Monday, 24 February 2014

Inasikitisha: Ana kipaji, ni maarufu, shida lukuki

KATIKA michezo na sanaa, mchezaji ama msanii ana mwongozo wa mwelekeo wake wa baadaye, ingawa anaweza kuanza kwa kusuasua na baadaye kung’ara ama baadaye nyota yake kufifia na kupotea kwenye fani.
Hadhara Charles (24) ni mmoja wa wanawake wenye vipaji katika michezo, hashindani kama walivyo wanamichezo wengine bali ni mtaalamu wa kumiliki na kuchezea mpira kadri anavyotaka kwa kupiga danadana kwa miguu, kichwa au kuumiliki kwa kutumia mgongo au mabega yake.
Ni mambo ambayo yamempa umaarufu kiasi kwamba hakuna shabiki wa soka nchini anayehudhuria mechi kubwa za kimataifa na zile za Ligi Kuu Bara kwenye viwanja mbalimbali ukiwamo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambaye hamjui mwanadada huyu mwenye kipaji cha kuchezea mpira.
Utundu wa kuchezea mpira, umempa fursa za kufanya maonyesho katika mechi mbalimbali za Ligi Kuu na hata mechi za kimataifa na kutembelea nchi mbalimbali zikiwemo Gabon, Cameroon, Ethiopia, Malawi na Afrika ya Kusini.
Kwa mashabiki wengi, Hadhara huwa burudani ya kipekee kwao hasa wakati wa mapumziko inapochezwa mechi kubwa, hapo atawaonyesha mbwembwe zake za kuchezea mpira kwa staili mbalimbali. Hadhara amezungumza na Mwanaspoti mambo mbalimbali kuhusu utundu wake huo, ikiwemo alikotoka, mafanikio, changamoto anazokutana nazo pamoja na malengo yake ya baadaye.
Alikotoka
“Nimeanza tangu nikiwa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Bwilingu, Chalinze, Pwania, nilikuwa napenda sana kucheza soka hasa kupigapiga danadana mpaka nilipohitimu darasa la saba mwaka 2004,’’ anasema Hadhara.
Anafafanua kuwa hakuweza kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na uwezo mdogo wa kifedha na badala yake alitumia muda wake mwingi kucheza soka mtaani zaidi akionyesha ufundi wa kuumiliki na kuuchezea mpira jambo ambalo lilikuwa burudani kwa wengi.
 “Niliacha kufanya maonyesho mitaani baada ya kugombana na wanawake wenzangu kwani walidai kuwa nawadhalilisha kutokana na kuonekana kama mwanamke mchafu na asiyejithamini,” anasema Hadhara.
Mafanikio
“Nimefanya ziara katika nchi mbalimbali, ziara yangu ya mwisho ilikuwa mwaka juzi nilipokwenda Afrika Kusini kwenye fainali za michuano ya Mataifa ya Afrika kati ya Nigeria na Burkina Faso. Lakini mbali na huko pia nimeenda Gabon, Cameroon, Ethiopia, Malawi na Kenya.
“Huko nilikuwa nafanya kwenye mashindano mbalimbali ya soka au yale yaliyokuwa yanaandaliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali ‘NGO’s’ la Oxfam ambao walikuwa kama wadhamini wangu, hawa huwa wanaandaa mashindano yao yanayojulikana kwa jina la ‘Play for the union’. “Taasisi hiyo sikuingia nayo mkataba wa maandishi bali tulikuwa tunakubaliana tu kulipana kiasi fulani, fedha waliyokuwa wananipa ilikuwa ndogo sana, nakumbuka mara ya mwisho safari ya Afrika Kusini nililipwa Sh 400,000 kabla ya hapo walikuwa wananilipa Sh 200,000,” anasema.

