Friday, 13 June 2014

Timu za Afrika kufungua kampeini, leo Cameroon.

Baada ya kushuhudia mechi ya kwanza ya fainali ya kombe la dunia la mwaka huu huko Brazil,mamilioni ya mashabiki kutoka bara Afrika hii leo watafungua macho na kupaza sauti zao wawakilishi wa kwanza wa Afrika The Indomitable lions wa Cameroon ikitoana kijasho na Mexico katika mechi ya pili ya kundi A. Timu hizi zimewahi kukutana mara moja pekee kabla ya hii leo.Mexico ilishinda mechi hiyo ya kujipima nguvu kwa bao moja kwa nunge.
Mechi hiyo ilichezwa huko L.Angeles Marekani mwaka wa 1993 ,lakini hii leo hii haitategemea historia wala ukweli kuwa Mexico haijawahji kuishinda timu yeyote ya Afrika katika kombe la dunia ,la dakika tisini katika uwanja wa Arena das Dunas,ulioko Natal ndizo zitakazoamua yupi kati yao ni kidedea.

Kocha wa Mexico Miguel Herrera atakuwa bila ya mshambulizi nyota Javier Hernandez kutokana na kuwa hajafunga bao lolote katika mechi tisa.Kocha huyo atawategemea Giovani dos Santos na Oribe Peralta katika safu ya ushambulizi huku akitarajia Guillermo Ochoa kulinda lango lake.
Kwa upande wao Cameroon ambao walifanya mgomo wa marupurupu kabla ya kuabiri ndege ya Brazil ,nyota wao Samuel Etoo anatarajiwa kuanza katika mechi hii licha ya kuwa hayuko timamu kiafya.
The indomitable Lions walifuzu kwa mashindano haya baada ya FIFA kubatilisha matokeo ya kichapo mikononi mwa Togo.

Kocha Volker Finke anakabiliwa na changamoto ya mshikamano wa timu yake iliyowasili Brazil siku nne tu zilizopita baada ya mgomo huo wa marupurupu.Timu yake ndiyo yenye kushikilia rekodi ya kushindwa mara nyingi kuliko timu zote.Cameroon imepoteza mechi 24 na kushinda mechi moja pekee kati ya 13 ilizoshiriki.
Cameroon iliilaza Saudi Arabia bao 1-0 mwaka wa 2002.Katika mashindano haya Camerooon imemshirikisha mchezaji mchanga zaidi katika kikosi chao Fabrice Olinga mwenye umri wa miaka 18.

 Uhispania vs Uholanzi

 Mechi nyengine itakayokuwa ikitazamiwa na mamilioni ya mashabiki kote duniani ni Mabingwa watetezi wa kombe la dunia Uhispania .
Mabingwa hao huko Afrika Kusini mwaka wa 2010 wanafungua kampeini yao dhidi ya Uholanzi katika Arena Fonte Nova, Salvador.
Mechi hii itakuwa kumbukumbu ya fainali miaka minne iliyopita lakini Kocha wa Uhispania Vicente del Bosque hana sababu ya kuwa na wasiwasi kwani anajivunia kikosi dhabiti kinachosheheni mabingwa wa dunia mabingwa wa kombe la Ulaya na mabingwa wa taji la bara Uropa.
kati ya mechi kumi walizochuana Uhispania imeishinda Uholanzi mara tano na ikashindwa mara nne.
Kocha mpya wa Manchester United na Uholanzi Louis van Gaal anamtegemea nyota wa united Robin van Persie Wesley Sneijder na Dirk Kuyt kudhibiti tikitaka ya wahispania.
Bila shaka ukitaka kutizama janja na janjaure basi kaa kitako usubiri mechi hii.
Mechi ya mwisho hii leo itakuwa ya baina ya Chile na Australia.
Kinyume na mechi baina ya Uhispania na Uholanzi itakayoshuhudia tiki taka mechi baina ya chile na Australia inatarajiwa kuwa ya kasi na nguvu kutokana na mifumo ya timu hizo mbili.

 Chile dhidi ya Australia

Australia haijawahi kushinda mechi yeyote ya kombe la dunia wala alama yeyote ila ile waliojinyakulia mwaka wa 1974 walipotoka sare ya suluhu bin suluhu dhidi ya CHILE
'The Socceroos' wameshindwa na Chile katika mechi zao zote za kujipima nguvu.
Australia ambayo inaorodheshwa katika nafasi ya 62 katika orodha ya timu bora na shirikisho la soka duniani FIFA, ndiyo timu ya chini kabisa katika orodha hiyo ya FIFA inayoshiriki katika mashindano haya huko Brazil.
Kwa upande wao Chile wamewahi kushinda mechi mbili pekee kati ya 17 walizocheza za kombe la dunia.
Chile ilizilaza Honduras na Switzerland huko Afrika kusini mwaka wa 2010.
Wanamtegemea nyota wao Arturo Vidal kuwafungia mabao .
Australia kwa upande wao wanawategemea Mark Bresciano na Tim Cahill kusonga mbele katika hatua ya makundi

No comments:

Post a Comment