Friday 2 May 2014

Nyalandu amtimua Mkurugenzi Wanyamapori Kamati ya Bunge.


Hatua ya kurejeshwa kazini Mkurugenzi wa Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa baada ya kutimuliwa kazi na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu imeibua mapya baada ya mkurugenzi huyo kutimuliwa katika Kamati ya Bunge jana.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira walikubaliana na pendekezo la Nyalandu kutaka Profesa Songorwa asijitambulishe katika kikao cha kamati hiyo kwa kuwa hakuwa anatambulika.
Sakata hilo lilitokea wakati kigogo huyo na watendaji wengine walipokuwa wakijitambulisha kabla ya kuanza kwa kikao cha kamati hiyo kilichokuwa kikijadili Bajeti ya Serikali mwaka 2014/15.
Februari mwaka huu, Profesa Songorwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Jafari Kidegesho walisimamishwa kazi na Nyalandu akisema ni utekelezaji wa azimio la Bunge katika Ripoti ya Operesheni Tokomeza Ujangili.
Hata hivyo, watendaji hao, walirejeshwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza kwamba baada ya Nyalandu kukataa kumtambua, wajumbe walimuunga mkono wakisema nao hawamtambui kwa sababu hatua aliyochukuliwa ilitokana na uamuzi uliofikiwa na Kamati ya Operesheni Tokomeza, ambayo ni sehemu ya Kamati hiyo ya Bunge.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Nyalandu alikiri kumzuia Songorwa kujitambulisha: “Kwanza sikujua kama angekuwapo katika kikao kile, maana suala lake bado hatujalizungumza ofisini. Sikuona sababu ya yeye kujitambulisha. Tukirejea ofisini tutalizungumza na kazi zitaendelea kama kawaida, ila azimio la Bunge dhidi yake lipo wazi. Uamuzi haurudi nyuma na itabidi apangiwe kazi nyingine.”
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli alishindwa kukiri wala kukataa kutokea kwa jambo hilo zaidi ya kusema jambo hilo iulizwe Wizara ya Maliasili na Utalii.Profesa Songorwa hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo na simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila majibu.
Mwananchi

No comments:

Post a Comment