Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza kumhoji Mwakilishi wa Uzini,
Mohamed Raza, kwa tuhuma za kugombanisha viongozi na wananchi na
kushindwa kutetea misingi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Raza anatuhumiwa kufanya hayo katika matamshi
anayodaiwa kuyatoa kwa waandishi wa habari kupitia mkutano wake wa
Oktoba mwaka jana na mkanda wa video umetumika kama ushahidi katika
kikao cha Kamati ya Siasa ngazi ya jimbo na wilaya.
Akizungumza na waandishi wa habari huko Malindi
jana, Raza alisema ametakiwa kujibu hoja 16 na Kamati ya Siasa ya Jimbo
la Uzini na kwamba tayari kamati imetoa mapendekezo kwa ngazi ya wilaya.
Alisema kikao cha kwanza kilikutana Oktoba 27
mwaka jana na kumtaka ahudhurie kwa madai kuwa kulikuwa na mambo muhimu
aliyopaswa kuyatolea ufafanuzi kutokana na matamshi yake katika mkutano
wake na waandishi wa habari.
“Niliwasilisha ombi la udhuru kutokana na
kukabiliwa na safari nchini Dubai, nikaomba wanitajie maeneo ambayo
hawajayafamu ili niwajibu kwa maandishi, wenzangu walikuwa wagumu na
waliendelea kunijadili bila kunipa nafasi ya kujitetea,” alisema Raza.
Alisema wakati akitafakari hayo, alipokea barua
nyingine ya wito kutoka Wilaya ya Kati akitakiwa ahudhurie kikao cha
Desemba 13 huko Dunga na kujibu tuhuma 16. Raza aliwataja baadhi ya
viongozi waliohudhuria kikao hicho kuwa ni, Hassan Mrisho Vuai, Shukuru
Adam Ali, Ame Abdallah Ame, Shaaban Jabu Kitwana, Mju Silima Makame na
Arada Ali Abdallah.
Wengine ni Vuai Ali Mohamed, Usi Ali Mtumwa,
Salama Mussa Bilal, Khalfan Salum Suleiman, Ali Makame Usi, Mussa Ali
Hassan na Haji Mkema Haji.
Raza alizitaja tuhuma zinazomkabili kuwa ni pamoja
na kuzungumzia hadharani, masuala mazito na yenye utata akiwa
mwakilishi wa CCM, kuhoji uhalali wa marais Dk Jakaya Kikwete na Dk Ali
Mohamed Shein kuhusu kuunda Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba na
kuitisha Bunge la Katiba.
Nyingine ni kutetea muundo wa Serikali tatu, kuwahasimisha wananchi wa Bara na Zanzibar kuchukiana na viongozi wa Muungano.
Nyingine ni kutamka kuwa Watanganyika hawawezi kutawala Zanzibar na kwamba wakijaribu watatawala miembe na minazi.
Pia kutoa kuponda ilani ya uchaguzi inayotaka Serikali mbili akisema mwisho wake ni Kisiwa cha Chumbe.
Mwananchi.
Mwananchi.
No comments:
Post a Comment