Serikali imeanzisha mfumo mpya wa udahili kwa wanafunzi
wanaoingia kidato cha kwanza, kwa kuwalipia ada watakaojiunga na shule
binafsi.
Vilevile, imeanzisha utaratibu utakaoshirikisha
shule binafsi na zinazoendeshwa na Serikali katika kuteua wanafunzi
watakaojiunga na sekondari.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni
Mchome, alisema kuwa utaratibu huo unatarajiwa kuanza kutumika pia kwa
wanafunzi wanaotarajiwa kuingia kidato cha tano mwaka huu.
Alisema kuwa mfumo huo utasaidia kuwezesha
wahitimu wengi, waliofanya vizuri kupata nafasi za kuendelea na masomo
huku pia shule nyingi zikiwa na uhakika wa kupokea wanafunzi.
“Tunajua kumekuwa na tatizo la shule nyingi kukosa
wanafunzi zikiwamo za Serikali kwa kuwa wapo wanafunzi ambao
huchaguliwa kujiunga na shule za Serikali, lakini wazazi wao huwapeleka
kwenye shule binafsi,” alisema Profesa Mchome na kuongeza;
“Vilevile, kuna watoto ambao hushindwa kuendelea
na masomo ya sekondari licha ya kufanya vyema kama ilivyotokea kwa mwaka
huu kutokana na uchache wa madarasa.”
Profesa Mchome alitoa mfano wa kujitokeza kwa
tatizo hilo mwaka jana akisema kuwa idadi kubwa ya wanafunzi waliomaliza
darasa la saba na kupata matokeo mazuri, walikosa shule, hivyo
kulazimika kusubiri uteuzi wa pili, wakati wenzao tayari wameshaanza
masomo.
“Lakini chini ya utaratibu huo wa udahili wa
pamoja, Serikali imekusudia kuweka utaratibu maalumu utakaowawezesha
baadhi ya wanafunzi kuendelea na masomo kwenye sekondari binafsi kwa
utaratibu maalumu wa malipo,” alisema Profesa Mchome.
Aliwatoa wasiwasi watu walio na tabia ya kubeza
shule za Serikali zinazolalamikiwa kuwa na matokeo mabaya kwenye
mitihani mbalimbali ya taifa, akisema kuwa hata shule binafsi zimekuwa
zikishika nafasi ya mwisho.
“Hadi sasa elimu inayotolewa nchini kwa ubia na
sekta binafsi bado haijafikia kwenye kiwango cha ubora, kwani hata kwa
shule binafsi zipo zinazofanya vibaya, ikilinganishwa na za Serikali,”
alisema.
Profesa Mchome aliongeza: “Zipo shule za sekondari za Serikali zinazofanya vizuri kama vile Kilakala na Ilboru.”
Alibainisha kuwa Serikali imekusudia kuziimarisha
shule zake kongwe nchini ili ziwe na majengo bora, maabara zenye vifaa
na walimu wa kutosha.
Alifafanua kwamba mpango wa kuboresha shule hizo unatarajiwa kuanza mwaka huu wa fedha na kwamba utarejesha heshima ya kitaifa na kurudisha dhana ya kuanzishwa kwa shule hizo.
”Vitakuwa ni vituo bora ingawa hii haipo kwenye
mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, lakini ni mpango wetu wa pili. Pia
tunatarajia tutashuka katika ngazi ya mkoa kwa kujenga shule nzuri
katika kila mkoa ambao hauna shule kongwe,” alisema Profesa Mchome.
Alieleza kuwa wanatarajia kushuka hadi ngazi ya
wilaya baada ya kuziimarisha sekondari za mkoa na kwamba hatua hiyo ipo
katika mpango endelevu wa Serikali.
Mchome alisema kwamba awali, Serikali ilikusudia
kuanza kuutumia utaratibu huo kwa wanafunzi waliomaliza darasa la saba
mwaka jana, lakini ilishindikana kutokana na wamiliki wa shule binafsi
kutaka muda zaidi wa kuelimishwa.
Akizungumzia utaratibu huo Mwenyekiti wa Chama cha
Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongsco), Mahmoud Mringo alisema
kuwa Serikali imeshawasilisha dhamira hiyo, lakini haijaweka wazi
utekelezaji wake.
Alisema kuwa utaratibu huo hautakuwa na matatizo
endapo kutakuwapo usawa na wanafunzi kupewa fursa ya kuchagua shule kama
ilivyo kwa vyuo vikuu .
“Mpango siyo mbaya ila tunachotaka ni ushirika wa
sawa kwa sawa. Shule ziwekwe kwa pamoja na mwanafunzi apewe nafasi ya
kuchagua kama inavyofanyika katika vyuo vikuu na siyo kuwachukua
wanafunzi waliokosa nafasi serikalini,” alisema Mringo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu
Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch alisema kuwa mpango huo hauwezi kuwa na
manufaa katika elimu kutokana na kutaka kuwanufaisha watendaji wa Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi aliodai wengi wao ndiyo wamiliki wa shule
binafsi.
Alidai kwamba kutaka fedha katika shule zao ndiyo
sababu ya watendaji na wanaofanya uamuzi katika sekta ya elimu kuleta
mpango huo ambao alisema kuwa mwisho wa siku utaibua mgogoro mkubwa.
“Mfumo kama huu ulijaribiwa katika nchi za Amerika
Kusini, lakini ulishindikana kwa sababu ni mfumo mbovu, unachangia
kuibua migogoro kwenye jamii. Tatizo ni kwamba, watoa uamuzi katika
sekta hii ndiyo wamiliki wa shule binafsi,” alisema Oluoch akidai na
kuongeza;
“Upande wa CWT hatujashirikishwa katika hili na
sisi tunalisikia, lakini mpaka sasa tunaona haufai kabisa kwa maendeleo
ya elimu nchini.”
No comments:
Post a Comment