LICHA ya umilionea wake mkubwa unaoongezeka kila kukicha
kutokana na mafanikio yake makubwa katika soka, wazazi wa staa wa Real
Madrid, Gareth Bale wameendelea kuishi katika nyumba yao ya kimaskini
jijini Cardiff.
Si kwa sababu ya tabia za uchoyo za staa huyo,
hapana, Bale si mchoyo, lakini wazazi wake wenyewe wamemkatalia kuhamia
katika nyumba ya kifahari aliyowanunulia kwa sababu wanapenda kuendelea
kukaa katika nyumba ya kota.
Bale, ambaye ni mwanasoka ghali zaidi duniani
baada ya kuhamishwa kwa kiasi cha Pauni 85 milioni kutoka Tottenham
Hotspur kwenda Real Madrid katika usajili wa kipindi cha majira ya joto
cha mwaka jana alisema angewapatia wazazi wake, Frank na Debbie kiasi
cha Pauni 1 milioni kwa ajili ya kutafuta jumba la kifahari la kununua
na kutimiza ndoto zao za kuishi maisha mazuri.
Lakini wazazi hao walimwambia Bale (24), kwamba
wamezoea na kusikia raha kuishi katika nyumba yao ya vyumba vitatu
ambayo Bale alikulia kabla ya kuibuka kuwa mchezaji ghali duniani.
Debbie (50), alimwambia rafiki wa familia yake
hiyo kwamba kitendo cha Gareth kuwapa ofa ya nyumba kilikuwa cha huruma
na kizuri, lakini wanapenda kuendelea kuishi walipo huku wakiwa na
majirani wazuri waliowazoea.
Yeye na mumewe, Frank (54), ambaye ni mstaafu wa
shule moja jijini humo, walinunua nyumba hiyo ya kawaida kwa kiasi cha
Pauni 12,000 miaka 30 iliyopita kabla ya Bale hajazaliwa na kwa sasa
nyumbani hiyo ina thamani ya Pauni 170,000.
Ni hapo ndipo walipomlea Bale na dada yake, Vicky
huku Bale akijifunza kucheza soka katika bustani iliyopo kando ya nyumba
hiyo na kuharibu mali za watu.
Baada ya kupatiwa kiasi hicho cha pesa na Bale kwa
ajili ya kusaka nyumba, yeye na mumewe walienda kutafuta nyumba ya
kifahari katika eneo la Vale of Glamorgan. Vile vile walitafuta nyumba
yenye thamani ya Pauni 415,000 karibu na eneo la wanaloishi.
Hata hivyo, mwishowe waliamua moja kwa moja kubaki
katika nyumba yao waliyoishi kwa miaka 30 iliyopita ambayo inaashiria
historia yao huku wakigoma kuwaacha majirani zao wenye upendo wa dhati
kwao.
Debbie alimwambia rafiki yake mmoja kuwa wanapata
kila wanachokitaka kwa kuwa hapo na itakuwa jambo gumu kwao kuhama
katika nyumba ambayo watoto wao walikulia.
No comments:
Post a Comment