Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba ametoboa madudu
aliyoyaona kipindi kifupi alichokaa kwenye ofisi hiyo baada ya kuapisha
hivi karibuni.
Alisema amegundua sheria ya ununuzi ni uchochoro wa wizi wa kistaarabu unaotishia ustawi wa taifa.
Mwigulu alisema ni wizi wa kutisha kuona mtu
binafsi akinunua soksi dukani analipa Sh2,000, lakini akitumia sheria ya
ununuzi soksi ya aina ileile itanunuliwa kwa Sh80,000.
Alisema sheria hiyo ni mzigo mzito kwa Serikali na
kutoa mfano mwingine kwamba, waziri mmoja alikwenda safari ya kikazi
nje ya nchi, lakini aliamua kwenda na mkewe kwa gharama zake alimlipia
Sh1 milioni, lakini yeye kwa utaratibu sheria ya ununuzi alilipiwa na
Serikali tiketi ya Sh4 milioni wakati walikuwa ndege moja na viti
vinavyofuatana.
Mwigulu alisema hayo juzi jioni alipozungumza na
wafanyabiashara jijini hapa kupitia Chama cha Wafanyabiashara Wenye
Viwanda na Kilimo (TCCIA), huku wakimweleza kuwa sera mbaya ya kodi
ndiyo inayosababisha watu wengi kukwepa ulipaji kodi.
‘Nakiri kwamba kweli ipo haja ya kurekebisha
sheria ya kodi na sera yake, kutokana na mambo ninayoyaona na
yatafanyiwa kazi kipindi kifupi kijaacho,’’ alisema.
Mwigulu alisema kwa kuanza utekelezaji, tayari
amewaagiza maofisa wa wizara wamwandalie orodha ya misamaha ya kodi na
wahusika wake muda wa miaka mitano. Pia, ameagiza kupatiwa orodha ya
walipa kodi wakubwa na jinsi wanavyolipa.
“Pia, nimewataka wanipe orodha jinsi zilivyolipa
kodi kampuni kubwa zinazobadili majina kila baada ya muda fulani,
hususan za simu ili kujua wanavyolipa kodi,” alisisitiza.
Naibu waziri alisisitiza kwamba Sera ya Kodi
imesababisha kuanzishwa kwa sheria ya ununuzi ambayo nia yake ilikuwa
nzuri, lakini sasa imekuwa kichaka cha wizi wa kistaarabu na
itarekebishwa.
Kuhusu umuhimu wa mashine ya elektroniki, alisema
yeye ni muumini wa mashine hizo kwamba ipo haja kwa wafanyabiashara wote
kuielewa vizuri ili waweze kuona faida zake na kwamba, itawaondolea
usumbufu.
Wakurugenzi wa halmashauri waonywa
Awali juzi asubuhi, Mwiguli alizungumza na
wakurugenzi wa halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya kwenye Ukumbi wa Mkapa
ambapo aliwataka kuacha mara moja mambo ya ufisadi na kuwataka kusimamia
kwa akili fedha hizo ili kukwepa jela.
Mwananchi
Mwananchi
No comments:
Post a Comment