MWAKA mpya 2014 ulianza kwa matumaini makubwa
miongoni mwa wadau wa soka kwamba maendeleo yamefikiwa, ambapo
ilitarajiwa Tanzania ianze kutumia tiketi za elektroniki.
Tiketi hizo zilianza kutumika lakini yalikuwa majanga, teknolojia ikakataa au wadau wakashindwa kuiweka inavyotakiwa.
Sintofahamu hiyo imeturudisha kule kule kwenye tiketi za vishina, ambapo kuna wanaofaidi kwa kukaa milangoni.
Nimeambiwa kuna jamaa wana vishina vya mechi
zilizopita baina ya Yanga na Al Ahly na kwamba si ajabu hata mechi ijayo
watavitumia au kurekebisha kidogo tu.
Soka imekuwa sehemu ya kwenda kula na si sehemu ya
kwenda kutumia uzalendo, elimu, ujuzi na maarifa kuhakikisha sekta hii
nayo inakua kiteknolojia na kulifaidisha taifa kiuchumi.
Tiketi za elektroniki ni hatua moja ndogo tu ya
kuendea usasa zaidi, kwa sababu wenzetu huku wanabofya kwenye mtandao wa
kompyuta, kulipia na kupata tiketi. Tutaona baadaye mifumo yao, manufaa
na mapungufu kama yapo.
Kwetu Tanga yalikuwa maafa zaidi maana milango ya
elektroniki haikuwafungulia washabiki waliofika Mkwakwani na inaelezwa
zaidi ya nusu ya washabiki waliingia bure.
Wapo watu hata ndani ya mfumo wa uongozi wa soka
katika klabu, mikoa na ngazi ya taifa wanapendelea mfumo wa kuchana
tiketi pale mlangoni.
Ndiyo maana nachelea kusema kwamba mfuko wa elektroniki umekwama bali labda itakuwa sahihi zaidi kusema umekwamishwa.
Zipo tetesi pia kwamba Wachina walipokuwa
wakijenga Uwanja wa Taifa ambao ni wa kisasa zaidi Afrika Mashariki
walitoa wazo la kuweka mfumo huo moja kwa moja lakini ‘wadau wa
maendeleo’ wakakataa. Kisa? Wanajua wao.
Kwa hali ilivyokuwa mbaya, wakati Ligi Kuu
Tanzania inaanza kuhusiana na suala la tiketi, Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) halikuwa na la kufanya zaidi ya kuzuia matumizi ya tiketi
hizo. Niseme tu kwamba kuna watu waliopinga tangu awali tiketi hizo na
wataendelea kupinga nyingine zozote zenye mfumo wa kuziba mianya ya
wizi.
Wenzetu hapa Uingereza na mataifa mengine
yaliyoendelea kisoka, ambayo hatuna budi kuyaiga katika mazuri yao,
wanaoruhusiwa kuuza tiketi za mechi hapa ni klabu husika tu au mawakala
wao waliopo kisheria na si kuchagua sijui vibanda vya soda au mikate
Mwenge, Tandika au Ilala Bungoni.
Ni kosa kubwa kujihusisha na uuzaji wa tiketi ovyo, lakini kama
ambavyo kuna wachumia tumbo hapo nyumbani, wapo hapa wanaojaribu kuzi
upload tiketi kwenye tovuti mbalimbali na baadhi hudiriki kwenda karibu
na viwanja na kuziuza kwa bei ya juu.
Bodi ya Ligi Kuu (Premier League) hapa England
wamekuwa wakali sana wakishirikiana na mamlaka za dola kupambana kwa
mafanikio makubwa na wauzaji feki wanaotundika tiketi kwenye tovuti na
kuziuza na pia watu kadhaa wamedakwa na kushitakiwa kwa kuzilangua
viwanjani.
Hili, pengine sawa na linaloweza kuwa limetokea au
litatokea nyumbani, linakwenda sambamba na uuzaji wa tiketi za
kughushi, ndiyo maana kama kuna kitu kinasisitizwa sana kwenye nchi hizi
ni kununua tiketi (na bidhaa nyingine zozote) kwa mhusika halali na
kupata stakabadhi.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaposisitiza
ukinunua dai stakabadhi na ukiuza toa stakabadhi, ni jambo ambalo huku
ni la lazima, hata kama hutaki utajikuta umechanganyiwa stakabadhi ama
na bidhaa zako au na chenji.
Klabu mwenyeji huuza tiketi zake lakini huwawekea
wageni idadi wanayokubaliana na hutolewa mapema, iwe ni mechi ya Ligi
Kuu au ya kimataifa na wala hutaona mkanganyiko.
Tiketi zikisemwa zimeisha basi shabiki ambaye
angetaka kwenda uwanjani anashauriwa abaki nyumbani, atazame kwenye
televisheni na kuwahi kutazama mtandaoni ratiba ya mechi inayofuata
anunue mapema tiketi yake awe nayo kibindoni.
Malalamiko ambayo yamepata kuwapo ni tiketi za
baadhi ya mechi kuwa ghali sana, mojawapo ya klabu zenye aina hiyo ni
Arsenal lakini watu wanaoingia Emirates ni karibu 60,000.
Bodi ya EPL kwa mfano, imekuwa ikisambaza
matangazo kwa njia mbalimbali kuwaasa washabiki walio ng’ambo ambao
wangependa kuingia England kutazama mechi za EPL kuwasiliana kwanza na
klabu husika kwenye tovuti zao.
Ni tofauti kabisa na jamaa wa Mbeya City
wanaopanda Coaster zao na kutinga Dar kwa ajili ya mechi dhidi ya Simba
siku hiyo hiyo ya mechi pasipo kuwa na tiketi mkononi, maana watazipata
tu uwanjani na wanasema uwanja haujai, kwani eti si sawa na ndoo ya
maji.
Premier League pia inatoa angalizo kwa washabiki
hao, hasa wa ng’ambo kupendelea zaidi kununua tiketi kutoka kwa klabu
husika ili kujiridhisha kwamba ni halali.
Ununuzi wote huo ni kwa mtandao, ambao rafiki zangu wa Tanzania watakuwa hawaupendi.
Tiketi za mechi za EPL zina soko sana kutokana na
washabiki wengi kupenda kwenda wenyewe uwanjani kujionea mechi na
wachezaji wawapendao, hata kwa kusafiri umbali mrefu.
I.G.Saria,
M: +44 (0) 7791284317
E: saria@tanzaniasports.com
No comments:
Post a Comment