Monday, 16 June 2014

Maximo hawezi kuwa mwarobaini wa Yanga.


MIAKA miwili iliyopita, Chama cha Soka Afrika Kusini (SAFA) kilimwajiri Gordon Igesund kuwa Kocha mkuu wa Bafana Bafana kwa mkataba wa miaka miwili na kukabidhiwa majukumu makubwa mawili.

Jukumu la kwanza lilikuwa ni kuhakikisha timu yake inatinga katika hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) iliyofanyika hapo Bondeni mwaka 2013.

Jukumu la pili ilikuwa ni kuisaidia timu kufuzu Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 zinazoendelea sasa nchini Brazil.

Kwa bahati mbaya sana, Bafana Bafana iliishia hatua ya robo fainali ya mashindano ya Afcon 2013, pia ilishindwa kukata tiketi ya Kombe la Dunia 2014. Kwa mtaji huo, Kocha Igesund alishindwa kutimiza yale yote ambayo aliagizwa na waajiri wake.

Wiki iliyopita, SAFA imetangaza kuwa haitamuongeza mkataba Igesund mara mkataba wake wa sasa utakapomalizika mwishoni mwa mwezi huu. Sababu za uamuzi huo ni kuwa Kocha huyo aliyeaminiwa sana na Wasauzi wakati alipoajiriwa, ameshindwa kutimiza kwa ukamilifu majukumu aliyopewa na waajiri wake.

Turejee nyumbani. Timu ya soka ya Yanga imetangaza kusudio la kumwajiri Marcio Maximo kuwa kocha mkuu kuanzia msimu ujao. Kusudio hilo limepokelewa kwa vifijo na wapenzi wa klabu hiyo kubwa nchini.

Maximo anaaminika na Wanayanga kuwa atakuwa mwarobaini wa timu kuleta vikombe vingi Jangwani. Anaaminika na Wanayanga kuwa atasaidia kupandisha kiwango cha uchezaji kwa timu hiyo ili kufikia kiwango halisi cha kimataifa kama jinsi alivyofanya kwa Taifa Stars enzi zake.

Pia, anaaminika kuwa atarejesha mshikamano wa Wanayanga wote na mapenzi makubwa kwa timu yao kama alivyofanya wakati akiifundisha Stars. Hayo ndiyo matarajio makubwa ya wapenzi na mashabiki wa timu hiyo wanaoungojea kwa hamu ujio wa Maximo kama kweli atakuja.

Swali moja ambalo nimekuwa nikijiuliza mara baada ya Yanga kuja na kusudio hilo ni kwamba, hivi kweli Yanga imewahi kuwa na tatizo la makocha? Hivi ni kweli kuwa kufanya vibaya kwa Yanga kwenye michuano ya kitaifa na kimataifa kunatokana na tatizo la kocha au ni matatizo mengine?

Tangu Yanga ianze kubadili makocha kuanzia kwa Srejodevic Milutin ‘Micho’, Sam Timbe, Dusan Kondic, Tom Saintfiet, Ernest Brandts na wengineo, sijawahi kuona kocha aliyekuwa kimeo kiasi cha kutakiwa kutimuliwa kazi haraka. Makocha wote walikuwa na uwezo mkubwa na historia nzuri, ingawa wote waliishia kutimuliwa mapema.

Sababu kubwa ni kwamba, makocha wote hawa waliingia Yanga bila kupewa hadidu za rejea na matokeo yake wametimuliwa bila kuwa na makosa yoyote. Makocha hawa walitakiwa kukabidhiwa majukumu kama SAFA walivyomkabidhi Igesund. Kushindwa kwao kutekeleza majukumu waliyopewa, ingekuwa ndiyo tiketi yao ya kutimuliwa kazi, labda itokee huruma ya mwajiri wako. Lakini haikuwa hivyo kwa Yanga!

Makocha wengi wa Yanga wametimuliwa kutokana na ama kuwa wakweli kupita kiasi, na wengine kwa kushindwa tu kuifunga Simba. Brandts alitimuliwa huku timu yake ikiongoza ligi, kisha akaajiriwa kocha aliyeishusha timu na kumaliza ligi ikiwa nafasi ya pili. Hapo ni kocha yupi bora kati ya Brandts aliyetimuliwa na huyo aliyemrithi? Nauliza tu.

Maximo anakuja kwa staili ile ile ya watangulizi wake. Kutokana na hali hiyo na kwa mfumo wa uongozi wa sasa, hata wakija akina Maximo kumi, Yanga itabaki kuwa Wahapahapa tu!


Mwanaspoti

No comments:

Post a Comment