Wednesday, 22 January 2014

 Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume 
OFISI za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zinatarajiwa kuhama kwa muda Karume, Ilala jijini Dar es Salaam mapema mwezi ujao kupisha uendelezaji wa eneo hilo, ikiwa ni moja ya ilani za Rais mpya, Jamal Malinzi.

Eneo hilo linatarajiwa kujengwa jengo la ghorofa 12 sambamba na maduka kuzunguka Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Chanzo cha habari cha uhakika kutoka ndani ya shirikisho hilo, kiliiambia Tanzania Daima kwamba ofisi hizo za TFF sasa zitahamia maeneo ya Posta mpya katika jengo la PPF ili kupisha ujenzi huo na kila kitu kimekamilika kwa ajili ya uhamisho huo.
Mtoa habari huyo ambaye hakutaka kuandikwa jina lake gazetini, alisema malengo ya Malinzi ni kujengwa jengo la kitega uchumi Karume, ambalo mbali na ofisi linatarajiwa kuwa na maduka zaidi ya 100 kuzunguka eneo hilo.
“Hii ni moja ya ilani ya Malinzi wakati wa kampeni zake kama mnakumbuka, mwezi ujao mwanzoni tunahama hapa na kwenda PPF na ujenzi unaanza mara moja,” alisema mtoa habari huyo.
Aliongeza kuwa lengo la kufanya ujenzi huo ni kuongeza fedha ndani ya shirikisho na kupunguza kuhangaika kusaka wadhamini, licha ya kuwa wao ni muhimu katika maendeleo ya soka nchini.
TFF inamiliki Uwanja wa Karume wenye hati namba 27026 iliyotolewa Novemba 10, 1981 wenye ukubwa wa ekari 8.2.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment