu,
Mmachinga, shabiki wa kawaida na kila mtu. Sisi unamnufaisha mchezaji
peke yake.
Mwanaspoti
Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment