Utata umeibuka kuhusu alipo mfanyabiashara maarufu nchini, Alex
Masawe baada ya kuwepo kwa tetesi kuwa ameachiwa huru huko Dubai, Falme
za Kiarabu (UAE) alikokuwa akishikiliwa.
Masawe ambaye alikamatwa katika uwanja wa ndege
huko UAE akitokea Afrika Kusini, kati ya Juni 20 na 25, mwaka jana,
anatuhumiwa kwa makosa mbalimbali yakiwamo ya mauaji.
Mkuu wa Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) -
Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile alikiri
kuwapo kwa taarifa kwamba Masawe ameachiwa huru na hayupo Dubai ingawa
bado tawi la Interpol katika nchi hiyo halijatoa taarifa yoyote.
“Tumejaribu kuwasiliana nao mara kwa mara kuhusu
kumrudisha nchini lakini hawajajibu lolote. Hivi karibuni tuliwasiliana
nao lakini hawajatujibu, kwa hiyo tumebaki na maswali. Kwa kifupi
hatujui alipo hadi sasa,” alisema Kamishna Babile.
Alisema awali, baada ya kukamatwa huko Dubai, Tawi
la Interpol Tanzania lilikuwa linafanya mchakato wa kumrudisha nchini
ikiwamo kutuma ombi la kumrejesha mhalifu nchini, lakini ghafla
mawasiliano yakakatika.
“Taarifa zilizopo ni kuwa Masawe ameachiwa huru, kwa vigezo gani hatuelewei,” alisema Babile.
Babile alisema iwapo atakuwa ameachiwa na polisi
wa UAE, basi itakuwa ameachiwa kutokana na sheria za nchi hiyo ingawa
bado Tanzania itaendelea kumsaka kwa udi na uvumba.
“Sisi tutaendelea kumsaka kama kawaida, iwapo
atakamatwa nchi nyingine au ikitokea akaonekana hapa nchini, tutaendelea
na mchakato wa kumfungulia kesi kwa sababu sisi tunajua kuwa ana
makosa,” alisema Babile.
Massawe alitajwa mahakamani Aprili 4, mwaka jana
katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara, Onesphory Kituly ambaye aliuawa
katika mazingira ya kutatanisha Novemba 6, 2011 nyumbani kwake
Magomeni, Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo, mshtakiwa wa kwanza ni
mfanyabiashara Abubakar Marijani, maarufu kama ‘Papaa Msofe’ na
mshtakiwa mwingine ni Makongoro Joseph Nyerere.
Nyerere aliwahi kulalamika mbele ya Hakimu Mkazi,
Agnes Mchome anayesikiliza kesi hiyo, akidai kwamba kumekuwa na
ucheleweshaji wa shauri hilo kutokana na ndugu wa marehemu Kituly kutaka
Massawe akamatwe ili ajumuishwe.
Mtuhumiwa huyo aliomba jalada la kesi yao
lipelekwe mahakamani hapo kwa ajili ya kulifanyia kazi. Alitoa
malalamiko hayo baada ya Wakili wa Serikali, Mwanaisha Kombo kudai
upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe mpya ya
kutajwa kwake.
Mwananchi
Mwananchi
No comments:
Post a Comment