Sunday 29 September 2013

Mtuhumiwa ugaidi Kenya alipitia Arusha


Wakati Serikali ya Kenya imeliomba Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) kumkamata Mwingereza Samantha Lewthwaite (pichani), taarifa zinadai kuwa mwanamke huyo alipitia mpaka wa Namanga, Arusha kwenda Nairobi ambako anahusishwa na tukio la ugaidi.
Lewthwaite, ambaye ni maarufu kwa jina la ‘Mjane mweupe’ inaaminika anashirikiana na kundi la magaidi la Al-Shabab la Somalia.
Kundi hilo ndilo linaaminika lilihusika na mashambulizi kwenye jengo la Westgate jijini Nairobi, wikiendi iliyopita.
Hata hivyo, taarifa ya Interpol ilisema kuwa alikuwa anatakiwa kujibu mashtaka ya kumiliki mabomu na kupanga njama za ugaidi Desemba 2011.
Interpol haikuhusisha maombi hayo ya Serikali ya Kenya na mashambulizi ya Nairobi.
Pia Lewthwaite inasemekana aliingia nchini humo kwa kutumia mpaka wa Tanzania.
Baadhi ya vyombo vya habari vya Afrika ya Kusini, vinasema mwanamke huyo alitumia pasi ya kusafiri ya nchi hiyo kuingia Kenya kwa kutumia mpaka wa Namanga uliopo mkoani Arusha.
Taarifa hizo zinasema mwanamke huyo alitumia mpaka wa Lunga Lunga na Namanga kati ya Februari na Agosti mwaka 2011 akitumia jina la Webb.

No comments:

Post a Comment