Nairobi. Shambulizi la kigaidi lililoua watu 67
nchini Kenya wiki iliyopita, limeanza kuchukua sura mpya baada ya
kubainika kuwa mawaziri wanne na mkuu wa majeshi walipewa tahadhari
kabla kuhusu kutokea kwa tukio hilo.
Taarifa hizo mpya zimekuja wakati ripoti nyingine
za uchunguzi zikibainisha kuwa huenda magaidi walioshambulia jengo la
Westgate walitoroka kupitia njia ya ardhini inayoanzia kwenye maegesho
ya magari chini ya jengo hilo.
Kuhusu mawaziri
Tahadhari hiyo iliyoanza kutolewa Januari mwaka
huu, iliwaonya viongozi hao ambao pia ni wanachama wa Baraza la Usalama
la Taifa, kuwa Kundi la Al-Shabaab lilikuwa likipanga shambulizi jijini
Nairobi.
Kwa mujibu wa ripoti ya kuzuia ugaidi iliyonukuliwa na Gazeti la The Saturday Nation,
imewataja Waziri wa Fedha, Julius Rotich, Waziri wa Mambo ya Ndani,
Joseph ole Lenku, Waziri wa Ulinzi, Raychelle Omamo, Waziri wa Mambo ya
Nje, Amina Mohammed na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Julius Karangi kuwa
walikuwa na taarifa za shambulizi hilo.
“Taarifa ilitolewa kwao ikiwatahadharisha
kuongezeka kwa vitisho vya ugaidi na mipango ya kuanzishwa kwa
mashambulizi mfululizo katika miji ya Nairobi na Mombasa kati ya
Septemba 13 na 20, 2013,” inasema ripoti hiyo.
Ripoti hiyo inasema kuwa magaidi walikuwa
wakipanga shambulizi linalofanana na lile lililotokea Mumbai, India
ambapo walishambulia jengo na kuteka raia.
Pia, taarifa hiyo ilitolewa kwa Kamati ya Ushauri
ya Usalama wa Taifa katikati ya Septemba, mwaka huu ambapo taarifa za
kiintelijensia zilionyesha kuwa Al-Shabaab wameongeza harakati zao Kenya
na kwamba walikuwa wanapanga shambulizi.
Kamati hiyo ambayo ndiyo ngazi ya juu ya usalama
nchini Kenya, inajumuisha Rais, Naibu Rais, Waziri wa Ulinzi, Mambo ya
Nje, Mambo ya Ndani, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Majeshi,
Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa na Mkuu wa Jeshi la Polisi.
Viongozi wote waliotajwa kupewa taarifa
hawakupatikana, hata ujumbe mfupi wa maandishi waliotumiwa na gazeti
hilo kwenye simu zao haukujibiwa.
Shambulizi la wiki iliyopita kwenye jengo la
kibiashara la Westgate jijini Nairobi, linalomilikiwa wa raia wa Israel,
liliua watu 67 na zaidi ya watu 170 kujeruhiwa.
No comments:
Post a Comment