Friday 2 May 2014

Msuva: Nina siri tatu hamzijui.


WINGA Simon Msuva ameweka wazi mambo matatu yaliyomfanya ang’are kwenye kikosi cha Yanga msimu huu na kuzima kelele za mashabiki waliokuwa wakimlaumu kwa makosa kadhaa mara kwa mara.
Msuva alikuwa akilaumiwa kwa makosa kadhaa mzunguko wa kwanza msimu uliopita lakini baadaye akabadilika na akamaliza ligi akiwa tegemeo kikosini.
Alipozungumza na Mwanaspoti, Msuva alisema: “Kwanza nilijifunza kitu kuwa mashabiki wanataka mambo mazuri tu na siyo mabaya. Kupitia wao nikawa kila ninapokuwa uwanjani, nahakikisha najituma kwa nguvu zangu zote na kurekebisha makosa yote ambayo nilikuwa nayafanya nao wanayakemea ili nisiwaangushe.”
“Pili nimekuwa nafanya sana mazoezi yangu binafsi mbali na yale ninayokuwa nafanya pamoja na timu, hata kama ninapokuwa kambini huwa nafanya na zaidi ni kukimbia kutengeneza stamina na kasi ndiyo maana uwanjani nakuwa fiti,”alisema Msuva.
“Lakini cha tatu ni kufuata maelekezo ya kocha kwa kutimiza kila kitu ambacho anakihitaji. Kama unavyojua kila kocha anastahili yake ya ufundishaji, vile unavyomfuata ndiyo unakwenda naye sawa,”alisema Msuva ambaye uwepo wake umeongeza kasi kwenye fowadi ya Yanga hasa anaposimama na winga mwenzake, Mrisho Ngassa.

No comments:

Post a Comment