Friday 27 September 2013

UN yajadili azimio kuhusu Syria


Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linajadili rasimu ya azimio kuhusu silaha za kemikali za Syria baada ya Marekani na Urusi kukubali mapendekezo ya azimio hilo.
Wanachama kumi na tano wa baraza hilo huenda wakapigia kura azimio hilo baadaye leo, hii ni kwa mujibu wa wanadiplomasia katika umoja wa Mataifa.
Makubaliano hayo yanamaliza mvutano wa miaka miwili na nusu katika Umoja wa mataifa kuhusu Syria.
Inaonekana kama hatua muhimu katika mwafaka unaosakwa sana kwa ushirikiano wa Marekani na Urusi ambapo Syria itafichua zana zake za kemikali na kuziharibu ifikapo mwaka 2014
Urusi na China mara tatu zimekuwa zikizuia maazimio ya nchi za magharibi katika baraza la usalama dhidi ya Rais wa Syria, Bashar al-Assad.
Baraza hilo lilijadili azimio hilo Alhamisi Jioni katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa.
Kabla ya mkutano huo Marekani na Urusi zilitofautiana kuhusu maandiko na mapendekezo ya azimio hilo.
Marekani kwa ushirikiano na Ufaransa na Uingereza, zilikuwa zimependekeza kuchukau hatau za kijeshi dhidi ya Syria.
Urusi nayo ilipinga azimio hilo kwa sababu ya tisho la kuvamia Syria kijeshi.
Mataifa hayo ni wanachama wenye uwezo wa kupiga kura ya turufu dhidi ya pendekezo lolote katika baraza hilo.

No comments:

Post a Comment