Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ameingilia kati vita ya
kuwania urais mwaka 2015 kwa kukemea kwa baadhi ya makada wa chama hicho
kuanza kampeni mapema.
Kadhalika, ameziagiza Kamati za Maadili na Usalama
za chama hicho kuwachukulia hatua stahiki viongozi na wanachama wake
wanaomwaga fedha ili kupata uongozi.
Rais Kikwete alizungumzia masuala hayo kwa nyakati
mbili tofauti; juzi wakati alipokutana na Halmashauri ya CCM ya Mkoa wa
Mbeya na jana kwenye kilele cha sherehe za maadhimisho ya miaka 37 ya
kuzaliwa chama hicho.
Kauli yake imekuja wakati kukiwa na vita ya maneno
baina ya makada wa chama hicho, kutokana na kauli iliyotolewa na Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye alitangaza kuanza rasmi kwa
safari aliyoiita ya matumaini ya ndoto zake, ambayo amesema itatimiza
ndoto za Watanzania kupata elimu bure, majisafi na maendeleo ya uhakika.
Lowassa alitoa kauli hiyo wakati wa hafla ya mwaka
mpya aliyowaandalia marafiki na jamaa zake, Januari Mosi, mwaka huu
huko Monduli mkoani Arusha.
Tamko hilo lilileta hisia kuwa ametangaza nia ya
kugombea urais mwaka 2015 kupitia CCM na kusababisha malumbano baina ya
wazee, vijana, viongozi na makada wa chama hicho wakimtuhumu kuwa
anakivuruga chama kwa kutangaza nia hiyo kabla ya muda wa kampeni
kuanza.
Akizungumza wajumbe wa Halmashauri ya CCM ya Mkoa
wa Mbeya kwenye Ukumbi wa CCM, Mbeya, Rais Kikwete alisema kuanza kwa
kampeni kabla ya wakati wake ni moja ya mambo yanayosikitisha.
“Hili ni moja ya mambo yanayosikitisha. Lakini
suala zima tumelikabidhi kwa Mzee Mangula (Phillip - Makamu Mwenyekiti
wa CCM Bara), ambaye atalisimamia na kulishughulikia,” alisema.
Rais Kikwete alikuwa akijibu swali na Mwenyekiti
wa CCM wa Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi ambaye alimtaka kufafanua kama
kampeni zimeanza ndani ya CCM au bado.
Kumwaga fedha
Akihutubia katika mkutano wa hadhara kwenye Uwanja
wa Sokoine, Mbeya jana, Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM,
alisema kutoa fedha kunaharibu taswira ya chama hicho na kukiweka katika
hatari ya kupoteza ushindi katika chaguzi zinazokuja.
“Agizo la CCM la miaka mingi iliyopita ni kwamba
kila ngazi kuwa na shughuli za kuwaingizia mapato sambamba na kuwa na
mfuko wa uchaguzi. Agizo hili bado halijatekelezwa na ndiyo linakiathiri
chama,” alisema Rais Kikwete.
Mwananchi
Mwananchi
No comments:
Post a Comment