KIKOSI cha timu ya soka ya Al Ahly ya Misri, kitafikia kwenye
hoteli ya kifahari ya Kempinski jijini Dar es Salaam, lakini kwenye
msafara wao watakuja na mpishi wao maalumu.
Timu hiyo ya Misri imepanga kutua Dar es Salaam
leo Jumanne ingawa haijawapa taarifa Yanga na tayari maofisa wao wapo
jijini wakiandaa mazingira.
Hata hivyo timu hiyo imezuga kwenye mitandao yao
kwamba hawako vizuri kiuchumi kwa sasa na kwamba hata Sh112 milioni
walizotumia kwa safari ya kuja nchini wamezipata kwa kuungaunga.
Al Ahly inayowasili na msafara wa watu 32 miongoni
mwao wachezaji wakiwa 22 na viongozi 10, mpishi wao ni raia wa
Ujerumani ambaye atashirikiana na wataalamu wa hoteli hiyo.
Timu hiyo ilizikataa hoteli tano za awali
ilizotafutiwa na Yanga kwa madai kwamba zina vyumba vidogo. Ikiwatumia
maofisa kadhaa wa ubalozi wa Misri nchini, Al Ahly iliamua kuchagua
hoteli hiyo huku ikipata uwanja wa mazoezi katika Shule ya Kimataifa ya
Tanganyika (IST), Masaki sehemu ambayo ina ulinzi mkali na mashabiki
hawaingii kirahisi.
Mkurugenzi wa Michezo wa Al Ahly, Sayyid Abdul
Hafiyz, alitarajiwa kuwasili jana Jumatatu kuungana na maofisa wengine
waliotangulia.
No comments:
Post a Comment