Uamuzi wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuruhusu malori makubwa ya
mizigo yaendelee kuzidisha uzito wa mizigo, umetajwa kuwa ni hatari na
utaisababishia Serikali hasara ya mamilioni ya fedha.
Hasara hiyo inatokana na uharibifu wa barabara za
lami ambao unachangiwa kwa kiasi kikubwa na malori yanayozidisha uzito
wa mizigo kinyume cha sheria na kanuni namba 7 (3) ya Sheria ya Usalama
Barabarani ya 2001.
Ujenzi wa barabara ni wa gharama kubwa na hata
ukarabati wake umekuwa ukitengewa mabilioni ya fedha za walipakodi
kutokana na uharibifu unaofanywa.
Mathalani katika bajeti yake ya 2013/14, Serikali
kupitia Wizara ya Ujenzi, imetenga kiasi cha Sh314.535 bilioni kwa ajili
ya mpango wa matengenezo ya barabara kuu na barabara za mikoa.
Kiasi hicho cha fedha ambacho ni zaidi ya robo ya
bajeti nzima ya wizara hiyo kwa mwaka, kinatosheleza kujenga barabara
mpya ya lami yenye urefu wa kilometa zipatazo 315, kwa makadirio ya
kilometa moja kugharimu Sh1 bilioni. Katika mwaka huu wa fedha, bajeti
nzima ya Wizara ya Ujenzi ni Sh1.226 trilioni.
Kauli ya Dk Magufuli
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, aliwahi
kunukuliwa akisema ataendelea kusimamia sheria ya barabara namba 30 ya
mwaka 1973, hadi anaingia kaburini kwa kuhakikisha hakuna magari ambayo
yanazidisha uzito na kuharibu barabara.
“Nchini Ujerumani, uzito wa magari yote ni tani
40, Uingereza tani 40, Ufaransa 40, Urusi 38 lakini Tanzania tani 56,
wakati mwingine tunakamata hadi tani 96,” alisema Dk Magufuli.
Hata hivyo, ujasiri wa Dk Magufuli ulizimwa na
amri ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyetengua agizo la waziri huyo na
kuamua kuruhusu magari yenye uzito uliopitiliza kuendelea kutumia
barabara.
Mwananchi
Mwananchi
No comments:
Post a Comment