Mchungaji Ambilikile Mwaisapila (Babu wa Kikombe) wa Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri Tanzania (KKKT), amesema Mungu ameendelea kujifunua kwake
na kumuonesha kuwa Tanzania itakuwa kioo cha Afrika na dunia kwa ujumla.
Alitoa
kauli hiyo juzi mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati akizungumza
na wakazi wa kijiji cha Samunge, wilayani Ngorongoro mkoani Arusha
wakati msafara wa Waziri Mkuu uliposimama nyumbani kwake ili kumsalimia
akiwa njiani kurejea mjini Arusha.
Mchungaji
Mstaafu Mwaisapila alisema kuna mambo mengi ambayo yameandikwa kwenye
Biblia, lakini hayakutokea Israeli na sasa yatafanyika hapa Samunge.
“Mungu
ametupenda sana, yanakuja mambo makubwa na wala hayako mbali. Kama mimi
ni mzee na nitayaona, kwa hiyo mtarajie kuwa hayako mbali kutokea,”
alisema huku akishangiliwa na wananchi.
Alisema
katika mafunuo aliyopewa na Mungu ameoneshwa kwamba watu wengi zaidi
watafurika kijijini Samunge kuliko ilivyokuwa hapo awali. Alitumia fursa
hiyo kuishukuru Serikali kwa misaada iliyotoa wakati wa kugawa kikombe
ikiwemo mahema, maji na ulinzi.
Waziri
Mkuu, Pinda ambaye yuko mkoani Arusha kwa ziara maalum ya kusikiliza
matatizo na migogoro ya ardhi yanayowakabili wakazi wa wilaya ya
Ngorongoro, katika tarafa za Ngorongoro, Loliondo na Sale alisema
anakubaliana na utabiri wa Mch. Mwaisapila kwani Tanzania imejaliwa gesi
nyingi na mafuta mengi ambavyo vitabadili sura ya Taifa hili.
"Mungu
ametupa gesi nyingi sana, katika miaka miwili tutakuwa na umeme kila
mahali. Tuna makaa ya mawe ambayo ni nishati kubwa na sasa tuna fursa ya
kupata nishati ya umeme kutoka ardhini (Geo-thermal) katika Ziwa
Natron," alisema.
Alisema
Tanzania imekuwa kimbilio la kila mwekezaji na sababu kubwa ni amani na
utulivu uliopo nchini. Aliwaeleza wakazi wa Samunge kwamba mapema
mwakani mkandarasi wa barabara atakuwa katika eneo lao kwa ajili ya
ujenzi wa barabara ya lami ambapo awamu ya kwanza itaanzia Wasso hadi
Mto wa Mbu kupitia Samunge.
No comments:
Post a Comment