Rais Jakaya Kikwete ametangaza kuwa Bunge Maalumu la Katiba
litaanza Februari 18 mwaka huu huku akiwataka viongozi wa vyama vya
siasa nchini kuweka mbele masilahi ya Taifa na siyo ya vyama vyao.
Rais Kikwete alisema wajumbe 640 wa Bunge hilo
wengi ni wafuasi wa vyama vya siasa, hivyo wanatakiwa kukubaliana kwa
hoja badala ya kila upande kuvutia kwake.
Aliwaonya pia wanasiasa kutokazania suala la
muundo wa Muungano peke yake, bali waangalie na masuala mengine yaliyomo
kwenye rasimu hiyo ambayo ni muhimu kwa Taifa.
Bunge la Katiba linafanyika baada ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kukamilisha kazi yake ya miezi 20 kukusanya maoni
ya wananchi na kuandaa Rasimu ya pili Katiba ambayo ilitolewa Desemba
30, mwaka jana.
Akizungumza na viongozi mbalimbali wa vyama hivyo
jana katika mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, Rais Kikwete
alisema kama wanasiasa wakikubaliana, hakuna mwananchi yeyote
atakayepinga uamuzi utakaopitishwa na Bunge hilo.
“Nimeshauriana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali
Mohammed Shein kuwa Bunge Maalumu la Katiba lianze vikao Februari 18,
mwaka huu. Bunge hili litafanyika kwa siku 70 na kama mambo yatakuwa
hayajamalizika zinaweza kuongezwa siku 20,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza: “Nyinyi ndiyo wenye jukumu la kuipatia
nchi yetu katiba nzuri inayojali masilahi ya watu wake ndani ya pande
zote za Muungano, kuanzia watu wanapoishi, wanapotoka na asili yao.
Msije mkafanya uamuzi utakaowaingiza katika uadui na chuki.”
Katika hotuba yake ya dakika 70, Rais Kikwete
alisema yapo mambo mengi ya kujadili katika Bunge hilo, siyo muundo wa
Muungano pekee.
“Mnakwenda kuijadili Katiba kuhusu masuala
mbalimbali yenye masilahi ya nchi yetu, siyo mambo ya Muungano tu.
Wekeni utaratibu ili muweze kukubaliana hata katika masuala ambayo kila
mmoja ana msimamo wake,” na kuongeza:
“Kuna suala la ukomo wa kugombea ubunge kuwa
vipindi vitatu. Hii maana yake ni kuwa kama umeshakuwa mbunge kwa
vipindi vitatu huwezi kugombea hata urais,” alisema na kuongeza;
Kwa mujibu wa Rasimu ya Kwanza ya Katiba, Ibara ya
75 (e) mgombea urais alitakiwa kuwa na sifa za kugombea ubunge, ikiwamo
ya kutowahi kuwa mbunge kwa vipindi vitatu. Hata hivyo kwenye Rasimu ya
Pili itakayojadiliwa na Bunge hilo, ibara ya 79 inayozungumzia sifa za
kuwania urais, hailazimishi mgombea urais kuwa na sifa za kuwania
ubunge.
Rais Kikwete alisema wanasiasa wana dhamana ya
kuwapatia Watanzania Katiba itakayodumu kwa miaka 50 ijayo na kuimarisha
Muungano, umoja, amani na utulivu, siasa safi na kuongeza kasi ya
maendeleo na ustawi wa wananchi.
Mwanachi
Mwanachi
No comments:
Post a Comment