Kiteto. Wamasai ni miongoni wa jamii chache
duniani, ambazo zimefanikiwa hadi sasa kudumisha mila zake. Katika mila
za jamii hii, zipo ambazo zinapaswa kuendelezwa na nyingine zinapaswa
kupigwa marufuku.
Miongoni mwa mila ambazo zinapaswa kuendelezwa ni
pamoja na kuendelea kutambua na kuheshimu viongozi wa mila ‘Laigwanaji’
kuheshimu viongozi wa rika na Serikali, kuishi kwa umoja na kudumisha
tamaduni.
Mila ambazo zimepitwa na wakati katika jamii hii ni pamoja na kurithi wajane, ukeketaji watoto na kuoa watoto wadogo.
Katika makala hii, leo nitazungumzia mila ya kuoa
watoto wadogo kama nilivyobaini katika vijiji kadhaa wanapoishi Wamasai,
wilayani Kiteto, Mkoa wa Manyara.
Nikiwa katika uchunguzi wa mapigano baina ya
wafugaji wa Kimasai na wakulima katika vijiji saba vinavyozunguka eneo
la Hifadhi ya Emborey Murtangosi nakutana na mtoto wa miaka 12
aliyeolewa.
Nilipata bahati ya kufika katika familia ya mtoto
huyu, katika Kitongoji cha Ndiligishi kaya ya Engusero Sidani baada ya
kuwa ni moja ya familia ambazo zimeathirika na mapigano baada ya
kuchomewa makazi na kuibiwa vyakula.
Wakati nahojiana na wanafamilia napata fursa ya
kuonana na mtoto huyo aliyegeuzwa kuwa mke, nashawishika kumuhoji baada
ya kuona akiwa amejitenga na watoto wenzake huku akiwa na mawazo.
Mtoto huyo ambaye jina lake tumelihifadhi kutokana
na sababu za kimaadili, hajui kiswahili vizuri, hivyo nalazimika
kumuomba mtoto mwenzake, Stela Paulo aje anisaidie kuongea naye.
Ananieleza kuwa yeye ni mke wa Lembau Leseri na ameolewa mke wa pili na ana miaka miwili ya ndoa.
Akiwa anaonekana kutokuwa na raha ya maisha,
mtoto huyo anasema wazazi wake, ndio walimpeleka kwa mwanaume baada ya
kupewa mahali.
Anasema hajui kusoma wala kuandika kwani hakufanikiwa kupelekwa shule na wazazi wake.
Ninapomdadisi kama angependa kusoma, anasema angepata fursa hiyo angefurahi lakini sasa haiwezekani tena kwani ni mke mtu.
Kwa umri wake na umbile bado ni mdogo lakini, anaeleza huku
akiwa kichwa chini na kwa aibu kuwa majukumu yote muhimu kwa mume wake
aliyepewa na wazazi anafanya.
Hata hivyo, mtoto huyu anaonekana afya yake kudhoofika kutokana na maradhi ya ngozi na huenda na majukumu ya kifamilia.
Mume wa mtoto azungumza.
Mume wa mtoto huyo, Lembau Leseri hivi sasa ni
mgonjwa na takriban wiki mbili, alikuwa amelazwa hospitali ya kiteto
kutokana na kutokewa na majipu mwilini.
Ananieleza kuwa, mtoto huyo ni mke wake wa pili, ambaye alimuoa kutoka kijiji jirani cha Taiko.
Anasema mke wake wa kwanza, Kawie Lembau sasa ana watoto saba.
Lembau haoni kama amefanya makosa kuoa mtoto mdogo, kwani ananieleza kuwa alimuoa kwa ng’ombe 15.
Hata hivyo, anaeleza maisha yake ya ndoa na mtoto
huyo, hayakuwa ya taabu kwa mwaka mmoja uliopita lakini sasa ana
matatizo kutokana na kukabiliwa na maradhi.
“Sijui naumwa nini kwani nimelazwa hospitali na wamenipa dawa nirudi nyumbani,” anasema.
Anasema licha ya maradhi yanayomkabili, maisha
yamekuwa ya magumu, mapigano ya ardhi yameifanya familia yake kukosa
chakula kwani zaidi ya magunia 50 ya mahindi yaliibwa.
Anasema pia vijana wa kiume wa familia yao,
wamekimbia kwa sababu polisi wanaendesha msako kuwakamata waliohusika
na mauwaji ya wakulima tisa kutokana na mapigano ya ardhi.
“Hali ni ngumu, mimi naumwa siwezi kutembelea
umbali mrefu kutafuta chakula, vijana wa hapa wamekimbia wanaogopa
polisi,”anasema Lembau
Hali ya njaa katika familia hiyo yenye maboma matatu,
inathibitishwa na jinsi nilivyoikuta akina mama wazee na watoto wadogo
walikuwa wakichemsha mchicha majira ya saa saba lakini hadi naondoka
takriban saa tisa walikuwa hawajala chakula kingine.
Mke mkubwa
Mke mwingine wa Lembau ambaye anaonekana ni mtu
mzima ni mkimya na nilipotaka anieleze kuhusiana na mke mwenza wake
anashindwa kusema kitu na anaingia ndani ya boma lao.
Lakini natambua kwa mila za kimasai ni nadra sana
mwanamke kuwa na ujasiri kupingana na mwanaume kutokana na misingi ya
mila na desturi zao.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wazungumza.
Shilinde Ngalula ni Mkuu wa Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC), anapatwa na mshangao anapoelezwa mtoto huyo ni
mke wa mtu hasa kutokana na umri wake mdogo.
Hata hivyo, baada ya kuzungumza naye anaeleza kusikitishwa na maisha ya ndoa ya mtoto huyu.
“Hili ni tatizo kubwa katika jamii hizi kwani
mtoto huyu alipaswa kuwa shule lakini kaolewa na mtu mzima ambaye sasa
ni mgonjwa,”anasema Shillinde.
Shilinde na maafisa wengine wa LHRC ambao
wanafanya uchunguzi wa mapigano baina ya wakulima na wafugaji wilayani
Kiteto Mkoa wa Manyara, anaahidi kutafuta muda muafaka kufuatilia maisha
ya mtoto huyo.
“Jamii hizi za pembezoni zinakabiliwa na matatizo
mengi ambayo mengine yanatokana na kutokuwa na mazingira bora ya kupata
elimu na huduma nyingine muhimu”
Shillinde hata hivyo, anaongeza kuwa umefika
wakati, Serikali na wadau wengine kufika maeneo ya vijiji katika jamii
kama za kimasai ili kusaidia kutatua matatizo yao ikiwepo ya
umasikini,elimu na mila zilizopitwa na wakati.
Je, maisha ya ndoa ya mtoto huyu yataendelea vipi
kwa sasa kwani licha ya kuwa na umri mdogo bado ana mzigo mkubwa wa
kumuuguza mume wake na je, nani atamuokoa na ndoa ya utotoni na
kumrejesha shule kwa watoto wenzake?Hili ni swali zito lisilo na jibu kwa sasa hata hivyo huenda LHRC
wakalivalia njuga suala hilo na haki kupatikana kama ambavyo tayari
wameahidi.
mwananchi
mwananchi
No comments:
Post a Comment