Tangu
mwaka jana juhudi za chini chini zilianza kufanywa na baadhi ya
Watanzania ambao hawajaridhika kuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere, alifariki kifo cha kawaida.
Baadhi
ya wafuasi wa Mwalimu Nyerere, wamekuwa wagumu kuamini kama kweli
Mwalimu alikufa kifo cha kawaida, kutokana na ukweli kwamba maradhi
yaliyomuua - saratani ya damu (leukemia) - hayana desturi ya kuua kwa
kasi kama ilivyotokea kwake.
Samuel Kasori, aliyekuwa Katibu Myeka wa Mwalimu, amezungumza na JAMHURI na
kusema; “Mwalimu anakuwa kwenye rekodi ya kufa haraka sana kwa ugonjwa
wa saratani ya damu. Ugonjwa huo huua taratibu, lakini kwa Mwalimu
ilikuwa tofauti kabisa. Kuna nini kilichotokea? Sitaki kuhoji sana,
lakini naamini kuna siku Watanzania na walimwengu wataujua ukweli.”
Maneno
ya Kasori yanaendana na ya Mwalimu James Irenge (Mwalimu wa Baba wa
Taifa), aliyoyatoa mwanzoni mwa mwaka jana baada ya mvutano wa kisiasa
kati ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa, na Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent
Nyerere (Chadema).
Baada
ya kauli ya Mbunge Nyerere kumtaka Mzee Mkapa aeleze chanzo cha kifo
cha Mwalimu, Mwalimu Irenge alijitokeza na kusema amefurahishwa mno
kusikia kuwa amepatikana kiongozi jasiri wa kuhoji namna Mwalimu
alivyougua hadi kufariki dunia.
“Mfikishieni
pongezi nyingi Mbunge Nyerere... huyo mtoto amefanya jambo la maana
sana kuuliza jambo hili, miaka yote nalia kwa sababu naamini Mwalimu
aliuawa.
“Kwa
kuwa suala hili limeulizwa hadharani, sasa nipo radhi kufa. Nikifa
nitakwenda moyo wangu ukiwa na furaha kwa sababu nimekuwa nikijiuliza ni
nani anayeweza kuhoji namna Mwalimu… mwanafunzi wangu alivyokufa,”
alisema Mwalimu Irenge.
Kauli
hiyo ya Mwalimu Irenge ya Machi, mwaka jana haikupita bure, kwani
Julai, mwaka huo, aliaga dunia mjini Musoma na kuzikwa kijijini kwake
Busegwe Nyanza wilayani Butiama.
Mwalimu
Irenge alianza kumfundisha Mwalimu Nyerere katika Shule ya Mwisenge
kuanzia mwaka 1934 hadi 1936. Mwalimu Irenge aliwahi kuhojiwa na Shirika
la Utangazaji la Uingereza (BBC) na kusema, binafsi hakuafiki Mwalimu
kupelekwa kutibiwa nchini Uingereza.
Alisema
alipinga kwa sababu alijua Waingereza si marafiki wa kweli wa Mwalimu,
kwa kuwa aliongoza harakati za kuwang’oa katika Tanganyika na katika
mataifa mengine, hasa Afrika Kusini na Zimbabwe, ambako Serikali ya nchi
hiyo ilikuwa ikiunga mkono utawala wa kidhalimu wa Wazungu wachache.
Mwakyusa na kifo cha Mwalimu
Profesa
David Mwakyusa alikuwa daktari wa Baba wa Taifa tangu mwaka 1987 hadi
Oktoba 14, 1999, siku Mwalimu alipofikwa na mauti jijini London,
Uingereza, kutokana na ugonjwa wa saratani ya damu (leukemia).
Katika
mahojiano aliyopata kufanya muda mfupi baada ya kifo cha Mwalimu,
Profesa Mwakyusa alisema walimjulisha Mwalimu kila kitu kuhusu ugomjwa
wa leukemia. Hata hivyo, kwenye maelezo yake anathibitisha namna ugonjwa
huo ulivyobadilika ghafla na kumsababishia mauti, ilhali kila
alipopimwa ilionekana hakuwa na sababu za kuanza matibabu mapema.
