Thursday, 16 January 2014

Ngono; sifa mpya inayotawala vyuo


Ni jambo la kusikitisha lakini ndiyo ukweli kwamba kuna baadhi ya wenye mamlaka katika shule wanatumia madaraka yao kujipatia ngono kutoka kwa wanafunzi.
Baadhi ya wanafunzi tayari wamenaswa, huku wengine wakiambukizwa virusi vya Ukimwi au kuwa nyumba ndogo; sababu kubwa ni umalaya wa baadhi ya walimu, huku kukiwa na hofu juu ya nini hatma ya hali hii.
Mbaya zaidi ni kwamba mwalimu akiomba uhusiano kwa msichana, akikataa, baadhi yao huwaharibia wanafunzi hao kwa maana ya kuwapa alama mbaya katika mitihani yao, hata kama walifanya vizuri.
Wapo ambao wanashawishiwa na walimu kuingia kwenye ngono, pia wapo wanafunzi wanawashawishi walimu kuanzisha uhusiano nao ili kufanya masomo yawe mepesi.
Uhalisia wenyewe              
Ngono inapandisha alama za kufaulu vyuoni, inamfanya aliye na uwezo mdogo kuwa kinara darasani.
Imefika hatua baadhi ya wanachuo wanajipanga wakati wa mitihani yao, wanamtoa mmoja kafara kwa ajili ya wengine, anashawishiwa akajipendekeze, agawe penzi kwa mwalimu ikibidi ilimradi tu mambo yawe mepesi kwenye mtihani. Staili hii sasa inaitwa ‘kuzima moto’.
Mchezo huu umekuwa maarufu, si kwenye vyuo vingi. Linapotamkwa neno rushwa mara nyingi baadhi ya watu wanayaelekeza mawazo yao kwenye sehemu zinazotoa huduma muhimu kama vile mahakama, hospitali, polisi kutokana na sababu kuwa ni rahisi kuonekana.
Kupenyeza kwa kasi rushwa kwenye sekta ya elimu kunaweza kuelezwa kuwa kunachochea kwa kasi kushuka kwa elimu miongoni mwa wanajamii nchini. Kushuka huko kunaanzia ngazi za chini na katika kwenda ngazi za juu.
Hali hiyo inatia shaka ya kuwepo kwa wataalamu wasio na uwezo. Haya mambo ndiyo yanafanya kuwepo kudharauliwa kwa wasomi wengi siku hivi, na hata maisha ya baadhi ya wasomi yanadhihitisha hilo kwamba wengine elimu haiendani na uhalisia wao.
Lakini ni mara chache sana watuhumiwa wa kutoa au kupokea rushwa hiyo wamekuwa wanakamatwa kwa kuwa sehemu kubwa ya utoaji na upokeaji hufanyika kwa faragha.

Agosti 20, 2007, Mhadhiri wa chuo kikuu kimoja, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu kwa tuhuma za kudai na kupokea rushwa ya Dola za Marekani 1,000 kutoka kwa mwanafunzi wake.
Mshtakiwa aliachishwa kazi na mwajiri wake siku mbili baada ya kufikishwa mahakamani. Hakuna waliofuatilia kesi hiyo hadi mwisho na kama mhadhiri alipatikana na hatia au aliishinda.
Utafiti uliofanywa takriban miaka kumi iliyopita ulibainisha kwamba sekta ya elimu hapa Tanzania, imechafuliwa na rushwa za ngono au fedha.
Msichana anayefanikiwa kuhitimu kwa rushwa za ngono huendeleza dhambi hiyo kupata ajira, vyeo kazini na hatimaye nyadhifa za juu za uongozi. Wanawake waliofanikiwa kwa njia hii wapo wengi katika utumishi serikalini, katika mahakama, vyama vya siasa, Bunge nakadhalika. 
Kinachotafutwa siku hizi na wasomi ni “bora elimu” na siyo “elimu bora”. Wasomi wanajivunia vyeti vya kuhitimu vyuo vikuu hata kama hawana maarifa yoyote ya kuboresha maisha ya binadamu.

No comments:

Post a Comment