HARAKATI za mageuzi nchini zina historia ndefu, zikianza kabla
ya uhuru ambapo wa wananchi kupitia vyama na vuguvugu za aina mbalimbali
waliungana ili kuwaondoa wakoloni.
Hadi mwaka 1961 chama cha Tanu kilichokuwa kikiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere kilishinda uchaguzi na kuunda Serikali.
Vyama vingine vilivyokuwepo ni pamoja na AMNUT, ANC na UTP.
Baada ya Mwalimu kuunda Serikali, alifanya
mabadiliko kadhaa ambapo mwaka 1965 alifuta mfumo wa vyama vingi na
kukifanya chama cha Tanu kushika hatamu za uongozi.
Mbali na kufutwa kwa mfumo huo, pia uhuru wa
vyombo vya habari na uhuru wa asasi za kiraia ulidhoofishwa huku jumuiya
mbalimbali za kiraia zikichukuliwa na kuwa jumuiya za Tanu.
Hata hivyo, hatua hiyo haikuwafurahisha baadhi ya watu akiwemo James Mapalala ambaye kwa wakati huo alikuwa ni mwalimu.
Mapambano yalipoanza
Akizungumza maisha yake hivi karibuni, Mapalala
anasema aliamua kupambana na mfumo huo kutokana na ukandamizwaji wa haki
za binadamu uliokuwa ukifanywa na Serikali tangu ngazi za juu hadi
chini.
“Nilianza mapambano yangu rasmi mwaka 1968 wakati
huo nikiandika makala katika Gazeti la Kiongozi wakati huo nikiwa naishi
Tabora. Nilieleza kutoridhishwa na mateso wanayopata wananchi wakati
huo ingawa kwa kweli Mwalimu Nyerere alikuwa na nia njema tu,” anasema
Mapalala na kuongeza:
“Viongozi wa vijiji wakati ule walikuwa wakitesa wananchi na mimi niliandika kila kilichotokea.”
Kutokana na hali hiyo Mapalala alijikuta matatizoni na kufungwa jela katika gereza la Uyui na huo ulikuwa ni mkasa wa kwanza.
“Mkuu wa mkoa wakati huo akiitwa Makinda ambaye ni baba wa spika wa sasa, Anna Makinda, aliniweka jela.
Nilikaa kwa muda fulani hadi maaskofu na mashehe wa mkoa huo
waliponihurumia na kumwandikia barua Mwalimu Nyerere kumwomba nitolewe,”
anasema.
Anasema ombi hilo lilikubaliwa na Mwalimu Nyerere na hivyo kutolewa.
Hapo alifungua ukurasa mwingine ambapo kutokana na
taaluma yake ya ualimu, aliomba na kupata kazi katika Shirika na la
Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) mwaka 1971.
“Nilitakiwa kwenda kufundisha Nigeria, hivyo
nikaenda kuripoti kisha nikarudi ili niichukue familia yangu.
Niliporudi, Jumapili moja nikiwa kanisani pale St. Peter, Oysterbay
nikakutana na Nyerere… akaniita na kuniuliza, ‘nasikia unataka
kuondoka?’ nikamjibu ni kweli. Akaniambia nisiondoke kuna kazi atanipa,
hivyo niripoti ofisi za Tanu pale Lumumba siku iliyofuata,” anasema.
Anasema siku hiyo alipofika ofisini hapo,
aliwakuta maofisa wa chama ambao walimpangia kazi ya kununua na kuuza
ng’ombe kutoka mikoani.
“Niliifanya kazi ile kwa shingo upande kwa miaka
miwili kisha nikaiacha. Hapo tena ile kazi yangu ya Unesco ikaota
mbawa,” anasema.
Anasema tangu wakati huo alianza kufanya kazi zake
binafsi ikiwa ni pamoja na kuwa mkandarasi wa majengo ambapo anasema
aliwahi kupata zabuni ya kujenga maghorofa ya bandari.