Swali:
Mwalimu alikuwa anajulikana kwa Watanzania kama mtu mwenye afya nzuri.
Wewe kama daktari wake unasemaje kuhusu afya ya Mwalimu kwa ujumla.
ibu:
Mwalimu alikuwa mtu mwenye afya nzuri kwa ujumla, ukiacha matatizo
madogo madogo ninayoweza kuyaita ya kawaida. Alikuwa na desturi ya
kufanya mazoezi na alikuwa mtu anayefuata masharti na ushauri aliokuwa
akipewa na madaktari.
Daktari
wa kwanza aliyekuwa anamhudumia Mwalimu baada ya Uhuru alikuwa Profesa
Mhonoli. Kuanzia mwaka 1979 alihudumiwa na Profesa Makene akisaidiwa na
Profesa Mtulia na mimi. Mwalimu alipostaafu mwaka 1985 alibakia daktari
mmoja tu, Profesa Makene. Makene alistaafu mwishoni mwa mwaka 1987 na
tangu wakatu huo mimi ndiye niliyekuwa daktari wake hadi alipoaga dunia
tarehe 14 Oktoba 1999.
Swali:
Baada ya kulazwa katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas jijini London,
ndipo Watanzania tulipotangaziwa kwamba Mwalimu aligundulika kuwa na
ugonjwa wa kansa ya damu mwishoni mwa mwaka 1998. Je, ugonjwa huu
unafikiri aliupataje?
Jibu:
Ugonjwa wa kansa ya chembe chembe nyeupe za damu, huwapata watu wenye
umri mkubwa na utafiti wa kisayansi haujafanikiwa kutambua ni kitu gani
hasa kinacholeta kansa hii. Kwa kawaida, kansa hii haioneshi dalili
wakati inapoanza na wengi wanagundulika kuwa nayo bila kuihisi.
Wagonjwa
wengi wanaishi zaidi ya miaka miwili bila kuhitaji matibabu, ni pale tu
ambako kansa hii inapoathiri kazi ya chembe chembe nyingine nyeupe au
nyekundu ndipo matibabu yanapoweza kufikiriwa.
Kinachohitajika ni mgonjwa kuonwa na daktari mara kwa mara, ili athari hizi zikionekana matibabu yaanze mara moja.
Swali: Baada ya kugundulika kwa ugonjwa wa Mwalimu, ulimshughulikia namna gani?
Jibu:
Baada ya Mwalimu kugundulika kuwa na kansa mwezi Agosti 1998, alielezwa
kuhusu ugunduzi huo na kuambiwa kuwa wakati ule ugonjwa ulikuwa
haujafikia hatua ya kuhitaji matibabu. Alielezwa haja ya kwenda kupimwa
mara nyingi zaidi kuliko ilivyokuwa kawaida yake na kwamba hapakuwa na
sababu ya kubadilisha mwenendo wa shughuli zake.
Ratiba
tuliyopewa ilimfanya Mwalimu arejee London, Novemba 1998, na majibu
yaliyoonesha kuwa hakukuwa na sababu ya kuanza matibabu. Aidha, mwezi
Januari 1999 alipimwa tena kwa mara nyingine ikaonekana hakuna haja ya
kuanza matibabu.
Mwezi
Mei 1999 alikwenda tena London akapimwa. Aliambiwa hakukuwa na sababu
ya kuanza matibabu na akapewa tarehe nyingine mwezi Agosti, 1999.
Safari
hii hitilafu zikaonekana katika damu. Hitilafu hizo zilionesha ulazima
wa matibabu ya kansa kuanzishwa. Mwalimu alishauriwa kurudi London,
Desemba 1999. Lakini hali yake ikabadilika kabla ya kurejea nyumbani
hadi ikabidi alazwe katika hospitali ya Mtakatifu Thomas ambako
alipoteza maisha yake.
Swali:
Mmoja wa watoto wa Mwalimu amedai kuwa familia haikujulishwa kuhusu
ugonjwa wa Mwalimu. Kuna ukweli wowote katika madai hayo?
Jibu:
Mwalimu mwenyewe aliwaeleza baadhi ya wanafamilia yake waliokuwa karibu
naye, kuhusu maradhi yake na mimi nilijua hivyo kwa vile hao
aliowaeleza waliniambia na wakawa wakiniuliza maswali kuhusu ugonjwa
wake.
