WAKATI Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), likisubiri majibu ya
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), juu ya hatima ya usajili wa
mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Okwi, Fifa wamekiri kuwa na vielelezo
vya Okwi na watatoa ufafanuzi.
Msemaji wa Fifa, Alois Hug, ameliambia Mwanaspoti
jana Jumapili kwamba tayari wameshapokea barua ya TFF, wakiomba kupatiwa
ufafanuzi juu ya usajili wa mshambuliaji huyo raia wa Uganda na muda
mwafaka watatoa jibu.
Hug alisema baada ya kupokea barua ya TFF,
wameanza kuifanyia kazi kwa kuipeleka katika kitengo kinachohusika na
usajili ili kupatia majibu yatakayotoa hatima ya Okwi kuitumikia Yanga.
Alisema, kwa sasa hawezi kutoa jibu lolote kuhusu
hatima ya mshambuliaji huyo ambaye Simba ilimuuza katika klabu ya Etoile
du Sahel ya Tunisia mapema mwaka jana kabla ya mchezaji huyo kuondoka
Tunisia akidai kutolipwa haki zake na kurudi klabu yake ya awali ya
Sports Club Villa ya Uganda iliyomuibua.
Hata hivyo akiwa Villa, Okwi alisajiliwa na Yanga,
usajili uliokuwa kiini cha utata kati ya mchezaji huyo na klabu ya
Simba ambayo bado inaidai Etoile na kuifanya TFF itafute ufafanuzi
kutoka Fifa.
“Tunachoweza kukuthibitishia ni kwamba Fifa
tumeshapokea barua kutoka TFF wakiomba ufafanuzi juu ya usajili wa
Okwi.” kwasasa hatuwezi kusema lolote mpaka ufafanuzi utakapotolewa,”
alisema.
No comments:
Post a Comment