Waziri wa Serikali za Mitaa nchini Uganda, Alex Onzima ametishia
kujiuzulu wadhifa wake iwapo Rais Yoweri Museveni hatakubali kutia
saini muswada unaohusu wapenzi wa jinsia moja.
Muswada huo uliopitishwa na Bunge la nchi hiyo
mwishoni mwa mwaka jana unatoa adhabu kali kwa wale watakaobainika
kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja, suala ambalo limekuwa likipingwa
na baadhi ya mataifa ya Ulaya ambayo yamekuwa yakitishia kusitisa utoaji
wa misaada ya kumaendeleo iwapo utatiwa saini.
Akizungumza na wanahabari kwenye hafla ya
kusimikwa kwa mkuu wa Diakonia ya Maracha katika kijiji cha Nyoro,
Onzima alisema hana namna kwa kuwa hajapata nafasi ya kumweleza lolote
Rais Museveni kuhusu muswada huo.
“Museveni anatakiwa aangalie kwa kina mambo muhimu
kwenye muswada huo. Yeyote aliyeko hapa ambaye anaripoti kwake aende na
amweleze kwamba sikubaliani hata kwa nukta moja katika suala hili hata
kama itakuwa ni kwa gharama ya kupoteza nafasi yangu ya uwaziri, nina
makazi yangu hapa Maracha,” alisema.
Hii ni mara ya kwanza kwa mtumishi wa juu wa
Serikali kuzungumza hadharani kupinga hatua ya Rais Museveni kuchelewa
kupitishwa muswada huo uliopitishwa Desemba 23 mwaka jana kuwa sheria.
Waziri huyo alimsifu Rais wa Senegal, Macky Sall kwa hatua yake ya
kumweleza Rais Barack Obama wa Marekani wakati wa ziara yake nchini humo
mwaka jana kwamba suala la wapenzi wa jinzia moja halina nafasi kwa
Afrika.
“Hebu fikiria iwapo Rais Obama angeotembelea
Uganda na kumuuliza Museveni kuhusu suala la wapenzi wa jinsia moja,
hivi nini kingetokea?” alihoji.
Waziri huyo amekuwa ni mmoja wa mawaziri ambao
wamekuwa wakipinga hatua ya Serikali kuchelewa kutoa uamuzi katika
masuala mengi, ambapo wakati fulani aliamua kujitoa kwenye chama tawala
cha National Resistance Movement (NRM) na kujiunga na Reform Agenda
mwaka 2001.
Baada ya kushiriki huko na kwua mpinzani wa
Serikali kwa muda, alirejea na kujiunga na NRM mwaka 2011 ambapo baadaye
aliteuliwa na rais museveni kuwa miongoni mwa mawaziri katika baraza
lake.
No comments:
Post a Comment