Swali:
Ukiwa daktari wa Mwalimu kwa muda mrefu, uliyekuwa ukisafiri naye mara
nyingi na kuwa naye karibu, je, unaweza kuzungumzia lolote kuhusu maisha
yake?
Jibu:
Mara nyingi tukiwa pamoja aliuliza maswali mengi kuhusu ugonjwa wake na
alisoma vijitabu kuhusiana na ugonjwa huo. Nadiriki kusema kwamba
aliufahamu ugonjwa huo kwa kina.
Madaraka Nyerere azungumza
Madaraka
Nyerere, mmoja wa watoto wanane wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere,
amezungumza na kusema ingawa haafiki kuanza uchunguzi wa kifo cha
babake, lakini kuna viashiria fulani fulani vinavyotia shaka.
Viashiria
hivyo, kwa mujibu wa Madaraka, ni namna alivyoanza kuikosoa Serikali
kwa mambo mengi, jambo analosema inawezekana halikuwafurahisha wengi.
Katika
mahojiano yake na JAMHURI wakati huu wa maadhimisho ya miaka 14 ya kifo
cha Baba wa Taifa, Madaraka ambaye kwa kawaida ni mpole, ameeleza
yafuatayo:
“Binadamu
wengi wanapenda sana kuamini kuwa kila jambo likitokea, basi kuna mkono
wa mtu. Na hivi karibuni kifo cha Mwalimu Nyerere kimehusishwa na njama
mahususi za kumuua.
“Kwa
desturi za Kizanaki, hakuna mtu anayekufa kwa sababu ya ugonjwa au
uzee, lazima yuko mtu miongoni mwa wale waliobaki hai ambao
wamesababisha kifo chake kwa njia za uchawi. Kwa mfano, Bibi Christina
Mugaya wa Nyang’ombe, mama mzazi wa Mwalimu Nyerere, mara baada ya kifo
cha mume wake, Mtemi Nyerere Burito, tarehe 30 Machi 1942, alitimuliwa
Butiama na kuhamia kwa ndugu zake katika kijiji jirani cha Muryaza,
baada ya kutuhumiwa kuwa alisababisha kifo cha mume wake.
“Kwa
hiyo hakurithiwa kama ilivyo desturi za wakati ule za mila za Kizanaki
na akaishi kwa jamaa zake hadi Mwalimu Nyerere alipotoka masomoni
Uingereza na kudai arudi nyumbani na akarudi, ingawa baadhi ya ndugu
zake hawakufurahia kurudi kwake Butiama.
“Kwa
hiyo basi, ni kawaida kabisa kwa hisia kama hizi kuwapo ndani ya jamii.
Lakini, kusema hivi haina maana kuwa haiwezekani kuwa tuhuma hizo ni za
kweli. Lakini mtu yeyote muungwana hawezi kuanza kutoa shutuma nzito
kama hizi bila kuwa na ushahidi usiotiliwa shaka na ambao hauna dosari.
“Lakini
naweza kuelewa kwanini baadhi ya watu ambao wanashikilia hizi tuhuma
kuwa zinaweza kuwa ni kweli. Tunamfahamu Mwalimu Nyerere kuwa, hata
baada ya kustaafu, hakukalia kimya uamuzi au matukio ambayo aliamini
yanaathiri baadhi ya misingi ambayo yeye aliiona kuwa ni nguzo
inayoshikilia nchi yetu. Baadhi ya haya ni uadilifu ndani ya uongozi,
umoja, uzalendo, na sera zenye kujali masilahi ya wengi badala ya sera
zinazokuza na kulinda nafasi kwa wachache kujinufaisha.
“Na
kwa kweli ukichunguza baadhi ya matukio kwenye nyanja ya siasa katika
kipindi hiki ambacho amefariki, yametokea mengi ambayo tunaamini kuwa
kama angekuwa hai asingenyamaza na angeyazungumzia kuyapinga na
kuyakemea au kuyatungia kitabu pale ambako ujumbe wake aliona unapuuzwa.