Anasema ni vigumu kwake kumudu maisha kwa fedha hizo kwani tayari ana watoto wawili wanaomtegemea ambao ni Hamoud  (6) na Fey (4) na zaidi ya hilo haishi pamoja na mzazi mwenzake ambaye alidai ameoa mke mwingine.
“Maisha ni magumu sana kwangu, watu wananiona nina fedha nyingi kupitia kipaji changu lakini siyo kweli naishi kwa shida, familia yangu inanitegemea mimi, kuanzia mama mpaka watoto.
“Mimi nimeishia darasa la saba na nina uhakika wanangu pia hawatasoma kwani uwezo wa kuwasomesha sina na hakuna mtu anayenisaidia, sijapata mafanikio yoyote kupitia fani yangu, nikienda Uwanja wa Taifa huwa nalipwa Sh 50,000 ambazo kwa matatizo niliyonayo na kazi ninayofanya haviendani,” anasema.
Kucheza soka
“Kwanza Chalinze hakuna timu ya soka ya wanawake, lakini hata ingekuwepo nisingeweza kucheza kwani sina pumzi ya kucheza dakika 90, huwa naishia dakika 45 halafu nina mshono ambao nilifanyiwa upasuaji wa tezi ubavuni,” anasema Hadhira.
Changamoto
“Napata changamoto nyingi ambazo watu hawazijui, nakumbuka tukio moja ambalo siwezi kulisahau katika maisha yangu, mapema mwaka huu kuna watu walinichukuwa kwenda kufanya onyesho Kenya, ni watu wanaojihusisha na mambo ya tiba mbadala.
“Kabla ya kufika huko, kuna sehemu waliweka kama kituo nikafanya onyesho langu lakini wakati naendelea kuonyesha kumbe wao wametafuta njia ya kunitoroka mpaka namaliza walikuwa wameondoka muda mrefu.
“Sikuwa na fedha yoyote ambayo ingeniwezesha kunirudisha nyumbani kwani mara nyigi huwa naahidiwa kulipwa baada ya onyesho, nilisikitika sana ingawa wasamaria wema waliokuwepo eneo hilo walinichangia zaidi ya Sh 100,000 nikarudi nyumbani,” anasema.
Anasema hata anapokuja Dar es Salaam kufanya maonyesho Uwanja wa Taifa huwa anapanda magari makubwa ‘Maroli’ kwa kuomba msaada kwa madereva wa magari hayo, hiyo ni kutokana na kukosa nauli na wakati mwingine kupunguza gharama za matumizi.
Mama yake akasirika.
“Mama yangu alikasirika sana na kuamua kuninyang’anya pasi ya kusafiri na kunipiga marufuku kufanya maonyesho sehemu yoyote kwani hakuna faida ninayoipata, ila naipenda fani yangu na ninatamani kuiba pasi hiyo ili nifanye mambo yangu kwani naona yanazidi kuwa magumu,” anasema Hadhara.

Hadhara anaomba msaada kwa mtu yeyote ambaye ataweza kumsaidia katika kuendeleza kipaji chake:  “Nakipenda kipaji changu ila nahisi kinakufa, naomba mtu anayeweza kuniendeleza anisaidie au ikishindikana nisaidiwe hata mtaji nifanye biashara ili niachane na kazi hii na niweze kuilea familia yangu, naumia sana.”
Rais Jakaya Kikwete
Hadhara anasema kuwa alifunga safari mpaka nyumbani kwa Rais Jakaya Kikwete kijiji cha Msoga wilaya ya Bagamoyo kuomba msaada wa kuendelezwa kipaji chake ambapo alipewa ahadi ya kusaidiwa. “Nafikiri Rais Kikwete ana mambo mengi, nakumbuka mwaka jana nilienda kwao, nilitoa maelezo na kuacha namba yangu ya simu, Rais alinipigia baada ya wiki moja na kuniambia kuwa amepata taarifa zangu na kuniahidi kunisaidia.
“Lakini tangu tuzungumze ni mwaka sasa umepita sijapata taarifa mpya, siwezi kumlaumu kwani ana mambo mengi, naamini ipo siku atakumbuka na kunisaidia naipenda fani yangu na sipendi ife,” anasema.

Mwanaspoti

No comments:

Post a Comment