Friday 2 May 2014

Anayeendesha maisha kwa kutegemea urefu wa kucha.


Inaweza kuonekana kuwa ni kitu cha ajabu kwa binadamu wa kawaida kukaa bila kukata kucha kwa mwaka moja, lakini kumbe inawezekana kabisa mtu kufuga kucha kwa muda wa miaka 12.
Hilo limedhihirishwa na John Waweru, raia wa Kenya ambaye amefanikiwa kufuga kucha zake kwa muda wa miaka 12 na kufikia urefu wa futi moja na inchi 3.
Katika mahojiano yake na gazeti la Nairobi News, Waweru anaweka bayana kuwa kucha hizo ndizo zimekuwa chanzo kikuu cha kumwingizia kipato.
Anasema amefanikiwa kuzigeuza kucha hizo kuwa mojawapo ya kivutio cha utalii nchini Kenya kutokana na kuwafanya watalii kuzishangaa na hivyo kumpatia pesa kama malipo ya kivutio hicho.
Ili kuzidi kuwavutia watalii Waweru amezipaka kucha zake rangi zilizopo katika bendera ya Kenya hali inayomwongezea mvuto zaidi.
“Nimezipaka rangi ya bendera yetu kwa kuwa watalii wengi wanaokuja kupiga picha na mimi wanazipenda rangi hizo ili kuwafurahisha wateja wangu,” anasema Waweru akiongea na Kenya News
Anasema siku biashara ikiwa nzuri ana uhakika wa kurudi nyumbani na Sh5,000 (sawa na Sh94,000 za Kitanzania).
Waweru (33) anasema tangu mwaka 2002 alipoanza kufuga kucha hizo hajawahi kuzikata wala kuzipunguza kutokana na sababu yoyote ile.
“Baada ya kumaliza shule nilipata kazi lakini kucha zikawa zinakua kwa kasi kiasi cha kunifanya nishindwe kutimiza majukumu yangu nikaona bora niache kazi ili ziendelee kukua bila kikwazo chochote, nazilinda sitaki zikatike kwa namna yoyote.”
Anafafanua kuwa kikubwa anachokifanya ni kuilinda rasilimali hiyo akiamini kuwa ndiyo mtaji wake, hivyo siku zote hujaribu kujiweka mbali na ugomvi au hatari yoyote itakayosababisha kucha hizo kukatika.
“Tangu nimeanza kufuga kucha nimekuwa mtulivu mno. Najiweka mbali na ugomvi ili nisije kupoteza chanzo changu cha mapato. Nafahamu fika kuwa kupigana kunaweza kusababisha kucha zangu zikatike kitu ambacho sitaki kitokee,” anasema.
“Hata pombe nimeacha kunywa. Najaribu kufanya kila linalowezekana ili kucha zangu zisiingie kwenye hatari na huwa nazifunika kuziepusha na
purukushani.”
Kutokana na urefu wa kucha hizo, Waweru anashindwa kufanya baadhi ya shughuli zake kama vile kufua, kupika na kazi nyingine za mikono hivyo amelazimika kumwajiri kijana.
Mlo
Waweru analazimika kula vyakula maalumu vyenye madini ya ‘Calcium ‘ambayo kwa kiasi kikubwa husaidia kucha kuwa imara.
“Kwa kuwa nataka kucha zangu zizidi kukua na kuwa imara nalazimika kula vyakula ambavyo ninaweza kupata madini ya ‘calcium’ na vilevile nahakikisha nakunywa maziwa na maji ya kutosha”
Kuhusu familia anasema kuwa hana mke, lakini anaye mpenzi ambaye ameridhika na namna alivyo na siku zote amekuwa akimuunga mkono kwa kila anachokifanya.
Anaeleza kuwa imekuwa kawaida kwake anapoamka asubuhi na kuanza safari kwenda kwenye vituo vya utalii ambako hukutana na watu mbalimbali wanaotaka kuona kucha zake na kupiga naye picha.
Licha ya kuwapo Wakenya ambao pia huvutiwa na kucha zake, wapo baadhi yao ambao huzihusisha na imani za kishirikina na kumhisi kuwa mchawi.
“Nimekuwa nikikutana na changamoto mbalimbali hata kutoka kwa ndugu zangu wakinitupia vijembe kuwa kucha zangu ni ishara ya kumwabudu shetani.”
Hata hivyo, Waweru amekuwa akitupilia mbali madai hayo kutokana na malengo ambayo amejiwekea na namna ambavyo kucha hizo zimekuwa mkombozi wa maisha yake.
Mafanikio
“Ninachoamini ni kuwa kucha zangu ni kivutio cha utalii kwahiyo siwezi kuchukulia maneno hayo kama sababu ya kunirudisha nyuma. Zimenisaidia sana kubadili maisha yangu sina kazi ninayofanya lakini naweza kumudu gharama za maisha,” anasema Waweru
Kupitia pesa amefanikiwa kujenga nyumba ya vyumba vinne ambavyo amevipangisha. Vilevile ameweza kufungua saluni inayohusika na utengenezaji wa kucha ambayo pia imekuwa sehemu ya kumwingizia kipato.
Anawasihi vijana kutokujibweteka kusubiri kazi za kuajiriwa au kutegema siku zote kukaa ofisini na badala yake kutafuta namna nyingine za kuwaingizia kipato kama ambavyo amefanya yeye.
Waweru anaamini kuwa ana kucha ndefu kuliko wote barani Afrika na matarajio yake siku moja ni kumfikia na hata kumpita Lee Redmond, ambaye ameingizwa kwenye Guiness Book of Records.
Mwananchi.

No comments:

Post a Comment