Hata hivyo anasema ilipofika mwaka 1983, mapambano
yake yakaanza tena ambapo wakati huo kulikuwa na mkutano wa wanasheria
jijini Dar es Salaam ambao pia walimkaribisha.
“Wakati huo kulikuwa na wanasheria kutoka katika
Chama cha Tanganyika Law Society walinialika kwenye mkutano uliokuwa
ukizungumzia matatizo ya demokrasia nchini. Walizungumzia matatizo ya
mfumo wa chama kimoja, lakini hawakutoa suluhisho. Mimi nilipendekeza
uanzishwe mfumo wa vyama vingi nchini,” anasema Mapalala.
Hata hivyo, pendekezo hilo halikutiliwa maanani
hadi mwaka 1984 wakati Chama Cha Mapinduzi kikiwa na mkutano mkuu ambapo
Mapalala alifanya tena ‘uchokozi’ wake.
“Mwaka 1984 nilimwandikia barua Mwalimu Nyerere
wakati wa mkutano mkuu wa CCM nikimtaka kuanzishwa kwa mfumo wa vyama
vingi. Hapo ndipo matatizo yakaanza kwani niliwekwa kizuizini. Nilikuwa
nikihamishwa kutoka kituo kimoja cha polisi hadi kingine kwa karibu
mwaka mmoja. Lakini zikufunguliwa kesi yoyote,” anasema.
Anaongeza kuwa mwaka 1986, aliyekuwa Waziri wa
Mambo ya Ndani, Muhidin Kimario alimkamata na kumfunga minyororo na
kumpeleka kizuizini mkoani Lindi ambako alikaa hadi mwaka 1990 na wakati
huo nilikuwa nikihamishiwa kisiwani Mafia.
Licha ya matatizo yote hayo Mapalala anasema hakukata tamaa na mawazo yake ya kuanzisha mfumo wa vyama vingi.
“Baada ya kutoka kizuizini, nilirudi tena na
mawazo ya kuanzisha chama cha siasa. Nilikuwa na wenzangu ambapo
tulianzisha chama wakati hakukuwa na sheria ya vyama vingi,” anasema na
kuongeza:
“Hatukuogopa, tulikwenda kwa Waziri wa Mambo ya
Ndani, wakati huo Augustine Mrema na kumweleza haja yetu hiyo. Mrema
alikuwa mkali sana akatufokea na kutufukuza.”
Baada ya kuona hivyo anasema waliamua kuandamana wakidai haki ya kuanzisha chama cha siasa,
“Tulikuwa watu 35 hivi, wakati maandamano yetu
yanaanza. Tulipokuwa tukikaribia Kariakoo, watu waliongezeka na kufika
hadi 1,000. Polisi wakaingilia kati na kuwakamata watu 25, mimi
nikakimbilia Ubalozi wa Sweden kujificha.”
Anaendelea kusema kuwa, wale wanachama
waliokamatwa na kupelekwa mahabusu waligoma kula kwa siku kadhaa na
kuanza kuitisha Serikali.
“Ilibidi Serikali ije kuniomba niwasihi wale
chakula. Ikabidi kitolewe chakula kizuri tena kutoka Kilimanjaro Hotel
na kupelekwa gerezani na kuwabembeleza kula,” anasema.
Wakati mivutano hiyo ikiendelea, tayari
kulishaanza kujitokeza mabadiliko ya kisasa na kiuchumi ulimwenguni
ambapo mfumo wa ukomunisti ulianza kuanguka.
Kuanzisha, kufukuzwa CUF
Baada ya misukosuko ndipo walianzisha chama chao rasmi kikitwa Chama cha Wananchi (CUF) mwaka 1991.
Baada ya Serikali kupitisha sheria ya vyama vingi
mwaka 1992, Mapalala anasema wanaharakati wengine wa mageuzi walikutana
ukumbi wa Diamond Jubilee mwaka huo na kuanzisha chama cha NCCR-Mageuzi.