Kwa
hiyo, mtu yeyote anayefuatilia hali ya uongozi nchini, na watu wengi
wanasema hivi, ni kuwa Mwalimu Nyerere angekuwapo labda baadhi ya uamuzi
na mienendo ya baadhi ya viongozi wetu ungekuwa tofauti kwa kuogopa
kauli yake au kuandikiwa kitabu , kitakachojenga hoja inayopingana na
uamuzi wa viongozi. Na pengine baadhi ya uamuzi ambao umefanyika,
usingefanyika.
“Kwa
hiyo kwa mantiki hii unaweza kuanza kujenga hoja kuwa baadhi ya wale
waliofanya uamuzi unaoonekana unaenda kinyume au na maadili ya uongozi,
au unapingana na masilahi ya umma, walitafakari kuwa njia rahisi ya
kurahisisha mipango yao ni kumuondoa huyu mzee mapema. Hiyo unaweza
kusema, lakini haitakuwa sahihi kufanya hivyo bila kuwa na ushahidi.
“Nimewahi
kusikia tuhuma kuwa Rais Kikwete anatuhumiwa kuwa ndiye mtu aliyetumwa
na nchi za Magharibi kukimaliza Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nilivyosikia
tuhuma hizi niliona kichekesho, lakini ukiangalia baadhi ya matukio
katika uongozi wake ambayo yanaweza kuashiria hoja hiyo, unaweza
kuyapata.
“Enzi
za Mwalimu Nyerere waliotuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya uongozi
waliitwa pembeni na kuambiwa wajiuzulu. Miaka ya hivi karibuni wale
ambao walikabiliwa na tuhuma za aina hiyo waliombwa kutafakari wao
wenyewe uamuzi sahihi wa kuchukua. Uamuzi mgumu haufanyiki, upinzani
wanapata mada ya kuzungumzia kwenye mkutano wao ujao, na CCM inazidi
kudhoofu. Kama nilivyosema hakuna ushahidi wa wazi, lakini kuna
viashiria tu.
“Nafikiri
njia nzuri ya kufunga mjadala huu ni kuzungumza kama wanasheria
wanavyosema: hakuna ushahidi mpaka sasa unaothibitisha hizo tuhuma juu
ya njama za kumuua Mwalimu Nyerere.
“Hoja
kuwa uchunguzi ufanyike kubaini kama aliuawa, sioni kama zitaleta faida
yoyote kwa sababu ameshafariki tayari na hakuna uchunguzi utakaorudisha
uhai wake. Tunamkumbuka Mwalimu Nyerere kwa maandishi na matamshi yake.
Na naamini kuwa katika uhai wake aliandika na kutamka masuala yote
aliyoamini ni ya msingi kwake na kwa jamii.
“Kuna
kiongozi mmoja aliyewahi kusema iwapo kuna wazo la msingi ambalo
binadamu amelisema katika uhai wake, basi hilo wazo litadumu hata kama
aliyelisema hayuko tena duniani. Badala ya kutafuta wachawi sasa hivi,
mimi nafikiri wale wote ambao wanaamini kuwa Mwalimu Nyerere alitoa
mchango mkubwa kwa nchi hii, watumie muda wao kutafakari kazi aliyofanya
na kujumuisha fikra zake na matendo yake kupima yale ambayo bado
yanaweza kuwa suluhisho dhidi ya baadhi ya changamoto zinazoikabili
Tanzania sasa hivi.
“Iwapo
hoja zake zina nguvu katika mazingira ya sasa, basi hazihitaji yeye
mwenyewe kuzisemea. Wanaoziamini wazichambue na wazitumie kama silaha ya
kupambana na upungufu ambao tunauona leo katika nyanja mbalimbali.
“Lakini
pia ni muhimu kwa vijana kujitafutia elimu kuhusu hayo yaliyopita, ili
kupata mifano mizuri ya uongozi ambayo iliweka masilahi ya Taifa mbele
na kuzuia kabisa hizi hoja za siku hizi za kumpa kila mtu fursa ya
kufanya anavyotaka. Zinazungumzwa fursa za mwananchi, lakini ukweli ni
kuwa baadhi ya viongozi wanapigana vikumbo na wananchi hao hao kutafuta
fursa zao binafsi,” amesema Madaraka
No comments:
Post a Comment