UMEWAHI kuona rubani anaiteka ndege yake? Bila shaka unakumbuka
kisa cha rubani msaidizi, Hailemedhin Abera (31) aliyeiteka ndege ya
Ethiopian Airlines Jumatatu ya wiki iliyopita kwa madai ya kuwa na
msongo wa mawazo kwa kufiwa na mjomba wake.
Abera, ambaye amefanya kazi kwenye shirika hilo
maarufu la ndege kwa miaka mitano alijifungia kwenye chumba cha marubani
baada ya rubani mkuu kwenda msalani.
Rubani huyo msaidizi ‘aliendesha’ ndege hiyo kwa
saa sita na badala ya kuipeleka Roma, Italia aliipeleka Geneva, Uswisi
ambako alitua baada ya kuomba kupewa hifadhi nchini humo.
Rubani huyo alifanya kituko kwa kuwatisha abiria
kwa kuchomoa vikasha vya hewa ya oksijeni kwenye ndege hiyo na kutishia
kuzima mfumo wa hewa iwapo abiria hao wasingekubali kufuata maelekezo
yake.
Rubani huyo akawaambia abiria kwa ukali: “Kaeni
chini, vaeni vikasha vya oksijeni kwenye viti vyenu, nitakwenda kukata
mfumo wa hewa ya Oksijeni.”
Baada ya rubani huyo kuwazungusha abiria kwa saa
sita angani wakiwa hawajui hatima yao, alitua Geneva na kushuka kupitia
dirishani kwa msaada wa kamba huku akiomba hifadhi kabla ya
kujisalimisha kwa polisi.
Ndege hiyo aina ya Boeing 767-300 iliyokuwa na
abiria 201 na wahudumu iliondoka mjini Addis Ababa na kutua mjini
Geneva, ikiwa imebakiza mafuta yanayayoiwezesha kuendelea kuwepo hewani
kwa dakika 20 tu.
Si ndege tu ambayo inaweza kutekwa, hata viongozi
wa Simba wamewateka nyara wanachama wao kwa kuitisha mkutano mkuu Machi
16 ambao utajadili ajenda moja tu ya mabadiliko ya katiba.
Itakuwaje Simba yenye migogoro mingi iwe na ajenda
moja tu ya kujadili mabadiliko ya katiba wakati wanachama wanataka
kujua suala la uwanja wao wa Bunju B.
Itakuwaje ijadiliwe ajenda moja tu katika mkutano
huo wakati wapo baadhi ya wanachama katika Simba ambao wanataka kujua
Emmanuel Okwi aliuzwa vipi kwenda Etoile du Sahel ya Tunisia bila
malipo yoyote.
Wanachama wanataka kupata majibu inakuwaje Okwi licha ya ubora wake auzwe kwa mkopo na fedha haijalipwa mpaka sasa?
Wanachama wanataka kujua inakuwaje mchezaji wao
kiraka Shomari Kapombe apelekwe AS Cannes ya Ufaransa kwa mkataba ambao
hauna maelezo ya kujitosheleza.
Kapombe, miongoni mwa wachezaji bora Afrika Mashariki na Kati sasa yupo nchini akiwa hajui hatima yake, lakini Simba wapo kama vile hawana shida naye.
Kapombe, miongoni mwa wachezaji bora Afrika Mashariki na Kati sasa yupo nchini akiwa hajui hatima yake, lakini Simba wapo kama vile hawana shida naye.
Simba imecheza mechi nne na kupata pointi mbili
tu, kuna tatizo gani hapo. Wanachama wanataka kupata majibu sahihi kuna
tatizo gani katika timu hiyo?
Matatizo yote hayo yanapaswa kujadiliwa katika
mkutano mkuu wa wanachama wa Simba na hasa ikizingatiwa kuwa kuna
mgawanyiko mkubwa ndani ya uongozi na Kamati ya Utendaji.
Kwa misimu miwili mfululizo, Simba inashindwa
kushiriki mashindano ya Shiriisho la Soka Afrika (CAF) iwe Ligi ya
Mabingwa au Kombe la Shirikisho. Wanachama wanataka kujadili hayo.
Inawezekana Simba inataka kufika mahali fulani
kuzuri, lakini viongozi wake wamewateka wanachama na wanawapeleka sehemu
nyingine huku wakiomba hifadhi maalumu.
Yule rubani wa Ethiopia aliiteka ndege kwa madai
alikuwa na msongo wa mawazo baada ya kufiwa na mjomba wake, sielewi
viongozi wa Simba wamepata msongo wa mawazo baada ya kufiwa na mjomba
yupi?
Mwanaspoti
Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment