Monday 16 June 2014

Yafuatayo baadhi ya mambo ambayo unapaswa kuyafanya baada ya kubaini kuwa mpenzi wako amekusaliti.


Kubaliana na kilichotokea


Kama keshakusaliti ni tukio ambao limeshatokea na haliwezi kufutika. Kubali kuwa umetendwa, huzunika lakini mwisho liache lipite ili uweze kujipanga upya.

Usijilaumu

Wapo ambao wakishasalitiwa hujuta kukubali kuingia kwenye uhusiano na watu waliowatenda. Utamsikia mtu akisema “najuta kumkubalia awe mpenzi wangu”. Kujilaumu kwa namna hiyo hukutakiwi kwani kutakufanya uzidi kunyong’onyea.

Jitoe

Jifanye kama vile aliyesalitiwa siyo wewe bali ni rafiki yako kisha jiulize ungemshaurije? Ushauri ambao ungempa basi uchukue kisha uufanyie kazi.

Pima ulivyoathirika

Je, kitendo cha mpenzi wako kukusaliti kimekukosesha imani juu yake? Kama ni hivyo, unadhani una sababu ya kuendelea kuwa naye au unahisi madhara aliyokupatia huwezi kumvumilia?

Mweleze ukweli

Kwa vyovyote utakavyoamua ni lazima umweleze ukweli juu namna alivyokuumiza kwa usaliti wake. Hata kama utampa nafasi nyingine lazima ajue jinsi alivyokuumiza ili iwe changamoto kwake.

Chunguza kwa nini kakusaliti

Usiliache likapita hivi hivi, unatakiwa kujua sababu ya yeye kukusaliti. Je, kuna ambacho anakikosa kwako au ni tamaa zake tu? Jibu utakalolipata litakusaidia katika maisha yako ya kimapenzi.

Usikubali akulainishe

Huenda huyo mpenzi wako ni msanii na anaweza kukulainisha kwa maneno ambayo yanaweza kukufanya ukalichukulia tukio hilo kiurahisi. Kuwa na msimamo na eleza hisia zako kwa uwazi.

Amua kusuka au kunyoa

Likishatokea hilo jaribu kuzungumza na moyo wako. Uamuzi wa kuendelea kuwa naye au kumuacha uuchukue bila shinikizo. Hata kama kakuumiza, kama unadhani unaweza kumpa nafasi nyingine mpe ili usije ukajuta baadaye kwa kumkosa lakini kama unaona moyo wako unamkataa, muache.

Msamehe

Kwa uamuzi wowote utakaochukua ni lazima uwe tayari kumsamehe ili kuliondoa dukuduku lako rohoni. Kutokumsamehe kunaweza kukufanya ukawa unaumia kila wakati na kukosa amani.

Iwe fundisho kwako

Chukulia tukio hilo kama fundisho kwako. Huenda wewe ndiye uliyechangia kusalitiwa, kama ni hivyo badilika ili yasije yakakukuta kama hayo utakapokuwa na mwingine. Pia kama kusalitiwa kumetokana na kutoridhika kwa mpenzi wako, kuwa makini wakati wa kuchagua mwingine wa kuwa naye.

No comments:

Post a Comment