KWANZA walisikia straika Didier Kavumbagu amesaini Azam FC wakashituka, baadaye wakapotezea. Lakini Jumatano mchana waliposikia Frank Domayo naye amesaini huko wakachanganyikiwa wakaitana ghafla klabuni.
Hao ni wazee wa Yanga ya Dar es Salaam ambao wametoa onyo kali na kusema kwamba wachezaji wao wote wawe huru kuondoka, lakini endapo beki Mbuyu Twite na kipa Deo Munishi ‘Dida’ wakiondoka tu, patachimbika.
Wazee hao wamesisitiza kwamba wameupa uongozi angalizo kwamba wafanye wanavyoweza wachezaji hao wasiondoke Yanga na kama ikishindikana watazungumza mambo mengine.
Twite yuko kwenye mazungumzo na Azam ambapo amewashinikiza Yanga wampe Sh80 milioni asaini mkataba mpya, jambo ambalo viongozi hawakubaliani nalo kwa madai kwamba mchezaji huyo licha ya kwamba ni kiraka lakini umri umemtupa.
Ndani ya wiki klabu ya Yanga imepata pigo kwa kuchukuliwa wachezaji wake Kavumbagu na Domayo huku baadhi ya wanachama wakionekana kuchanganyikiwa na kutoelewa ni nini kimetokea ingawa Mwanaspoti linajua kwamba viongozi wa Yanga walizidiwa kete licha ya harakati zao za kupambana.
Kavumbagu na Domayo wamesaini mikataba mipya ya miaka miwili kila mmoja na mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Azam hivyo wapo tayari kuitumikia klabu hiyo msimu ujao wa ligi 2014/15.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu wa Baraza la Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali, alisema kuondoka kwa wachezaji hao kumewashitua huku akisisitiza kuwa viongozi wa Yanga wafanye kila wanaloweza kuhakikisha Twite na Dida wanabaki kwenye himaya yao.
Akilimali ambaye ana ushawishi mkubwa kwa wanachama wakongwe, alisema juzi Jumatano wazee walikutana katika Makao Makuu ya klabu hiyo kujadili juu ya uchaguzi wao ujao pamoja na kufanya tathimini ya ligi kuu msimu uliopita lakini kikao hicho hakikuweza kumalizika baada ya kuingilia habari za usajili.
“Hawa wote waondoke tu, ila wazee tutaumia sana endapo Twite na Dida wataondoka Yanga, sijui kilio chetu kitakuwaje na sijui nini kitatokea ndani ya Yanga, hivyo viongozi wetu wafanye wawezalo kuhakikisha wanawazuia wachezaji hao,” alisema.
“Tumeshika nafasi ya pili kwenye ligi jambo ambalo lilituhuzunisha sana, ila hatuwezi kulipinga kwani ndiyo mpira lakini sasa hivi tunaanza kupata picha kwamba huenda hata wachezaji hawakuwa na malengo, labda tayari walikuwa wameshawishiwa, hivyo waache waende tubaki na wale wazalendo na wataitumikia Yanga kwa moyo mmoja,” alisema Akilimali.
Akifafanua zaidi juu ya Twite, Mzee Akilimali alisema kuwa “Twite ni mchezaji mwenye nidhamu kubwa na anajituma, tunatamani angekuwa ndiye nahodha wa timu yetu ila haiwezekani kwa sababu siyo raia wa Tanzania, Twite haonyeshi tamaa ya fedha anaonyesha kipaji.
“Tumesikia Azam wanamtaka Twite ndiyo maana tumeweka wazi kuwa viongozi wahakikishe anabaki kuichezea Yanga, bado tunamuhitaji sana kutusaidia,” alisema Akilimali huku akisema wamesimama kujadili mambo ya uchaguzi mpaka Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji atakaporejea nchini.
Twite amekiri kufanya vikao viwili juzi Jumatano na viongozi wa Yanga vyenye agenda moja ya usajili na kushindwa kukubaliana lakini akasema anatoa siku mbili vinginevyo kuna maamuzi mawili atayafanya.
Twite raia wa Rwanda, ameliambia Mwanaspoti kuwa anahitaji kubaki katika klabu hiyo lakini kama ataendelea kuona muafaka unashindwa kupatikana atatafuta tiketi ya ndege na kuondoka nchini haraka kurudi kwao Rwanda na baadaye atatimkia DR Congo.
“Ni kweli nimezungumza na viongozi wa Yanga, nimefanya nao vikao viwili muhimu, nikiona bado hali inaendelea hivi muafaka haupatikani ni vyema nikaondoka hapa Tanzania nirudi nyumbani ambako nitafanya maamuzi,” alisema Twite.
“Unajua nawaheshimu sana mashabiki wa Yanga lakini sitaki kuzungumzia hizo habari za Azam mimi ndiyo najua ukweli, nasema katika siku mbili hizi kutoka leo (jana Alhamisi) ningependa kuona Yanga wanahitimisha hili vinginevyo inawezekana kabla ya kuondoka au baada ya kuondoka nitachukua maamuzi yangu.
“Hapa ni rahisi watu kukushushia lawama lakini hawaangalii ni jinsi gani mtu unavyovumilia, mimi ni mchezaji ninayejiheshimu najua ninachotaka najua nani ananihitaji, sina matatizo nikibaki Yanga lakini lazima ieleweke siwezi kucheza Yanga bila ya kuwa na mkataba ambao mimi nitakubaliana nao,”alisisitiza Twite.
No comments:
Post a Comment