Hata hivyo, anasema mwaka huo kulikuwa na chama
kingine huko Zanzibar cha ZUF (Zanzibar United Front) ambacho kilitaka
kuunganisha nguvu na chama cha bara ili kiwe cha kitaifa.
“Walipokuja bara kuangalia chama chenye nguvu, wakaridhika na
chama chetu na kuomba tuungane. Halmashauri kuu za vyama vyetu zikakaa
kujadili suala hilo na hatimaye kukubaliana. Mwaka 1993 niliteuliwa kuwa
Mwenyekiti wa Taifa wa CUF iliyoungana,” anasema.
Baada ya hapo anasema alifanya ziara katika mikoa karibu yote ya bara na Zanzibar kwa ajili ya kukitangaza chama hicho.
Hata hivyo, bahati haikuwa yake, anasema ilipofika
mwaka 1994 mambo yakabadilika kwani wenzake hasa viongozi wa Zanzibar
wakamgeuka na kuanza kumtuhumu kuwa anakisaliti chama.
Lakini mwenyewe anasema ilikuwa ni sababu za kidini pamoja na mkono wa Serikali uliokuwa ukiendelea kumwandama.
“Nilifukuzwa CUF kwa sababu za kidini tu. Ilikuwa
mwaka 1994 baada ya kukijenga chama hicho nikashangaa mambo yamebadilika
na viongozi wenzangu wamenigeuka. Wakawa wananishutumu kuwa natumiwa na
CCM, mara nimechana bendera za chama, na tuhuma nyingi tu. Lakini
nilipata hadi nyaraka zilizothibitisha sababu za udini,” anasema na
kuongeza:
“Wakati huo CUF ilikuwa ikifadhiliwa na nchi za
kiarabu, kwa hiyo wakasema ‘mtatakaje msaada wakati chama kinaongozwa na
kafiri?’ Ndipo vituko vikaanza. Lakini hata Serikali pia ilichangia,
nakumbuka siku ya mkutano wa kunifukuza kule Tanga, Msajili wa vyama vya
siasa wakati huo, George Liundi alikuwepo hadi saa tisa za usiku
akishadadia kufukuzwa kwangu.”
Baada ya kufukuzwa Mapalala akaanza upya tena
mikakati ya kuanzisha chama kingine. Hata hivyo ilimchukua muda mrefu
hadi mwaka 2003 ambapo alianzisha Chama cha Haki na Ustawi alichonacho
hadi sasa.
Tangu alipokianzisha alifanikiwa kupata diwani
mmoja tu mkoani Mara mwaka 2005 ambaye hata hivyo hakuendelea baada ya
kumaliza miaka yake mitano.
Mapalala anazungumzia pia tukio la kunyang’anywa
nyumba aliyokuwa akiishi maeneo ya Morocco jijini Dar es Salaam kwa amri
ya mahakama mwaka 2010, na kulihusisha na misukosuko aliyoipata katika
harakati za kuleta mageuzi nchini.
“Hapa unapoona ninaishi kwenye mabanda ya ng’ombe,
baada ya nyumba yangu kubomolewa kwa amri ya mahakama, yaani ni
misukosuko tu. Chama changu kinanitegemea kifedha lakini kwa hali hii
inaniwia vigumu kukisaidia,” anasema.
Anazungumziaje upinzani wa sasa?
Akizungumzia vyama vya upinzani vya sasa, Mapalala
anasema kuwa vimejikita zaidi kwenye kutafuta madaraka badala ya
kueleza sera zao kwa wananchi.“Tofauti kati ya upinzani tuliokuwa tukiupigania miaka ile na wa sasa,
ni watu kuwa na mawazo ya kwenda Ikulu tu bila kusema watawafanyia nini
wananchi baada ya kufika huko. Hata kwenye chama tawala, CCM, hali ni
hiyo hiyo, watu wanalilia tu Ikulu. Sisi tunasisitiza sera tu… sera
nzuri ndiyo zitakazouza chama, chema chajiuza kibaya chajitembeza,”
anasema.
Mwananchi
Mwananchi
No comments:
Post a Comment